Jun 15, 2023 02:23 UTC
  • Ununuzi wa mafuta kutoka Iran, nembo ya kufeli sera za vikwazo za Magharibi

Takwimu mpya zilizotolewa na Kituo cha Takwimu cha Ulaya (Eurostat) zinaonyesha kuwa, kwa mara ya kwanza tangu mwaka 2018, Ujerumani imeagiza shehena kubwa ya mafuta au bidhaa za petroli kutoka Iran licha ya vikwazo vya Marekani.

Takwimu hizo zinaonyesha kuwa, mwezi Machi mwaka huu, Ujerumani iliagiza tani 69,737 za mafuta ghafi au bidhaa za petroli kutoka Iran. Bulgaria, ikiwa mwanachama mwingine wa Umoja wa Ulaya, pia imeagiza tani 147 za mafuta ghafi au bidhaa za mafuta kutoka Iran katika robo ya kwanza ya mwaka huu. Jumla ya uagizaji wa mafuta wa Umoja wa Ulaya kutoka Iran katika kipindi hicho ulifikia tani 69 na 884, na kiwango hicho hakijawahi kushuhudiwa tangu Marekani ilipojiondoa katika makubaliano ya nyuklia ya JCPOA mwaka 2018. Kwa kuzingatia hayo, wanachama wawili wa Umoja wa Ulaya wameagiza mafuta ghafi au bidhaa za petroli kutoka Iran katika robo ya kwanza ya mwaka huu, kinyume na sera ya Marekani ya vikwazo vya mafuta dhidi ya Iran.

Mara ya mwisho Ujerumani iliagiza shehena ya tani 10,000 za mafuta ghafi au bidhaa za petroli kutoka Iran Oktoba 2018. Kiasi hicho cha mafuta ya Iran kiliagizwa na nchi ya Ulaya wakati serikali ya Marekani ilipokuwa bado haijafanya mabadiliko yoyote kwenye vikwazo vilivyo kinyume cha sheria dhidi ya Jamhuri ya Kislamu. Mwaka jana wa 2022, nchi tatu za Bulgaria, Romania na Poland ziliagiza jumla ya tani 4181 za mafuta ghafi au bidhaa za petroli kutoka Iran.

Kuanza tena uagizaji wa mafuta wa nchi za Ulaya kutoka Iran, ikiwemo Ujerumani, ambayo ndiyo nchi yenye uchumi mkubwa zaidi barani Ulaya, kunaonyesha kuwa sera ya vikwazo vya upande mmoja vya Marekani dhidi ya Iran, ambayo ilianza kutekelezwa mwezi Mei 2018 wakati wa utawala wa Trump ina kuungwa mkono na washirika Washington barani Ulaya, imefeli na kushindwa; na Wazungu wamelazimika kuliangalia upya suala hili kutokana na mahitaji yao ya mafuta, hasa baada ya kuwekewa vikwazo vya mafuta na Russia. Kwa hivyo, wakati ikiwa imepita miaka 5 tangu kuanza kutekelezwa vikwazo dhidi ya Iran na kwa kutilia maanani mabadiliko ya hali ya kiuchumi na kijiografia ya dunia ya sasa, haswa baada ya mashambulio ya Russia dhidi ya Ukrain, inaonekana kuwa mikakati ya viwanda vya kusafisha mafuta vya Ulaya ya kupuuza vikwazo vya Marekani dhidi ya Iran imeongezeka zaidi. Vilevile, kuingizwa kwa takwimu zinazohusiana na uagizaji wa mafuta ya Iran katika hifadhidata rasmi ya Ulaya kunaonyesha hamu ya duru rasmi za nchi za bara hilo ya kutaka kujiweka mbali na vikwazo au kwa uchache kuonyesha pingamizi lao kwa sera ya vikwazo vya Marekani dhidi ya Iran.

Kwa upande mwingine, kauli za hivi karibuni za Waziri wa Uchumi wa Ujerumani, Robert Habeck, zinaonyesha kuwa licha ya kaulimbiu za awali za maafisa wa serikali ya Ujerumani kuhusu kususia kikamilifu gesi ya Russia na kuchukua hatua za kukata utegemezi wa Berlin kwa Moscow katika sekta ya gesi, lakini bado kuna vizuizi na matatizo mengi ya kimuundo katika uwanja huu. Wakati Berlin inadai kuwa ilisimamisha kabisa kuagiza gesi kutoka Russia tangu Januari 2023, nchi zingine za EU zinaendelea kutegemea Moscow kwa ajili ya kukidhi mahitaji yao ya nishati. 

Robert Habeck

Robert Habeck amekiri kwamba iwapo uagizaji wa gesi asilia kutoka Russia kupitia Ukraine utasitishwa mwaka ujao, Ujerumani italazimika kupunguza au hata kuzima uwezo wake wa kiviwanda, na hakuna hali ya uhakika ya jinsi mambo yatakavyokuwa katika siku zijazo. Amefafanua kuwa watunga sera mjini Berlin wanapaswa kuepuka kurudia kosa walilofanya hapo awali kwa kudhani kuwa uhaba wa nishati hautaathiri uchumi.

Wakati huo huo, ikiwa utekelezaji kamili wa vikwazo vya Umoja wa Ulaya dhidi ya gesi ya Russia utapelekea nchi kama Austria, Slovakia, Italia na Hungary zishindwe kupata gesi kutoka Russia, sheria za kugawana gesi za Umoja wa Ulaya zitailazimisha Ujerumani kufidia uhaba huo, na suala hili litasababisha matatizo maradufu kwa wateja wa gesi ya viwandani nchini Ujerumani.

Licha ya vita kati ya Russia na Ukraine, Moscow bado inatekeleza mkataba wa kupeleka gesi huko Ulaya na kulipa gharama za usafiri kwa Ukraine. Hata hivyo, inaonekana kuwa kwa kutilia maanani mazingira ya sasa, ni jambo lililombali kurefushwa mkataba wa kununua gesi kutoka Russia baada ya kumalizika mwaka ujao wa 2024.  

Kwa ujumla tunaweza kusema kuwa, inaonekana kwamba, hatua na kauli za Berlin kuhusu uagizaji wa mafuta kutoka Iran hadi kukiri kwamba kusimamishwa gesi ya kutoka Russia kuna taathira mbaya kwa Ujerumani, zinaonyesha kuwa, licha ya madai ya hapo awali, lakini ukweli ni kwamba uchumi wa Ulaya unatikiswa sana kutokana na uhaba wa nishati hiyo, na nchi za bara hilo haziweza kuendelea na sera iziyo sahihi ya vikwazo.

Tags