China na Taiwan kwenye mzingo wa mivutano iliyoibuliwa na Washington
https://parstoday.ir/sw/news/world-i86272-china_na_taiwan_kwenye_mzingo_wa_mivutano_iliyoibuliwa_na_washington
Ziara iliyopangwa kufanywa na Spika wa Baraza la Wawakilishi la Marekani na misaada ya silaha Washington kwa Taiwan vimezidisha hali ya wasiwasi katika Bahari ya China.
(last modified 2025-10-11T08:57:00+00:00 )
Jul 25, 2022 11:31 UTC
  • China na Taiwan kwenye mzingo wa mivutano iliyoibuliwa na Washington

Ziara iliyopangwa kufanywa na Spika wa Baraza la Wawakilishi la Marekani na misaada ya silaha Washington kwa Taiwan vimezidisha hali ya wasiwasi katika Bahari ya China.

Baada ya kutangazwa ziara tarajiwa ya Nancy Pelosi, Spika wa Baraza la Wawakilishi la Marekani huko Taiwan, sasa Washington imesema kuna uwezekano wa kutangaza marufuku ya kupaa ndege za China katika eneo hilo. Wakati huo huo, Taipei imedai kuwa ndege nne za kivita na nyingine mbili za upelelezi za China zimeruka katika anga ya Taiwan. 

Uingiliaji kati wa Marekani katika eneo la Asia ya Mashariki hasa katika Bahari ya Uchina, unaripotiwa kuongezeka. Sambamba na msimamo wa Joe Biden wa kuiunga mkono Taiwan dhidi ya China na uwepo wa meli za kivita za Marekani katika Mlango-Bahari wa Taiwan, baada ya kuidhinisha uuzaji wa silaha za kijeshi kwa Taiwan zenye thamani ya dola milioni 108, Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani sasa inapanga ziara ya Nancy Pelosi kisiwani Taiwan. Kauli na hatua hizi za kuchochea mvutano zinaendelea huku Beijing ikiitaka Marekani kuacha mara moja kuingilia mambo ya ndani ya China na kuheshimu mamlaka ya nchi hiyo.

"Wang Wenbin", msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya China amesema kuhusiana na suala hilo kwamba: "Uuzwaji wa silaha za Marekani kwa Taiwan unadhoofisha mamlaka na maslahi ya kiusalama ya China na una athari mbaya kwa usalama na amani ya Mlango-Bahari wa Taiwan na uhusiano kati ya nchi hizo mbili. Kwa msingi huo, China Itaendelea kuchukua hatua madhubuti katika kutetea mamlaka na maslahi ya usalama wake."

Wang Wenbin

Baada ya kuanzishwa uhusiano rasmi kati ya Jamhuri ya Watu wa China na Marekani mwaka 1979, Bunge la nchi hiyo lilipitisha sheria ya msaada wa kijeshi kwa Taiwan, kwa kuzingatia uamuzi wa Rais na Bunge, ambayo ulijulikana kama "Policy of Strategic Ambiguity". Lakini sasa, kutokana na Marekani kuachana na sheria hiyo na kuingilia moja kwa moja na waziwazi masuala ya Taiwan kupitia ziara za viongozi wa nchi hiyo huko Taiwan na msimamo wa Rais Joe Biden kuhusu kadhia hiyo, ikiwa ni pamoja na uuzaji wa silaha na zana za kijeshi kwa Taipei, inaonekana kuwa Mlango-Bahari wa Taiwan na Bahari ya China Kusini vimegeuka na kuwa ghala kubwa la baruti linaloweza kulipuka wakati wowote.

David M. Lampton, mkurugenzi wa utafiti wa China katika Chuo Kikuu cha Johns Hopkins nchini Marekani, anasema waziwazi kwamba: "Uhusiano kati ya China na Marekani uko katika hali mbaya zaidi tangu kabla ya ziara ya Nixon na Kissinger nchini China mwanzoni mwa miaka ya 1970. Ingawa Taiwan ina umuhimu wa kimkakati kwa Marekani, lakini Washington haina wajibu wa kuilinda moja kwa moja Taiwan, na Sheria ya Mahusiano na Taiwan ya 1979 inaiwajibisha Marekani kuiuzia Taiwan silaha tu na si vinginevyo."

Suala la Taiwan sasa linatumiwa na Washington kama sehemu ya mikakati ya Marekani ya kuziburuta nchi kama Japan, Korea Kusini, na Australia katika mzingo wa sera za Marekani na kuhalalisha uwepo wa majeshi ya serikali ya Washington katika eneo la Pasifiki.

Lakini kutokana na kuongezeka kwa nguvu za kiuchumi na kijeshi za China katika ushindani wake na Marekani na kupata nguvu zaidi msimamo wa Beijing kuhusu kurejesha mamlaka ya kisiwa cha Taiwan, Washington inataka kuishughulisha China na masuala ya kimkakati na kijiopolitiki, na kuzidisha mivutano katika eneo hilo kupitia njia ya kufanya mazoezi ya kijeshi angani na majini karibu wa mipaka ya China na kutoa misaada mbalimbali kwa Taipei. Kuhusiana na hilo, Liu Jieyi, mkuu wa Idara ya Masuala ya Taiwan nchini China, anasema: "China inapendelea amani kuliko mizozo huko Taiwan, na iwapo eneo hilo litaungwanishwa tena na China, Beijing itatekeleza sera ya "nchi moja na mifumo miwili", na nguvu ya China itaifaidisha Taiwan."

Kwa mukhtasari tunaweza kusema kuwa, kwa kuzingatia mamlaka ya nchi hiyo katika kisiwa cha Taiwan, China inalitambua eneo la njia ya majini na Mlango-Bahari wa Taiwan kuwa ni eneo lake la baharini na inafanya jitihada za kuzuia harakati na uchochezi wa Marekani katika eneo hilo.

Wakati huo huo inaonekana kuwa, Taipei inataka kufuata nyayo za Ukraine na kupata uungwaji mkono zaidi kutoka kwa Merekani na nchi za Magharibi kwa ujumla kupitia sera ya kuzua taharuki. Hata hivyo China imechukua stratijia ya kujiepusha na mizozano hiyo sambamba na kuzidisha jitihada za kurejesha mamlaka yake katika kisiwa cha Taiwan.