EU na mikakati mipya nchini Mali ya kuzuia wahamiaji haramu
Umoja wa Ulaya umesema unatekeleza mikakati huko Mali kwa lengo la kuzuia kuendelea wimbi la wahamiaji haramu kuelekea Ulaya.
Mjumbe wa Umoja wa Ulaya nchini Mali amesema kuwa umoja huo unajiandaa kutekeleza mipango miwili kwa bajeti ya yuro milioni 41 na laki sita lengo likiwa ni kudhamini usalama na amani katika maeneo ya kaskazini mwa Mali. Hatua hiyo inatekelezwa na Umoja wa Ulaya ili kukomesha wahamiaji haramu kuelekea katika nchi za Ulaya.
Ripoti ya Umoja wa Ulaya imeeleza kuwa bajeti hiyo itatoka katika mfuko wa fedha za dharura kama ilivyoafikiwa katika kikao cha mwezi Septemba mwaka jana huko Malta.
Mkakati wa kwanza wa bajeti ya yuro milioni 29 utatekelezwa katika maeneo ya Mopti na Gao ili kuimarisha usalama wa mipakani na kuandaa uwanja wa kutambuliwa na kukamatwa magenge yanayohusika na uvushaji wa wahamiaji haramu na wale wanauza viungo vya binadamu. Mkakati wa pili wa Umoja wa Ulaya pia utatekelezwa kupitia makundi ya radiamali za haraka na kuimarisha ulinzi wa mipakani katika eneo la Sahel la Afrika.