Feb 26, 2023 11:23 UTC
  • Maelfu waandamana Italia, Ujerumani kupinga vita na kupewa silaha Ukraine

Maelfu ya wananchi wa Italia wamefanya maandamano katika miji mbalimbali ya nchi hiyo kulalamikia vikwazo vya Magharibi dhidi ya Russia, huku vita vya Ukraine vikiingia mwaka wake wa pili.

Maandamano makubwa zaidi yameshuhudiwa katika mji mkuu Rome na jijini Milan, chini ya kaulimbiu ya 'Ulaya yataka Amani'. Baadhi ya mabango yaliyokuwa yamebebwa na waandamanaji hao yalikuwa na jumbe zinazosema "Hapana kwa Vita" na "Amani". 

Kadhalika waandamanaji hao katika miji ya Pisa, Florence, na Lecce miongoni mwa miji mingine ya Italia wamefanya maandamano hayo ya kupinga kupewa silaha na zana za kijeshi serikali ya Kiev. Baadhi ya mabango yaliyokuwa yamebebwa na waandamananaji yalikuwa yameandikwa "Ondoa Italia kutoka NATO".

Waandamanaji hao nchini Italia wameitaka serikali ya Waziri Mkuu wa nchi hiyo, Giorgia Meloni iache kuipa silaha serikali ya Kiev, sambamba na kufanya jitihada za kusitisha vita hiyo ambavyo vimemaliza mwaka mmoja sasa.

Maurizio Landini, mwanasiasa wa mrengo wa usoshalisti wa Rome ambaye ni mmoja wa waandaaji wa maandamano hayo amesema, "Sisi tunawakilisha asilimia kubwa ya mtazamo wa umma ambao unasisitiza kuwa hautaki vita, bali unataka amani."

Maandamano Italia

Wakati huo huo, maelfu ya wananchi wa Ujerumani wameandamana katika mji mkuu Berlin, wakitoa mwito wa kufanyika mazungumzo ya amani baina ya Russia na Ukraine. 

Waandamanaji hao waliokusanyika jana Jumamosi katika Medani ya Brandenburg mjini Berlin wametoa mwito kusitishwa vita vya Ukraine, sambamba na kuanza mazungumzo ya amani.

Hii ni katika hali ambayo, akthari ya serikali za Magharibi zinapinga mpango wa amani wa China kwa ajili ya kuhitimisha vita vya Ukraine, licha ya vita hivyo na vikwazo dhidi ya Russia kuwa na taathira hasi kwa wananchi wa nchi hizo.

 

Tags