Russia yatungua makombora ya Marekani ya HARM
https://parstoday.ir/sw/news/world-i91906-russia_yatungua_makombora_ya_marekani_ya_harm
Russia imesema vikosi vyake vya ulinzi wa anga vimefanikiwa kutungua makombora manne yaliyotengenezwa na Marekani ya HARM, katika anga ya eneo la Belgorod.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Dec 20, 2022 03:53 UTC
  • Russia yatungua makombora ya Marekani ya HARM

Russia imesema vikosi vyake vya ulinzi wa anga vimefanikiwa kutungua makombora manne yaliyotengenezwa na Marekani ya HARM, katika anga ya eneo la Belgorod.

Taarifa iliyotolewa jana Jumatatu na Igor Konashenkov, Msemaji wa Wizara ya Ulinzi ya Russia imeeleza kuwa, makombora manne aina ya AGM-88 High-speed Anti-Radiation Missiles (HARM) ya Marekani yametunguliwa katika anga ya eneo la Belgorod, yapata kilomita 40 kaskazini mwa mpaka wa Russia na Ukraine ndani ya saa 24 zilizopita.

Duru za habari zinaarifu kuwa, serikali ya Washington ilituma nchini Ukraine makombora ya aina hiyo katikati ya mwezi Agosti mwaka huu 2022.

Makombora hayo yaliyozalishwa na Marekani yameripotiwa kuvurumishwa kutoka kwenye ndege za kivita za Ukraine za MiG-29 na Su-27.

Silaha za Wamagharibi zilizopelekwa Ukraine

Gavana wa eneo la Belgorod amesema kwa akali mtu mmoja alipoteza maisha huku kadhaa wakijeruhiwa juzi Jumapili katika mashambulio ya makombora ya Ukraine katika eneo hilo.

Haya yanajiri siku chache baada ya serikali ya Russia kutangaza kuwa, uamuzi wa Jeshi la Nchi za Magharibi NATO wa kuipa Ukraine mfumo wa kujilinda kwa makombora wa Patriot umechukuliwa kwa lengo la kuishambulia Russia na hiyo ina maana ya kuihalalishia Moscow kuzishambulia nchi wanachama wa NATO.