Apr 09, 2023 02:14 UTC
  • Kuchapishwa ripoti rasmi ya serikali ya Biden kuhusu kuondoka Afghanistan

Ikulu ya Rais wa Marekani (White House) Alhamisi iliyopita iliwasilisha ripoti yake rasmi kuhusu namna serikali ya Biden ilivyoondoka kwa madhila na fedheha huko Afghanistan. Ndani ya ripoti hiyo, serikali ya Trump imetajwa mara kwa mara kuwa ndio inayopaswa kulaumiwa kwa jinsi Marekani ilivyondoka huko Afghanistan katika hali ya mivutano.

Ripoti hiyo aidha imeituhumu serikali ya wakati huo ya Trump kuwa ilitatiza kuondoka Marekani huko Afghanistan  na kubainisha kuwa: Hakukuwa na ushahidi wowote kwamba kuongezwa muda, bajeti au wanajeshi zaidi wa Marekani huko Afganistan kungesaidia kubadili mkondo wa matukio nchini humo. Ripoti hiyo aidha imeashiria kupunguzwa kwa makusudi idadi ya wanajeshi kulikofanywa na serikali ya Trump. 

John Kirby, Mratibu wa Mawasiliano ya Kistratejia katika Baraza la Usalama wa Taifa ndani ya White House anasema kuhusiana na suala hili kwamba: Ripoti hii pia imeashiria kupunguzwa vikosi vya jeshi la Marekani huko Afghanistan wakati wa utawala wa Rais Trump, kuachiwa huru maelfu ya wanamgambo wa Taliban, kufanyika mazungumzo huko Doha ili kuhitimisha vita bila ya kuasisiwa serikali ya ndani na kusitishwa programu ya utoaji viza huko Afghanistan.  

John Kirby 

Ripoti hiyo yenye kurasa 12 inadai kuwa, serikali ya Marekani imepata funzo kutokana na kuondoka kwake huko Afghanistan.

Kama ilivyokuwa ikitazamiwa, ili kujitoa hatiani, serikali ya Biden sasa imeitupia lawama serikali ya Donald Trump na kuituhumu kuwa chanzo cha hatua zote hizo zilizopelekea wanajeshi wa Marekani waondoke kwa madhila na fedheha huko Afghanistan. 

Hii ni katika hali ambayo, kwa kuzingatia mbioni za uchaguzi ujao wa rais mwaka 2024, wapinzani wa chama cha Republican wanaompinga Rais Joe Biden wa chama cha Democrat, wanafanya kila wawezalo kukuza udhaifu na utendaji mbaya wake, ikiwa ni pamoja na uongozi wake mbaya kuhusu kuondoka vikosi vamizi vya nchi hiyo huko Afghanistan; nukta ambayo wapinzani wa chama cha Republican wanataka kuitumia kufanikisha kampeni zao katika uchaguzi ujao. Ikumbukwe kuwa wabunge wa chama cha Republican kwa muda sasa wamekuwa wakitaka kufanyike uchunguzi kuhusu Afghanistan. Kimsingi hili ni moja ya masuala ambayo chama cha Republican kiliazimia kuyafanyia utafiti baada ya kujinyakulia viti vingi katika Bunge la Wawakilishi katika uchaguzi wa katikati ya msimu wa Novemba 8 mwaka jana.   

Vikosi vamizi vya Marekani Afghanistan 

Kwa hakika hatua ya Marekani ya kuondoa haraka vikosi vamizi vya nchi hiyo huko Afghanistan kwa amri ya Rais wa nchi hiyo, Joe Biden, ambayo hatimaye ilipelekea kusambaratika serikali ya Afghanistan na kuingia madarakani kundi la Taliban; imemfanya Biden akabiliwe na ukosoaji mkubwa ndani na nje ya nchi hiyo. Ndani ya Marekani, Rais wa wakati huo, Donald Trump, ametaka Joe Biden kujiuzulu kufuatia mgogoro wa Afghanistan.  

Trump ambaye alianzisha mkakati wa kuviondoa vikosi vamizi vya Marekani huko Afghanisatn wakati wa utawala wake ameeleza kuwa: Kile alichofanya Biden huko Afghanistan ni maajabu matupuu; na hii itakuwa moja ya kushindwa kukubwa Marekani katika historia ya nchi hii. 

Nje ya Marekani pia waitifaki wa Ulaya wa Washington wamekosoa uamuzi huo wa Biden. Matteo Renzi Waziri Mkuu wa zamani wa Italia amesema: Rais wa Marekani amefanya kosa la kihistoria huko Afghanistan na ameendeleza njia ya Donald Trump.  

Matteo Renzi, Waziri Mkuu wa zamani wa Italia 

Licha ya kukosolewa pakubwa, lakini Joe Biden ameendelea kusisitiza kwamba uamuzi wake wa kuviondoa vikosi vya majeshi ya Marekani huko Afghanistan ulikuwa sahihi ili kuhitimisha vita vya muda mrefu vilivyoendelewa kwa miongo miwili.

Msimamo wa Biden wa kung'ang'ania haja ya kuhitimisha haraka uwepo wa wanajeshi vamizi wa Marekani huko Afghanistan ulimpelekea kutangaza muhula wa mwisho wa hadi kufikia Agosti 31 mwaka 2021 kuwa muda wa mwisho wa kuondoka vikosi vamizi vya Marekani nchini humo.

Marekani iliivamia na kuikalia kwa mabavu Afghanistan wakati wa utawala wa Rais George W. Bush baada ya mashambulizi ya Septemba 11 maka 20001 kwa kisingizio eti cha kupambana na ugaidi duniani na kuuondoa madarakani utawala wa Taliban ambao iliutuhumu kuwa na ushirikiano na mtandao wa kigaidi wa al Qaida. Idadi ya askari vamizi wa Marekani na muungano wa Nato nchini Afghanistan ilikuwa zaidi ya  140,000 baada ya kupita miaka kadhaa ya kukaliwa kwa mabavu nchi hiyo mnamo mwaka 2011. Pamoja na hayo, kusalia kwa miaka 20 vikosi vamizi vya Marekani na Nato katika nchi hiyo iliyoathiriwa na vita hakujawa na manufaa yoyote kwa Waafghani ghairi ya kuwazidishia ukosefu wa amani, hali ya mchafukoge, umaskini, uzalishaji na magendo ya madawa ya kulevya na kuongezeka vitendo vya ugaidi. Hatimaye vikosi vamizi vya majeshi ya Marekani viliandaa mazingira ya kusambaratika serikali ya Afghanistan na kudhibitiwa mji mkuu Kabul na kundi la Taliban.

Tags