93% ya Wamarekani watiwa hofu na mfumko wa juu wa bei
Uchunguzi mpya wa maoni uliofanywa huko Marekani unaonyesha kuwa, mfumko wa bei za bidhaa nchini humo unawatia wasi wasi asilimia 93 ya Wamarekani.
Utafiti wa maoni uliofanywa na shirika la habari la Fox News unaonesha kuwa, asilimia 67 ya Wamarekani walioshiriki kwenye uchunguzi huo wana 'hofu kubwa zaidi' kutokana na ongezeko la kutisha la mfumko wa bei nchini humo.
Aidha utafiti huo umeeleza kuwa, asilimia 25 ya waliohojiwa wana 'wasi wasi sana' kutokana na mfumko wa bei, huko asilimia 52 wakikata tamaa na kusema kuwa hali ya mambo itakuwa mbaya zaidi ndani ya mwaka mpya wa kifedha.
Kulingana na takwimu za Ofisi ya Takwimu za Kazi, mfumko wa bei za bidhaa nchini Marekani uliongezeka hadi 9.1% mwezi Juni, hicho kikiwa ni kiwango cha juu zaidi kuwahi kushuhudiwa katika kipindi cha zaidi ya miaka 40.
Mara ya mwisho mfumuko wa bei kufikia zaidi ya asilimia 9 nchini humo ilikuwa Novemba 1981. Sehemu kubwa ya ongezeko la Juni lilichochewa na kuongezeka kwa bei ya petroli, ambayo imepanda kwa karibu asilimia 60.
Aidha bei za umeme na gesi asilia pia zilipanda kwa asilimia 13.7 na asilimia 38.4 mtawalia, katika kipindi cha miezi 12 kilichomalizika Juni. Kwa ujumla bei za vyakula zilipanda kwa asilimia 12.2 ndani ya mwaka mzima wa kifedha nchini humo.
Uchunguzi mwingine wa maoni uliofanywa hivi karibuni na Jarida la Political na Taasisi ya Morning Consult ulionyesha kuwa, asilimia 60 ya wananchi wa Marekani wanaamini kuwa sera za serikali ya Rais Joe Biden ni sababu kuu ya kuongezeka mfumuko huo mkubwa wa bei nchini humo.