Watoto milioni 449 wanaishi katika maeneo ya migogoro
Shirika la Save the Children limesema mamia ya mamilioni ya watoto wanaishi katika maeneo yenye migogoro ya kivita na wanakabiliwa na hatari ya kifo.
Shirika hilo limesema hayo katika ripoti yake mpya iliyotolewa kwa mnasaba wa Siku ya Kimataifa ya Watoto Wasio na Hatia Waathirika wa Unyanyasaji inayoadhimishwa hii leo Juni 4.
Siku hiyo ilitangazwa na Umoja wa Mataifa mwaka 1982 kwa ajili ya kushughulikia mashaka ya watoto wanaosumbuliwa na unyanyasaji wa kimwili, kiakili na kiroho kufuatia hali mbaya ya watoto wa Palestina na Lebanon wanaosumbuliwa na ukatili wa utawala haramu wa Israel.
Ripoti ya Save the Children imeeleza kuwa, kufikia mwaka 2021, watoto wasiopungua milioni 449 walikuwa wanaishi katika maeneo ambayo yana makundi ya wabeba silaha na vikosi vya serikali ambavyo vinasajili watoto kuingia vitani. Imesema katika kipindi hicho, kesi 24,000 za unyanyasaji wa kuchupa mipaka dhidi ya watoto zilinakiliwa.
Shirika hilo la kutetea maslahi ya watoto duniani limebainisha katika ripoti yake hiyo kuwa, idadi ya watoto waliouawa katika maeneo ya vita duniani kipindi hicho ni takriban 2,515, mbali na wengine 5,555 kusababishiwa ulemavu.
Kwa mujibu wa ripoti hiyo ya shirika la Save the Children, nchi zinazoongoza kwa unyanyasaji na jinai dhidi ya watoto duniani ni Afghanistan, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Somalia, Syria, utawala haramu wa Israel na Yemen.