Seneta Murray: Demokrasia ipo hatarini nchini Marekani
https://parstoday.ir/sw/news/world-i87834-seneta_murray_demokrasia_ipo_hatarini_nchini_marekani
Seneta Patty Murray wa Marekani amesema kwamba demokrasia ya nchi hiyo imo hatarini, huku akitetea hotuba tata iliyotolewa na Rais Joe Biden wiki iliyopita.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Sep 05, 2022 21:44 UTC
  • Seneta Murray: Demokrasia ipo hatarini nchini Marekani

Seneta Patty Murray wa Marekani amesema kwamba demokrasia ya nchi hiyo imo hatarini, huku akitetea hotuba tata iliyotolewa na Rais Joe Biden wiki iliyopita.

Seneta Murray alisema hayo jana Jumapili katika mahojiano na kanali ya CNN na kuongeza kuwa, wafuasi wa rais wa zamani wa nchi hiyo Donald Trump, walikuwa tayari kutumia nguvu kupita kiasi kusimamisha ukabidhianaji wa amani wa madaraka mnamo Januari 6 mwaka jana.

Amebainisha kuwa: Naamini kuwa demokrasia yetu ipo hatarini hii leo. Nilikuwepo katika jengo la Kongresi mnamo Januari 6, nilishindwa kukimbia (vurugu zilipoanza). 

Seneta huyo ameendelea kusema kuwa: Nilifungiwa ofisini (vurugu zikiendelea), na niliwasikia wafuasi waliochochewa na Trump wakiushambulia mlango, wakisema kuwa wapo tayari kutumia nguvu kuteka taifa hili.

Kongresi ya US ilishambuliwa Januari 6

Mapema mwaka huu pia, Rais wa zamani wa Marekani alikiri pia kwamba, demokrasia ya nchi hiyo imo hatarini. Barack Obama aliashiria shambulizi lililofanywa na wafuasi wa Donald Trump dhidi ya jengo la Kongresi ya nchi hiyo na kusema kwamba demokrasia iko hatarini zaidi hii leo kuliko ilivyokuwa mwaka mmoja uliopita.

Kabla ya hapo pia, rais wa zamani wa Marekani Jimmy Carter alionya kwamba, demokrasia kote nchini humo iko hatarini na kwamba watu wa Marekani sasa wako kwenye ukingo unaopanuka kila siku wa kuangamia.