Ukame watishia kuzuka mapigano ya wenyewe kwa wenyewe nchini Uhispania
Ukame unaendelea kusini mwa nchi ya Ulaya ya Uhispania. Ukame huo umepelekea kukauka maji katika maeneo hayo, njaa na kupungua kipato cha wakazi wake ambao wanategemea sana kilimo na utalii. Ukame huo umezusha wasiwasi pia wa kutokea vita vya ndani baina ya jamii za watu mbalimbali wa nchi hiyo.
Shirika la habari la IRNA limeripoti habari hiyo na kuongeza kuwa, kupungua kiwango cha maji kusini mwa Uhispania kumezusha hofu ya kutokea mapigano ya wenyewe kwa wenyewe. Hata hivi sasa pia wakazi wa maeneo hayo wanalalamikia ugumu wa maisha yao kutokana na kubanwa sana katika matumizi ya maji. Hatua hizo za serikali zimewasababishia matatizo mengi wananchi hao wa kusini mwa nchi hiyo ya Ulaya.
Kipato kikubwa cha eneo la Málaga la kusini mwa Uhispania kinatokana na utalii. Kupungua maji kumevuruga mahusiano ya watu kwani wanaharakati wa mazingira wanawalaumu wakulima kwa kutumia maji kupita kiasi ili wapate mazao mwengi zaidi lakini wakulima wanapinga madai hayo.
Kiwango cha maji ya Ziwa Viñuela ambalo ni moja ya maziwa makubwa zaidi ya kusini mwa Uhispania kimeshuka mno na kuna hatari ya kukauka kabisa na bila ya shaka yoyote jambo hilo linawaathiri moja kwa moja wakazi wa eneo hilo ambao wanategemea sana utalii na kilimo.
Ripoti zinasema kuwa, kiwango cha joto kimepanda sana mwaka huu wa 2022 na kukausha vibaya maji ya Ziwa Viñuela kwa asilimia 12. Kwa mujibu wa ripoti hizo, ukame wa mwaka huu ulioikumba nchi hiyo ya Ulaya haujawahi kutokea katika kipindi cha miaka 1,200 iliyopita. Uhispania si nchi pekee ya Ulaya iliyoathiriwa vibaya na ukame.