Makumi ya wahajiri wahofiwa kufa maji wakielekea Italia
Makumi ya wahajiri wanahofia kuaga dunia baada ya boti yao kuzama wakijaribu kuelekea Italia.
Mamlaka za Ugiriki zimetangaza kuwa, operesheni ya uokozi na kusaka miili ya wahajiri waliokufa maji kwenye mkasa huo katika kisiwa cha Karpathos inaendelea.
Gadi ya Pwani ya Ugiriki imesema leo Jumatano kuwa, boti iliyozama yapata kilomita 61 mashariki mwa kisiwa cha Karpathos, ilikuwa imebeba wahajiri baina ya 60 na 80.
Habari zaidi zinasema kuwa, mpaka sasa wahajiri 29 (wote wanaume) wameokolewa, na kwamba aghalabu yao ni raia kutoka nchi za Afghanistan, Iraq na Iran.
Manusura wanasema boti hiyo ilikuwa imetokea mji wa Pwani wa Antalya, kusini mwa Uturuki, na ilikuwa inaelekea nchini Italia kabla ya kupinduka.
Hatima ya wahajiri hao waliookolewa haijulikani kwa kuwa Bunge la Ugiriki hivi karibuni lilipiga marufuku wakimbizi kuingia kwenye fukwe za baharini za nchi hiyo.
Hatua hiyo ya Bunge la Ugiriki iliyakasirisha mno makundi ya haki za binadamu, mashirika ya misaada na vyama vya upinzani.