Mar 12, 2023 09:49 UTC
  • Papa akosoa idiolojia ya watu kubadilisha jinsia zao

Kiongozi wa Kanisa Katoliki Duniani, Papa Francis amekosoa vikali kampeni ya kuhamasisha watu kubadilisha jinsia zao, na kuitaja nadharia hiyo kama moja ya ukoloni hatari zaidi wa kiidiolojia uliopo duniani hivi sasa.

Papa amesema hayo katika mahojiano na gazeti la Argentina la 'La Nación' na kueleza kuwa, kitendo hicho cha watu kubadilisha jinsia zao ni hatari kwa kuwa kinatia kiwingu katika tofauti za kimaumbile za wanaume na wanawake, mbali na kuhujumu thamani za kijinsia za matabaka hayo mawili.

Amesema wimbi hilo la kuwashajiisha wanadamu kubadilisha jinsia zao ni hatari kwa binadamu, utamaduni na tofauti za kijamii zilizopo miongoni mwa watu wa jamii tofauti. 

Papa amesema wanaounga mkono na kushajiisha watu kubadilisha jinsia zao hawana hekima wala uzoefu katika maamuzi yao, hasa kama wanaamini kuwa wapo katika njia ya ustawi na maendeleo.

Kuna wimbi kubwa la kampeni zinazoendeshwa na Wamagharibi hivi sasa kote duniani, za kuwashawishi watu kukumbatia ushoga, usagaji, kubadilisha jinsia na mahusiano ya kingono ya watu wa jinsia moja, chini ya mwavuli wa LGBTQ.

Papa karibuni alibariki mahusiano ya watu wa jinsia moja

Hii ni katika hali ambayo, hivi karibuni, Kiongozi huyo wa Kanisa Katoliki Duniani alitetea vitendo hivyo vichafu vya mapenzi ya watu wenye jinsia moja ambavyo vimekuwa vikilalamikiwa katika mataifa mbalimbali. Papa Francis na viongozi wa makanisa ya kiprotestanti nchini Uingereza na Scotland karibuni walishutumu kujinaishwa kwa uhusiano wa mapenzi ya watu wa jinsia moja katika nchi mbalimbali duniani.

Kiongozi huyo wa Vatican amekosolewa vikali na maaskofu na makasisi wahafidhina wa kanisa hilo haswa kutoka barani Afrika, kutokana na kauli yake hiyo inayoashiria kuwa anaunga mkono mahusiano na ndoa za watu wenye jinsia moja.

Tags