Jan 20, 2023 12:31 UTC
  • Lavrov: NATO iko vitani na Russia kupitia Ukraine

Sergey Lavrov, Waziri wa Mambo ya Nje wa Russia amesema kuwa muungano wa kijeshi wa NATO uko vitani na nchi hiyo kupitia Ukraine. Ameongeza kuwa: "Kinachotokea Ukraine ni matokeo ya maandalizi ya Marekani ya vita vya mseto dhidi ya Russia." Ameisitiza kuwa Umoja wa Ulaya umepoteza uhuru wake na sasa uko chini ya satwa ya Marekani moja kwa moja.

Lavrov ameendelea kusema kwamba, mgogoro wa Ukraine ulianza muda mrefu kabla ya operesheni maalum ya kijeshi ya Russia Februari mwaka jana. Ameongeza kuwa, "kulikuwa na ripoti za Benki ya Dunia na Shirika la Chakula Duniani ambazo zilitolewa kabla ya kuanza kwa operesheni ambazo zilibaini kwamba hatua za Marekani na washirika wake ndio sababu ya msukosuko wa kiuchumi duniani."

Huku akiashiria jaribio la nchi za Magharibi la kuzuia kuibuka ulimwengu wenye pande kadhaa za kuchukua maamuzi, Lavrov amesema: "Wakati Marekani inapohisi  kuwa usalama wake uko hatarini katika kona yoyote ya dunia, hutupilia mbali kanuni na sheria na kuchukua hatua bila kupata makubaliano yoyote."

Sisitizo la  Lavrov kuhusu vita vya niaba vya NATO vinavyoongozwa na Marekani dhidi ya Russia kupitia Ukraine ni muhimu hasa kwa kuzingatia mtazamo wa kivita wa Wamagharibi na muendelezo wa kutuma aina mbalimbali za zana za kijeshi na silaha nchini Ukraine.

Tangu kuanza vita nchini Ukraine, Marekani imetoa msaada wa kijeshi wa takriban dola bilioni 22 kwa Ukraine. Uingereza ambayo ilitoa pauni bilioni 2.3 kwa Ukraine mwaka 2022, ilitangaza wakati huo huo kutuma msaada mpya wa silaha kwa Ukraine mwaka 2023 ambapo imepanga kuipa serikali ya Kiev dola bilioni 2.77. Mapema Novemba 2022, katika mkutano wa mawaziri wa mambo ya nje wa Kundi la G7 huko Munster, Josep Borrell, mkuu wa sera za nje na usalama katika Umoja wa Ulaya, alitangaza kwamba umoja huo katika mwaka uliopita wa 2022, uliipa Ukraine dola bilioni 22. Bila shaka, kiasi hiki kinajumuisha usaidizi wa kijeshi na usambazaji wa silaha na hakijumuisha usaidizi wa moja kwa moja kwa Ukraine kutoka kwa nchi wanachama wa Umoja wa Ulaya.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Russia Sergey Lavrov

Wakati huo huo, Ursula van der Leyen, mkuu wa Tume ya Ulaya, alisisitiza katika taarifa yake Januari 13, 2023 kwamba mashinikizo dhidi ya Russia yanapaswa kuongezeka na kuwa Umoja wa Ulaya unapaswa kuendelea kuunga mkono Ukraine.

Marekani na washirika wake wa Ulaya na wasio wa Ulaya, kama vile Kanada, Australia, na hata Japan, wanaona vita vya Ukraine kuwa fursa ya kipekee kwa kile kinachoitwa kulipiza kisasi dhidi ya Russia na rais wake, Vladimir Putin, ambaye kwa zaidi ya miongo miwili amekuwa akikabiliana vilivyo na sera za kujitakia makuu na za kibeberu za Marekani na NATO  huko Ulaya, Asia Magharibi na Amerika Kusini na hata eneo la Aktiki.

Kwa mtazamo wa Rais Joe Biden wa Marekani na maafisa wakuu wa kijeshi na usalama wa utawala wake, vita vya Ukraine ni fursa ya kipekee na isiyoweza kurudiwa ya kupinga chochote kile dhidi ya Russia na kuidhoofisha na hatimaye kuzuia uundaji kamili wa mfumo wa kimataifa wenye kuhusisha pande kadhaa zenye kuchukua maamuzi yaani multilateralism.

Aidha, kwa mtazamo wa viongozi wa nchi za Magharibi, ushindi wa Russia katika vita vya Ukraine, hasa katika maeneo ya jirani ya NATO, utamaanisha kudharauliwa kwa shirika hilo la kijeshi na kupanuka kwa ushawishi na nguvu za kikanda na kimataifa za Russia, na vile vile kutabadilisha mlingano wa kiusalama, kijeshi na kisiasa barani Ulaya kwa madhara ya madola ya Magharibi. Kwa hivyo, Marekani na waitifaki wake wameazimia kufanya juu chini kuhakikisha kuwa Russia haipati ushindi katika vita vya Ukraine. Kwa mtazamo wa Russia, lengo la nchi za Magharibi la kuendeleza vita hivi ni kuidhoofisha kadiri inavyowezekana kwa lengo kuu la kusambaratisha Shirikisho la Russia. Hili ni suala ambalo Wamarekani wamekuwa wakilitazamia tangu enzi za Shirikisho la Sovieti.

Putin amezungumzia njama hiyo na kusema: Marekani imekuwa ikishiriki katika operesheni katika eneo kwa muda mrefu, na wamekuwa wakitayarisha mazingira tangu zama za Usovieti. Marekani imekuwa ikijihusisha na mzozo dhidi ya Russia kwa muda mrefu, sio tu leo ​​na sio baada ya ziara ya Zelensky huko Washington.

Ursula van der Leyen, mkuu wa Tume ya Ulaya

Kwa maelezo hayo, inatarajiwa kwamba vita vya Ukraine, ambavyo sasa viko katika  mwezi wake wa kumi na moja, na ambavyo vimesababisha hasara kubwa za kibinadamu na kijeshi, pamoja na uharibifu wa miundombinu ya Ukraine, sio tu kuwa havitaisha, lakini kwa kuzingatia misimamo ya Rais Volodymyr Zelensky wa Ukraine na uungaji mkono anaopata kutoka kwa Marekani, vita hivyo vitaendelea kushika kasi katika miezi ijayo.

Ishara ya hilo ni kuidhinishwa kwa msaada wa silaha mpya wa dola bilioni 1.8 na jumla ya msaada wa zaidi ya dola bilioni 40 katika mwaka huu wa 2023.

Tayari Biden ameidhinisha Ukraine kukabidhiwa magari ya kivita ya kisasa aina ya "Bradley." Uungaji mkono wa madola ya Magharibi kwa Ukraine ni kinyume kabisa na badai yao ya kupinga vita. Bila shaka, wakati huu uwezekano wa kupanuka wigo wa vita vya Ukraine ndani ya ardhi ya Russia utakuwa mkubwa zaidi kuliko siku za nyuma. Ni wazi kuwa kuendelea vita hivyo kutaongeza uwezekano wa kuenea kwake katika nchi jirani za Ukraine, hasa Poland au jamhuri tatu za Baltic, jambo ambalo litamaanisha kutokea makabiliano ya moja kwa moja ya kijeshi kati ya Russia na NATO.

Tags