China: Marekani isiitumie Afrika katika michezo yake ya kijiopolitiki
https://parstoday.ir/sw/news/world-i91632-china_marekani_isiitumie_afrika_katika_michezo_yake_ya_kijiopolitiki
Balozi wa China nchini Marekani amepinga madai ya Washington kuwa nchi za Afrika zimenasa kwenye mtego wa Beijing kutokana na madeni.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Dec 13, 2022 03:29 UTC
  • China: Marekani isiitumie Afrika katika michezo yake ya kijiopolitiki

Balozi wa China nchini Marekani amepinga madai ya Washington kuwa nchi za Afrika zimenasa kwenye mtego wa Beijing kutokana na madeni.

Qin Gang alisema hayo jana Jumatatu mjini Washington, kuelekea mkutano wa Marekani na Afrika na kusisitiza kuwa, Washington inapaswa kuacha kulitumia bara la Afrika katika michezo yake ya kijiopolitiki.

Gang ameeleza kuwa, madai ya Marekani kwamba China imezitumbukiza nchi za Afrika katika lindi la madeni hayana msingi wowote, kwani nchi za bara hilo zina madeni mara tatu zaidi kwenye taasisi za kifedha za Magharibi, ukilinganisha na China.

Mwanadiplomasia huyo wa ngazi ya juu wa China ameeleza bayana kuwa, "Uwekezaji na misaada ya kifedha ya China kwa Afrika sio mtego. Ni kwa maslahi (ya pande mbili)."

Rais Xi Jinping wa China katika mkutano wa viongozi wa Afrika kwa njia ya intaneti mwaka jana

Rais Joe Biden anatazamiwa kuwa mwenyeji wa Kongamano la Marekani-Afrika wiki hii mjini Washingto DC, hii ikiwa ni mara ya kwanza kwa mkutano kama huu kufanyika tangu mwaka 2014 wakati wa utawala wa Barack Obama.

Marais na viongozi 50 wa nchi za Afrika wanatazamiwa kushiriki mkutano huo ambao wadadisi wa mambo wanasema kuwa, Marekani inataka kuutumia kujikurubisha kwa Afrika, ikihofia ushindani mkali kutoka China na Russia.