Bahman 22 dhihirisho la nguvu za taifa la Iran
Tarehe 11 Februari ni siku ya kuadhimisha ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu maarufu kwa sherehe za Bahman 22 nchini Iran. Leo (Alkhamisi) Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran yameadhimisha miaka 37 ya tangu kupata kwake ushindi tarehe 11 Februari 1979.
Ushindi huo ulikuwa ni nukta muhimu sana na ya kudumu milele. Ushindi
huo adhimu si tu kwamba uliandaa uwanja wa kutokea mabadiliko makubwa na
ya kimsingi nchini Iran, bali mapinduzi hayo yamekuwa na taathira kubwa
kieneo na kimataifa. Hivyo maadhimisho ya Bahman 22 ni kukumbuka tukio
kubwa katika historia na yanaonesha namna Mapinduzi ya Kiislamu na mfumo
wa Jamhuri ya Kiislamu ulivyoimarika, ulivyo msafi na ulivyo na
harakati nyingi za maana.
******
Wanafikra na wachambuzi wengi wa
masuala yanayohusiana na mapinduzi tofauti duniani wote wanakubaliana
kuwa, Mapinduzi ya Kiislamu ya nchini Iran, licha ya kupita zaidi ya
miongo mitatu tangu yalipopata ushindi, hadi hivi sasa hayajajitenga na
malengo yake ya tangu awali kabisa na hadi leo hii wananchi wa Iran
wanashirikiana kwa wingi mno kulinda na kufanikisha malengo ya mapinduzi
yao ya Kiislamu. Kwa maneno mengine ni kuwa, licha ya kwamba mapinduzi
yote mengine duniani huwa yanaachana na malengo yao ya awali kadiri siku
zinavyopita na hatimaye kudhoofika na kusambaratika kabisa mapinduzi
hayo, lakini Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran yameweza kudumu katika
malengo yake yale yale ya awali licha ya kuweko mashinikizo mengi na
njama za kila aina, kuanzia vita vya kujihami kutakatifu vilivyoanzishwa
na utawala wa zamani wa Iraq dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran hadi
kuwekewa vikwazo vya kila aina vikiwemo vya kiuchumi, lakini mapinduzi
haya hayajatetereka, bali yameendelea kuwa imara na kuzidi kuyaathiri
mataifa mengine duniani.
Hatua zilizochukuliwa na maadui wa Mapinduzi
ya Kiislamu kama vile kuiwekea Iran vikwazo vya kiuchumi, na kujaribu
kulikwamisha taifa hili katika jitihada zake za kujiletea maendeleo
kwenye nyuga tofauti, zote zimeshindwa. Pamoja na kuwa, Iran inakiri
kwamba vikwazo vimelisababishia matatizo taifa hili, lakini pia ugumu
huo umezidi kuyaimarisha Mapinduzi ya Kiislamu na kuyapa nguvu za kuzidi
kujitegemea.
Hii ina maana ya kwamba, kusimama kidete taifa la Iran
katika kukabiliana na madola ya kiistikbari na kibeberu, si nara na
maneno matupu, bali Mapinduzi ya Kiislamu ambayo ni mapinduzi yenye
uungaji mkono mkubwa zaidi wa wananchi duniani, yamewaandalia wananchi
wa Iran mazingira mazuri sana kiasi kwamba wananchi hao wameweza kupiga
hatua nzuri mno kuelekea kwenye ufanikishaji wa malengo yao, bila ya
kutoka angalau kidogo nje ya malengo makuu matukufu ya Mapinduzi ya
Kiislamu.
*******
Malengo na shabaha za kimapinduzi za taifa la
Iran kwa hakika zinadhihirika wazi katika mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu.
Pamoja na kwamba watu ambao wanazijua fikra za mapinduzi haya wanatambua
kuwa, kushiriki kwa wingi mno wananchi wa Iran katika maadhimisho ya
Bahman 22 ni kutangaza upya utiifu wao kwa malengo ya Mapinduzi ya
Kiislamu lakini kujitokeza kwa wingi kiasi chote hicho wananchi katika
maadhimisho ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu kuna na ujumbe mwingine,
nao ni wa kuwatangazia walimwengu kuwa katika taifa la Iran kuna umoja
na mshikamano mkubwa kati ya wananchi wote.
Kwa kushiriki kwa wingi
mno na kwa kauli moja na kwa hamasa na shauku kubwa wananchi wa Iran
kwenye maadhimisho ya Bahman 22 kunazidi kuyapa kinga matunda ya mfumo
wa Jamhuri ya Kiislamu na kuwathibitishia walimwengu kuwa, wananchi wa
Iran kamwe hawako tayari kuona mafanikio yao yanachezewa na kwamba
mrengo wowote unaokwenda kinyume na malengo matukufu ya Mapinduzi ya
Kiislamu, iwe ni wa ndani au nje ya mipaka ya Iran, hauwezi kutia doa
kwenye msimamo huo.
