UN yasikitishwa na hatua ya DRC kumtimua msemaji wa MONUSCO
(last modified Fri, 05 Aug 2022 01:14:42 GMT )
Aug 05, 2022 01:14 UTC
  • UN yasikitishwa na hatua ya DRC kumtimua msemaji wa MONUSCO

Umoja wa Mataifa umekosoa vikali hatua ya serikali ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo ya kumfukuza nchini humo msemaji wa kikosi cha kulinda amani cha Umoja wa Mataifa MONUSCO.

MONUSCO imesema katika taarifa kuwa, imesikitishwa na hatua hiyo ya DRC ya kumtaka Mathias Gillmann, Msemaji wa kikosi hicho cha UN aondoke nchini humo haraka iwezekanavyo, ikimlaumu kwa kuchochea hali ya wasiwasi iliyopeleka kuzuka mauaji ya kutisha wiki iliyopita.

Taarifa hiyo imesisitiza kuwa, kikosi hicho cha kulinda amani kina nia ya kweli ya kuendelea kushirikiana na Wakongomani na mamlaka za nchi hiyo, ili kutekeleza jukumu kilichopewa na Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa.

Watu 36 waliuawa wiki iliyopita wakiwemo askari wanne wa kulinda amani wa Umoja wa Mataifa wakati mamia ya wananchi walipomiminika mabarabarani na kuchoma moto majengo ya MONUSCO na maeneo mengine mbalimbali ya mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo.

Maandamano ya Wakongamani dhidi ya askari wa MONUSCO

Kikosi cha MONUSCO kimepangiwa kuondoka DRC mwaka 2024 lakini serikali ya Kongo inataka askari hao waondoke haraka zaidi nchini humo kutokana na kuongezeka malalamiko ya wananchi. Hayo ni kwa mujibu wa Waziri wa Mambo ya Nje wa DRC, Christophe Lutundula.

Mara kwa mara wananchi wa Kongo DR wamekuwa wakiandamana kulalamikia kikosi hicho cha kulinda amani cha Umoja wa Mataifa kwa kushindwa kuwalinda katika kipindi cha miongo miwili cha kuweko kwao nchini humo, na kila leo mauaji ya raia yanaendelea kufanywa na magenge yenye silaha hasa katika maeneo ya mashariki mwa DRC.

 

Tags