Mar 07, 2023 02:31 UTC
  • Mzozo katika kikao cha G20

Kikao cha kundi la G20 ambacho kiliitishwa kwa kutiliwa mkazo suala la vita vya Ukraine, kimedhihirisha mzozo na hitilafu kubwa zilizopo baina ya nchi wanachama katika masuala tofauti ya kisiasa na kiuchumi kiasi kwamba kikao hicho kilimalizika bila ya kufikiwa makubaliano yoyote.

Sergey Lavrov, Waziri wa Mambo ya Nje wa Russia alitumia kikao hicho kukumbusha kuwa, hadi sasa kundi la G20 halijawahi kujadili vita vyovyote vile duniani bali muda wote limekuwa likijishughulisha tu na masuala makuu ya fedha na uchumi. Alisema, hivi sasa na baada ya Russia kuonya kwa miaka mingi kuwa haiwezi kukaa hivi hivi kuangalia kwa macho tu usalama wake ukihatarishwa, ghafla moja tunaliona kundi la G20 linaonesha kuguswa mno na mgogoro wa Ukraine. Cha ajabu ni kuwa kundi hilo linaguzwa na mgogoro huo tu peke yake na halitaki kabisa hata kugusia migogoro mingine.

Kikao hicho kimefanyika kama tulivyotangulia kusema; kwa kulipa umuhimu mkubwa suala la vita vya Ukraine. Lakini wanachama wa kundi hilo la G20 wana tofauti nyingi baina yao tena zinazokinzana kuhusu vita hivyo vyenyewe. Marekani ilitaka kikao hicho kiilaani Russia kwa vita vya Ukraine lakini Russia na China zilipinga vikali. Janet Yellen, waziri wa hazina wa Marekani alisema kuwa, ni jambo la dharura kikamilifu kwa kikao cha G20 kuilaani Russia kwa vita vya Ukraine, lakini suala hilo halikuweza kuungwa mkono na wanachama wote bali limezua mifarakano na hata kulaumiwa Marekani kwa kutoa pendekezo kama hilo.

Kikao cha G20 kimemalizika bila ya kufikiwa mwafaka wowote

 

Ripoti zinaonesha kuwa, vita vya Ukraine vinazisababishia hasara kubwa za kiuchumi; chi nyingi duniani na hasa wanachama wa G20. Lakini nchi wanachama wa kundi hilo badala ya kujadiliana njia za kukabiliana na hasara kubwa za vita hivyo kwa uchumi wa dunia, ndio kwanza zimekitumia kikao hicho kujaribu kufanikishia malengo yao ya kisiasa.

Kwa kweli vita vya Ukraine viligeuzwa kuwa maudhui kuu ya kikao cha G20 katika hali ambayo huko nyuma kundi hilo lilikuwa limenyamazia kimya kikamilifu jinai za Marekani katika nchi za Iraq, Libya na Afghanistan. Waziri wa Mambo ya Nje wa Russia amesema, inashangaza kuona kundi la G20 linaguswa tu na vita ya Ukraine na kukwepa kikamilifu kuzungumzia hatua za huko nyuma za Marekani katika nchi za Iraq, Libya, Afghanistan na Yugoslavia. Alisema, napenda kuwauliza waliokuwa viongozi wa kundi hilo, kwa nini miaka yote hiyo, kundi la G20 limeshindwa kutoa tamko lolote kukhusu hali mbaya ya nchi za Iraq, Libya, Afghanistan na hata Yugoslavia?

Undumilakuwili wa madola ya Magharibi katika matukio ya dunia

 

Ijapokuwa awali ilidaiwa kuwa, lengo la kikao cha hivi karibuni cha G20 lilikuwa ni kutatua mgogoro wa kiuchumi duniani na kuzipunguzia mzigo nchi zenye kipato cha chini, lakini Marekani na waitifaki wake walijaribu kuteka malengo ya kikao hicho na kukigeuza kuwa wenzo wa kutoa mashinikizo kwa Russia. Kwa kweli Marekani bado ina ndoto zile zile za kuifanya dunia kuongozwa na kambi moja chini ya udhibiti wake kwa kutumia visingizio vile vile vya vita dhidi ya ugaidi, kuzusha vita vya kieneo na kuzikalia kwa mabavu nchi kama Afghanistan na Iraq pamoja na kuingilia masuala ya ndani ya nchi kama Syria. Marekani imefikia hadi ya kuyakalia kwa mabavu baadhi ya maeneo ya Syria kwa ndoto zake hizo. Hivi sasa Marekani bado inang’ang’ania siasa hizo lakini wakati huo huo inajifanya kuguswa mno na vita vya Ukraine ambavyo ni Marekani na madola ya Magharibi ndio wachochezi wakubwa na waendelezaji wa vita hivyo.

Vasily Alekseyevich Nebenzya, Mwakilishi wa Kudumu wa Russia katika Umoja wa Mataifa amelaani vikali ukosefu wa uadilifu katika matukio ya dunia na kusema kuwa, jinai za nchi za Magharibi huko Iraq zimedharauliwa kikamilifu na hakuna hatua zozote zinazochukuliwa dhidi ya madola hayo vamizi.

Kwa kweli misimamo ya kindumilakuwili ya nchi za Magharibi katika masuala tofauti mara hii pia imevuruga kikao cha G20. Badala ya kikao hicho kuzungumzia masuala yanayoitesa dunia hivi sasa kwa siasa mbovu na za dhulma za madola hayo hayo ya kiistikbari, sasa hivi pia fursa hiyo muhimu imepotezwa vivi hivi kwa kuzushwa ndani yake mambo ambayo hayasaidii chochote katika utatuzi wa migogoro inayousumbua ulimwegu hivi sasa.

Tags