Russia: Ukraine imekiri kuwa na mpango wa kuunda bomu la atomiki
https://parstoday.ir/sw/news/world-i87652-russia_ukraine_imekiri_kuwa_na_mpango_wa_kuunda_bomu_la_atomiki
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Russia amesema, serikali ya Ukraine imekiri kuwa na mpango wa kuunda bomu la atomiki na katu haijawahi kuficha kwamba ilikuwa ikijiandaa kwa ajili ya kukabiliana kijeshi na Russia.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Aug 31, 2022 21:54 UTC
  • Russia: Ukraine imekiri kuwa na mpango wa kuunda bomu la atomiki

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Russia amesema, serikali ya Ukraine imekiri kuwa na mpango wa kuunda bomu la atomiki na katu haijawahi kuficha kwamba ilikuwa ikijiandaa kwa ajili ya kukabiliana kijeshi na Russia.

Kwa mujibu wa shirika la habari la Fars, Maria Zakharova, msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Russia ameeleza hayo katika mkutano wa kila wiki na waandishi wa habari jana Jumatano, alipoashiria kukiri kwa serikali ya Ukraine kwamba ilikuwa ikifanya jitihada za kutengeneza bomu la atomiki, na akabainisha kuwa, vikosi vya Ukraine vinakilenga kinu cha nyuklia cha Zaporizhzhia kwa kutumia silaha vilizopokea kutoka Magharibi.
Mwanadiplomasia huyo wa Russia ameongezea kwa kusema, misaada ya silaha inayotolewa na Magharibi kwa Ukraine inarefusha tu muda wa vita na kuongeza kiwango cha maafa.
Maria Zakharova

Katika mkutano wake huo wa kila wiki na waandishi wa habari, Zakharova amesisitiza kuwa, Umoja wa Ulaya unapuuza hatari zinazosababishwa na kulengwa kwa kinu cha nyuklia cha Zaporizhzhia na vikosi vya Ukraine.

Aidha, ameashiria ziara ya ujumbe wa Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki nchini Ukraine, na kueleza kwamba ziara ya wakaguzi hao kwenye kinu cha nyuklia cha Zaporizhzhia itafichua ukweli kuhusu vitendo vya uchochezi vya Ukraine.
Maria Zakharova ameeleza pia kuwa kuongezeka mivutano kuhusiana na kinu cha nyuklia cha Zaporizhzhia kunasababisha wasiwasi mkubwa, na hii ni katika hali ambayo wakaguzi wa Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki walitarajiwa kuanza ukaguzi wao katika kinu hicho cha nyuklia jana Jumatano.
Mnamo mwezi Machi, vikosi vya jeshi la Russia vilikiteka kinu cha nyuklia cha Zaporizhzhia, ambacho kinahesabiwa kuwa kinu kikubwa zaidi cha nguvu za nyuklia barani Ulaya.
Kiwanda hicho ambacho hakiko mbali na mstari wa mbele wa mapigano nchini Ukraine, kimeshambuliwa kwa makombora mara kadhaa katika wiki za hivi karibuni, na kuzidisha wasiwasi wa kutokea maafa ya nyuklia.../