Hivyo ujumbe muhimu unaopatikana katika
maadhimisho ya Bahman 22 ya kuadhimisha ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu
ni kusimama kidete taifa la Iran mbele ya maadui na njama zao ambao
wanatafuta kila njia kufanikisha njama zao hizo nchini Iran imma kupitia
vita vya moja kwa moja vya kijeshi, au kwa kutumia vita laini. Muono
huo wa mbali wa taifa la Iran umefelisha njama zote za maadui. Kwa
maneno ya wazi zaidi inabidi tuseme kuwa, kujitokeza kwa wingi mno
wananchi wa Iran na kwa hamasa kubwa katika maadhimisho ya Bahman 22
kuna maana ya kupinga ubeberu na uistikbari wa aina yoyote ile na ni
kusisitiza kwa mara nyingine tena kuwa wako imara katika kulinda haki
zao mbele ya madola ya kiistikbari. Huo ndio uhakika ambao unawafanya
mabeberu wa dunia watamani kupasuka kwa hamaki.
*******
Tunapozitupia
jicho kazi zilizofanywa na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika kipindi
cha miaka 37 iliyopita tutagundua kuwa, mfumo huo wa Kiislamu umeweza -
kwa ushujaa mkubwa - kuzishinda njama na mitihani yote mizito ya vita
vya kijeshi na vita laini na katika siku za usoni pia, taifa hili
halitaruhusu madola yanayopenda kujikumbizia kila kitu upande wake,
kulishinikiza kisiasa, kiuchumi kwa vitisho vya kijeshi na litahakikisha
kuwa Iran ya Kiislamu inazidi kupiga hatua katika njia yake ya
kujiletea maendeleo.
Mafanikio ya Iran katika uga wa kidiplomasia na
kuweza taifa hili kubadilisha vitisho vya maadui katika kadhia ya
nyuklia kuwa maelewano na kutambuliwa haki ya Iran katika uga wa nyuklia
pamoja na mafanikio mengine mengi, yanaonesha namna Iran ilivyo na
nguvu katika upande usiokuwa wa kutumia nguvu za kijeshi.
Maadhimisho
ya mwaka huu ya Bahman 22 ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran
yameambatana na ushindi mwingine mwingi katika nyuga za kisiasa na
katika mazungumzo ya nyuklia yaliyopelekea kuanza kutekelezwa mpango
maalumu wa JCPOA. Bila ya shaka yoyote, mafanikio hayo yatazidi kuutia
nguvu muqawama wa taifa la Iran na kuzidi kuwakatisha tamaa maadui wa
taifa hili. Mafanikio hayo yamezidi kuwafanya wananchi wa Iran wapate
nguvu za kupigania haki zao na kujiletea maendeleo, kama ambavyo
yanazidi kuyavutia mataifa mengine yanayopigania ukombozi duniani ili
nayo yasitetereke katika kukabiliana na madola ya kibeberu ulimwenguni.
Leo
hii Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imepata mafanikio makubwa katika nyuga
zote. Katika upande wa elimu na teknolojia, Iran leo hii iko juu ya
wastani wa ustawi na kuzalisha elimu na katika baadhi ya masuala ya
kisayansi kama vile kuzalisha seli shina katika elimu ya shabihishi
(cloning), katika teknolojia ya nyuklia na uzalishaji wa dawa za kila
namna za kutumia mionzi kwa kutumia teknolojia ya nyuklia kutibu
magonjwa sugu na vile vile katika uzalishaji wa fueli nyuklia
inayohitajiwa na vinu vya atomiki na kuzalisha mazao kwa kutumia
teknolojia ya Nano, pamoja na mafanikio mengine mengi, ni mambo ambayo
yameiweka Iran katika orodha ya nchi zilizopiga hatua kubwa katika elimu
na teknolojia za kisasa. Hii ni katika hali ambayo, katika miaka yote
hii, Iran iko chini ya vikwazo ambavyo maadui walioviweka wanajigamba
kuwa ni vikwazo vya kuifanya kilema Iran. Vikwazo hivyo vilikuwa vingi
kiasi kwamba madola ya kibeberu yalifikia hatua ya hata kuizuia Iran
isisambaze makala zake za kielimu kwenye majarida ya kielimu ya nchi za
Magharibi. Hata hivyo, leo hii tena, kipindi hicho kimeshapita. Katika
upande wa miamala ya kiuchumi ya baada ya kutekeleza mpango wa JCPOA wa
makubaliano ya nyuklia kati ya Iran na kundi la 5+1 pia, leo hii Iran
imekuwa chaguo la juu la nchi za Ulaya na Asia na kwamba mafanikio yote
haya yamepatikana licha ya kuweko ukwamishaji wa kila aina wa mabeberu
wanaoongozwa na Marekani.
******
Kiujumla ni kuwa, mafanikio
iliyopata Jamhuri ya Kiislamu ya Iran bila ya kutumia nguvu za kijeshi
ni makubwa sana katika nyuga tofauti na hilo linaonekana kwa uwazi
kabisa katika nyuga zote. Amma muda wa makala hii maalumu umeisha kwa
leo. Ni matumaini yangu mumeweza kufaidika vya kutosha. Ishini salama.