Iran yazitaka pande zote kutekeleza JCPOA ipasavyo
https://parstoday.ir/sw/news/world-i8794-iran_yazitaka_pande_zote_kutekeleza_jcpoa_ipasavyo
Mjumbe wa Iran katika Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki IAEA amezitaka pande husika kutekeleza kwa irada thabiti makubaliano ya nyuklia kati ya Iran na kundi la 5+1.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Jun 08, 2016 23:05 UTC
  • Iran yazitaka pande zote kutekeleza JCPOA ipasavyo

Mjumbe wa Iran katika Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki IAEA amezitaka pande husika kutekeleza kwa irada thabiti makubaliano ya nyuklia kati ya Iran na kundi la 5+1.

Akihutubia mkutano wa Bodi ya Magavana ya IAEA jana Jumatano, Reza Najafi, Balozi wa Iran katika wakala huo amesema pande zote zina jukumu la kutekeleza makubaliano hayo ya Vienna yajulikanayo kama Utekelezaji wa Mpango wa Pamoja wa Utekelezaji (JCPOA) kwa vitendo na sio tu kwa maneno matupu na kutoa taarifa. Mjumbe huyo wa Iran katika wakala wa IAEA aidha ameizitaka nchi za kundi la 5+1 kujiepusha na vitendo vinavyoweza kuyumbisha na kukwamisha mchakato wa kutekelezwa makubaliano hayo, yaliyofikiwa Julai mwaka jana na kuanza kutekelezwa Januari mwaka huu. Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imekuwa ikilalamikia mwendo wa kinyonga wa utekelezaji wa makubaliano ya nyuklia ya Vienna, licha ya IAEA kuthibitisha kuwa Tehran haijakengeuka mkondo wa makubaliano hayo.

Aprili mwaka huu, Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki IAEA kwa mara nyingine tena ulitoa ithibati kuwa serikali ya Tehran inatekeleza barabara makubaliano ya nyuklia yaliyofikiwa kati yake na kundi la 5+1 Julai mwaka jana 2015.

Ni vyema kuashiria hapa kuwa, Disemba mwaka jana, Bodi ya Magavana ya Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki (IAEA) ilipitisha kwa kauli moja azimio la kufunga faili la nyuklia la Iran baada ya kubaini kwamba miradi ya nyuklia ya taifa hili ni ya amani na haijawahi kuchukua mkondo wa kijeshi. Wanachama 35 wa bodi hiyo walisema baada ya Iran kutoa majibu ya kuridhisha kuhusiana na miradi yake ya nyuklia, IAEA imeamua kufunga faili hilo lililofunguliwa miaka 12 iliyopita.