Jun 01, 2023 06:31 UTC
  • Guterres: Waafrika wanaendelea kusumbuliwa na ubaguzi wa rangi

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa ametoa wito wa kukomeshwa ubaguzi wa rangi duniani.

 Antonio Guterres, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, ametoa wito huo katika ujumbe wake wa video na kuitaka jamii ya kimataifa kuchukua hatua za kutokomeza janga la ubaguzi wa rangi.

Akihutubia mkutano wa pili wa Jukwaa la Kudumu la Waafrika, Guterres amesema: Waafrika walio mbali na nchi zao wametajirisha jamii nyingine duniani kote na kusaidia katika nyanja zote za shughuli za kibinadamu.

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa amesisitiza kuwa: "Hata hivyo, tunafahamu kwa uchungu kwamba Waafrika wanaendelea kusumbuliwa na ubaguzi wa rangi uliokithiri na ubaguzi wa kimfumo."

Antonio Guterres amesema kuwa karne nyingi za utumwa na unyonyaji wa binadamu wakati wa enzi ya ukoloni zimeacha kivuli katika hali ya dunia ya sasa, na ameeleza matumaini kuwa umefika wakati wa kulielewa suala hili na kurekebisha makosa. 

Jukwaa la Kudumu la Watu Wenye Asili ya Afrika lilianzishwa mwaka wa 2021 na Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa kama utaratibu wa mashauriano kwa ajili ya watu wenye asili ya Afrika.

Kikao cha pili cha kongamano la jukwaa hilo kinakachofanyika katika makao makuu ya Umoja wa Mataifa mjini New York, kilianza Jumanne, Mei 30, na kitaendelea hadi Ijumaa, Juni 2.