Marekani yawataka raia wake waondoke haraka Ukraine
https://parstoday.ir/sw/news/world-i87358-marekani_yawataka_raia_wake_waondoke_haraka_ukraine
Marekani imewataka raia wake waondoke nchini Ukraine haraka iwezekanvyo, huku kukiwa na wasiwasi wa Russia kuanza kuushambulia mji mkuu wa nchi hiyo, Kiev.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Aug 23, 2022 23:49 UTC
  • Marekani yawataka raia wake waondoke haraka Ukraine

Marekani imewataka raia wake waondoke nchini Ukraine haraka iwezekanvyo, huku kukiwa na wasiwasi wa Russia kuanza kuushambulia mji mkuu wa nchi hiyo, Kiev.

Marekani inadai kuwa, Russia inajiandaa kuanza kushambulia majengo ya serikali na miundombinu katika mji mkuu wa Ukraine, Kiev ndani ya siku chache zijazo.

Marekani ilitoa indhari hiyo kwa raia wake walioko Ukraine jana Jumanne, wakati huu ambapo operesheni maalumu ya kijeshi ya Russia katika hiyo ya Ulaya Mashariki ikiingia katika mwezi wake wa saba.

Serikali ya Ukraine imepiga marufuku mikusanyiko ya watu jijini Kiev leo Jumatano. Wananchi wa Ukraine walikuwa wamepanga kukusanyika kwa ajili ya hafla za maadhimisho ya kumbukumbu ya uhuru kutoka utawala wa Sovieti.

Mashambulio ya makombora nje ya Kiev

Viongozi wa nchi mbalimbali duniani walitazamiwa kukusanyika mjini Kiev jana na leo Jumatano, katika hafla iliyopewa jina la 'Jukwaa la Crimea' lakini mikusanyiko imefutwa. Viongozi wa Kiev wamesema hafla hizo sasa zitafanyika kwa njia intaneti.

Moscow ilianzisha operesheni hiyo maalumu nchini Ukraine mnamo Februari 24, kwa lengo la kuizuia nchi hiyo isiendelee kujitanua kuelekea upande wa mashariki, kwa madhara ya usalama wa Russia.