China yafanya maneva ambayo hayajawahi kushuhudiwa karibu na Taiwan
China imefyatua makombora kadhaa ya balestiki kuelekea maji yanayoizunguka Taiwan katika mazoezi makubwa ya kijeshi kuwahi kushuhudiwa, likiwa ni jibu kwa ziara iliyofanywa na Spika wa Baraza la Wawakilishi la Marekani Nancy Pelosi katika kisiwa hicho.
Shirika rasmi la habari la China limesema, mazoezi hayo ya kijeshi yanayofanyika katika maeneo sita yaliyo karibu na Taiwan yataendelea hadi siku ya Jumapili.
Msemaji wa jeshi la China katika kamandi ya mashariki Kanali Mwandamizi Shi Yi ameeleza katika taarifa kwamba, vikosi vya makombora vya jeshi vimefyatua makombora kadhaa yaliyolenga eneo la mashariki ya pwani ya Taiwan.
Kanali Yi amesema, makombora hayo yote yalilenga shabaha kwa usahihi na akaongeza kwamba lengo la luteka hiyo iliyoanza leo ni kufanyia majaribio umakini wa makombora na uwezo wa kumzuia adui asijaribu kufika au kulidhibiti eneo hilo.

Wizara ya ulinzi ya Taiwan imesema jeshi la China limefyatua makombora ya balestiki aina ya Dongfeng katika maji ya kaskazini mashariki na kusini mashariki ya kisiwa hicho wakati wa mchana wa leo kwa saa za huko. Kwa mujibu wa wizara hiyo, makombora mawili yalifyatuliwa karibu na visiwa vidogo vya Taiwan vya Matsu vilivyoko kando ya pwani ya China.
Wizara ya ulinzi ya Taiwan imelaani mazoezi hayo ya kijeshi yaliyofanywa na China ikisema ni "hatua zisizo za busara ambazo zinadhoofisha amani ya eneo."
Mara ya mwisho China ilifyatua makombora kuelekea maji ya kisiwa cha Taiwan mwaka 1996 wakati wa duru ya pili ya uchaguzi uliomweka tena madarakani rais wa kisiwa cha Taiwan wakati huo Lee Teng-hui, ambaye mwaka mmoja kabla yake alifanya ziara nchini Marekani.
Beijing, ambayo ilikuwa imetishia kwamba safari ya Pelosi Taiwan itakuwa na matokeo mabaya, inasisitiza kuwa Taiwan ni sehemu ya ardhi kuu ya China na haijafuta uwezekano wa kutumia nguvu za kijeshi ili kushika hatamu za udhibiti wa kisiwa hicho.../