Utafiti: Akthari ya Wamarekani wanasema Biden ameligawa taifa
Aghalabu ya wapigakura nchini Marekani wanaamini kuwa, Rais Joe Biden wa nchi hiyo amewagawa Wamarekani katika utawala wake, badala ya kuwaunganisha.
Utafiti uliofanywa na jumuiya ya Convention of States unaonesha kuwa, asilimia 58.7 ya wapigakura walioshiriki kwenye utafiti huo wanaitakidi kuwa, Biden ameligawa taifa hilo, huku asilimia 20.6 pekee wakiamini kuwa amewaunganisha na kuwaleta pamoja wananchi wa nchi hiyo.
Asilimia 92.8 ya wafuasi wa chama cha Republican walioshirikishwa kwenye utafiti huo wa maoni wanaona kuwa, Biden ameshindwa kutekeleza ahadi aliyoitoa wakati wa kampeni ya kuwaunganisha Wamarekani.
Haya yanajiri siku chache baada ya utafiti mwingine uliotolewa Jumatatu iliyopita na shirika la Trafalgar kuonesha kuwa, Biden amevunja rekodi ya kushuka umashuhuri wake baina ya Wamarekani.
Utafiti huo unasema kuwa, umaarufu wa Biden umeshuka hadi kiwango cha chini kabisa na kufikia asilimia 39. Kiwango cha kuporoka umashuhuri na kiongozi huyo wa Marekani hakijashuhudiwa tena tangu mwaka 1974 katika kipindi cha utawala wa Richard Nixon.
Aidha utafiti uliofanywa mapema mwezi huu na Yahoo News ulifichua kuwa, asilimia 60 ya Wamarekani, nusu wakiwa ni wafuasi wa chama cha Democrats wanaitakidi kuwa, Marekani ipo katika mkondo mbaya na inaelekea kusiko.
Serikali ya Biden inakabiliwa na migogoro inayoongezeka katika uwanja wa sera za kigeni na uchumi, migogoro ambayo inaweza kuutumbukiza uchumi wa Marekani katika mdororo mkubwa.