Utafiti: Wanaume wa Ujerumani wanaunga mkono unyanyasaji dhidi ya wanawake
https://parstoday.ir/sw/news/world-i98680-utafiti_wanaume_wa_ujerumani_wanaunga_mkono_unyanyasaji_dhidi_ya_wanawake
Matokeo ya utafiti uliofanyika nchini Ujerumani yanaonyesha kuwa zaidi ya theluthi moja ya wanaume nchini humo wanaona kuwa unyanyasaji dhidi ya wanawake "unakubalika".
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Jun 12, 2023 04:30 UTC
  • Utafiti: Wanaume wa Ujerumani wanaunga mkono unyanyasaji dhidi ya wanawake

Matokeo ya utafiti uliofanyika nchini Ujerumani yanaonyesha kuwa zaidi ya theluthi moja ya wanaume nchini humo wanaona kuwa unyanyasaji dhidi ya wanawake "unakubalika".

Utafiti huo wa shirika la misaada kwa watoto la  Plan International Germany, ambao matokeo yake yalichapishwa siku ya Jumapili, umetathminiwa na watetezi wa haki za binadamu kuwa "wa kushtua na wa kusikitisha".

Kulingana na matokeo ya uchunguzi huo, asilimia 33 ya wanaume Wajerumani wenye umri wa miaka 18 hadi 35 wamesema wanakubali fikra kwamba "wakati fulani wanawapiga wake zao wakati wa mabishano."

Wakati huo huo, 34% ya wanaume wa Ujerumani wamekiri kwamba waliwahi kufanya ukatili dhidi ya wanawake. 

Kristin Kisner, mwanachama wa Chama cha Shirikisho la Wanaume, ambacho kinapigania usawa wa kijinsia nchini Ujerumani, amesema: "Matokeo haya ni ya kusikitisha na ya kushangaza."

Kisner ameongeza kuwa: "Inashangaza sana na kuumiza kuona kwamba theluthi moja ya wanaume wa Ujerumani wanapuuza unyanyasaji wa kimwili dhidi ya wanawake."

Utafiti huo wa shirika la misaada kwa watoto la Plan International ulifanyika mtandaoni kuanzia Machi 9 hadi 21.

Data za Polisi wa Shirikisho la Ujerumani zinaonyesha kuwa, zaidi ya wanawake 115,000 walikuwa waathiriwa wa unyanyasaji wa majumbani mnamo 2021.

Mnamo 2021, jumla ya wanawake 301 waliuawa na wenzi wao wa sasa au wa zamani.