Kusambaratika siasa za vikwazo; Marekani yapigia magoti mafuta ya Venezuela
(last modified Tue, 29 Nov 2022 02:27:59 GMT )
Nov 29, 2022 02:27 UTC
  • Kusambaratika siasa za vikwazo; Marekani yapigia magoti mafuta ya Venezuela

Baada ya kupita takriban miaka 10 ya vikwazo vikali vya Marekani dhidi ya Venezuela, hatimaye Washington imesalimu amri na imeamua kupigia magoti mafuta ya Venezuela.

Marekani na waitifaki wake wakiwemo pia vibaraka wa ndani ya Venezuela, waliweka mashinikizo ya juu kabisa dhidi ya serikali ya Caracas kwa shabaha ya kuipindua serikali hiyo na kupandikiza mfumo kibaraka wa kisiasa nchini humo. Lakini sasa, siasa zimebadilika kimataifa hasa kutokana na vita vya Ukraine. Nchi za Magharibi ikiwemo Marekani zinahaha hivi sasa kutafuta sehemu ya kufidia hasara zilizosababishwa na vita hivyo hasa upande wa nishati. Zimehisi kuwa, mafuta ya nchi kama Venezuela, ndiye mwokozi wao.

Hayo yamekuja baada ya Wizara ya Hazina ya Marekani kulipa shirika la Chevron, kibali cha miezi sita cha kununua mafuta na bidhaa za mafuta kutoka nchini Venezuela ambayo ni moja ya nchi tajiri sana kwa mafuta katika eneo la Amerika ya Latini licha ya kwamba kwa miaka mingi nchi hiyo iko chini ya mashinikizo makubwa ya Marekani na waitifaki wake. 

Rais Nicolás Maduro wa Venezuela

Kwa muda mrefu, nchi za Magharibi zikiongozwa na Marekani zimefanya njama za kila namna za kujaribu kuipindua serikali ya Venezuela au kuilazimisha ibadilishe misimamo yake na iwe kibaraka wa nchi hizo za Ulaya na Marekani, lakini zimeshindwa. Pamoja na kuweko mashinikizo yote hayo, lakini serikali ya Caracas miaka yote hiyo haikutetereka katika jitihada zake za kujiletea maendeleo kiasi kwamba katika miezi ya hivi karibuni, uchumi wa nchi hiyo umestawi kwa namna ambayo hata maadui wamelazimika kukiri uhakika huo. Rais wa Nicolás Maduro wa Venezuela alitangaza rasmi hivi karibuni kwamba, baada ya miaka minne ya mfumuko wa bei uliotokana na vikwazo vya Marekani, hatimaye Venezuela imerejea kwenye ustawi wake wa kiuchumi.

Kama tunavyojua, sasa hivi dunia imekumbwa na mgogoro mkubwa wa nishati. Nchi za Marekani na Ulaya zimejitia kwenye shimo la mgogoro huo kwa kuiwekea vikwazo vya kila namna Russia kwa kisingizio cha vita vya Ukraine. Hivi sasa lakini nchi hizo za Magharibi zimekiri kuwa haziwezi kuhimili mgogoro wa kukosa nishati, hivo zimeamua kubadilisha siasa zao kuhusu Venezuela. Russia kwa upande wake, imeamua kupunguza mno kuziuzia gesi nchi za Magharibi isipokuwa kwa masharti yaliyowekwa na Moscow, kama kununua nishati kwa sarafu ya Ruble ya Russia. Nchi nyingi hasa za Ulaya zimekumbwa na migogoro mikubwa ya kijamii na kiuchumi kutokana na uhaba wa nishati, huku msimu wa baridi kali ukiwa ndio umeingia tena. Hali hiyo imezilazimisha nchi hizo ikiwemo Marekani kubadilisha siasa zao na kwa hivi sasa Wizara ya Hazina ya Marekani imeamua kutoa kibali cha kuingiza mafuta kutoka Venezuala. Mbali na kibali hicho, shirika la uchimbaji mafuta la San Ramon lenye makao yao makuu huko California, nalo limepewa kibali cha kuingiza mafuta ghafi nchini Marekani kutokea Venezuela. Kibali hicho kilikuwa kimefutwa tangu mwaka 2019. 

Rais wa Marekani, Joe Biden

 

Mbali na vibali hivyo viwili, hivi sasa pia kuna mazungumzo yanaendelea baina ya timu ya mazungumzo ya serikali ya Venezuela na wapinzani baada ya kufanyika vikao visivyo rasmi miezi kadhaa iliyopita. Norway ndiye mpatanishi katika mazungumzo hayo. Inavyotarajiwa ni kuwa mazungumzo hayo yataishia kwenye kupunguzwa vikwazo vya mafuta vya Marekani dhidi ya Venezuala. Hayo yanajiri katika hali ambayo gazeti la Miami Herald la Marekani limefichua uhakika mwingine mchungu kwa wapinzani wa Venezurla. Limeandika: "Hivi sasa inaonekana wazi kuwa, Juan Guaidó, mkuu wa wapinzani wa serikali ya Venezuela, ameshapoteza uungaji mkono wa Washington." Ikumbukwe kuwa, huko nyuma, Marekani ilimpandisha juu Juan Guaidó kiasi cha kudai kuwa yeye ndiye rais wa Venezuela, njama ambazo lakini, hazikufua dafu mbele ya msimamo imara wa wananchi wa Venezuela na viongozi wao.

Ukweli ni kuwa hivi sasa Washington inafanya juhudi za kuingiza tena mafuta ya Venezuela kwa gharama yoyote ile. Ijapokuwa viongozi wa Marekani hawajakiri kushindwa na kufeli siasa zao za vikwazo dhidi ya Venezuela na hata hawatarajiwi kuwa kuna siku watakiri, lakini kufeli siasa hizo za kibeberu za Marekani kuko wazi kwa kila anayefuatilia matukio ya eneo hilo. Rais Nicolás Maduro wa Venezuela ametangaza wazi kuwa dunia haiwezi kutawaliwa na kambi moja, bali mfumo wa kambi kadhaa umeshazaliwa duniani na misimamo ya kuhakikisha nchi zote zina sauti sawa na zinapata haki zao zinazostahiki, itaendelea kupata nguvu siku baada ya siku.

Tags