Mapinduzi ya Kiislamu na kurejeshwa utambulisho wa Kiislamu wa wanawake wa Kiirani
(last modified Wed, 31 Jan 2024 13:33:57 GMT )
Jan 31, 2024 13:33 UTC
  • Mapinduzi ya Kiislamu na kurejeshwa utambulisho wa Kiislamu wa wanawake wa Kiirani

Hakuna shaka kuwa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran ni moja ya mapinduzi yaliyoongozwa na kusimamiwa kwa wingi na wananchi wenyewe duniani.

Ilikuwa muhali kuweza kuung'oa madarakani utawala wa kifalme wa Kipahlavi nchini Iran, ambao ulikuwa ukiungwa mkono na kupewa himaya na madola makubwa ya kigeni na vikosi  vya polisi na jeshi lenye nguvu, bila ya kushiriki kwa wingi na kwa umoja wananchi wa Iran katika harakati hiyo kubwa ya mapambano ya ukombozi. Pamoja na hayo, kile kilichofanikisha zaidi ushiriki wa wananchi katika harakati za Mapinduzi ya Kiislamu hapa nchini ni mahudhurio makubwa, ushiriki athirifu na wa kishujaa wa wanawake katika maandamano yaliyokuwa yakifanyika kote nchini dhidi ya utawala dhalimu wa Shah. 

Kabla ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu nchini Iran, wanawake sawa kabisa na wanaume, walikuwa wakitaabika na kuteseka kwa dhulma, ubaguzi na hali mbaya kiuchumi. Lakini kilichowakasirisha zaidi ni kukithiri kwa rushwa ya ngono na kutumiwa wanawake kama wenzo wa kushibisha matamaniio ya wanaume. Hata hivyo kutokana na kujiri Mapinduzi ya Kiislamu, Imam Ruhullah Khomeini (M.A) kiongozi wa harakati ya Mapinduzi alitoa kipaumbele maalumu kwa nafasi na uwezo wa  wanawake, na wao pia wakatoa mchango mkubwa katika harakati hiyo adhimu ya wananchi kwa hamasa ya aina yake kutokana na imani waliyokuwa nayo kwa kiongozi huyo. Imam alikuwa akiwaenzi wanawake na kusifu mahudhurio yao makubwa katika harakati za Mapinduzi. Alikuwa akisema: Ushindi huu umepatikana kutoka kwa wanawake wetu kabla ya wanaume. Kwa hakika wanawake wetu waheshimiwa walikuwa katika safu za mbele za mapambano. Wao ndio waliowatia ushujaa na ujasiri wanaume, na sisi tunathamini sana mchango wao." Heshima na imani hii kubwa kwa wanawake wa Kiirani viliimarisha mshikamano wao na Imam na Mapinduzi ya Kiislamu, na katika matukio tofauti ya baada ya Mapinduzi ya Kiislamu, wanawake nchini Iran walikuwa na nafasi na mchango muhimu katika kulinda na kutetea matunda na mafanikio ya Mapinduzi.     ****

Imam Ruhullah Khomeini (M.A)

Kiwango cha juu cha uaminifu wa wanawake wa Iran kwa utawala wa Kiislamu na nchi yao kilidhihirika zaidi wakati wa vita vya kulazimishwa vilivyoanzishwa na dikteta wa zamani wa Iraq, Saddam Hussein dhidi ya Iran. Katika muda wa miaka 8 ya kujihami kutakatifu, wanawake walikuwa wakitayarisha na kutuma chakula na vifaa vilivyohitajika kwa ajili ya wanamapambano wa Kiislamu katika safu za mbele za vita na kutoa msaada mkubwa katika mapambano ya kuilinda nchi. Wanawake karibu 6,500 waliuawa shahidi na maelfu ya wengine walijeruhiwa katika vita hivyo vya nadra kuwahi kushuhudiwa. Mkabala wake, Mapinduzi ya Kiislamu pia yamewatunuku wanawake mafanikio na fursa nyingi, muhimu zaidi ikiwa ni kuhuishwa heshima na utambulisho wao wa Kiirani na Kiislamu. Wanawake wa Iran hivi sasa, pamoja na kuwajibika katika  nafasi yao ya kuwa mama na mke nyumbani, pia wanafanya kazi katika nyanja mbalimbali za kijamii kama binadamu anayewajibika na mchapakazi, sambamba na kulinda utakasifu wao wa kimaadili, hadhi na heshima yao wakiwa na mavazi ya stara ya Kiislamu. Wanawake wa Kiirani hivi sasa  wana haki na uhuru sawa kabisa na wenzao wanaume. 

Wanawake wa Iran wanaweza kushiriki katika uchaguzi na kuwa wagombea ndani ya mipaka ya sheria. Kwa sasa mamia ya wawakilishi wanawake katika Majlisi ya Ushauri ya Kiislamu (Bunge) na mabaraza ya miji wanashughulika kuwahudumia wananchi. Wanawake pia wanafanya kazi katika mashirika 2,700 yasiyo ya kiserikali. Ajira za wanawake nazo pia zimeongezeka kwa kiasi kikubwa ikilinganishwa na kabla ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu, na sasa wanaunda asilimia 45 ya wafanyakazi wa serikali. Vilevile asilimia 25 ya nafasi za uongozi zinashikiliwa na wanawake wanaojituma na wataalamu.

Maendeleo ya wanawake katika shughuli za kijamii kwa kiasi kikubwa yanatokana na kuongezeka kwa kiwango chao cha elimu na utaalamu katika nyanya mbalimbali. Kabla ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu, ni 25% tu ya wanawake wa Iran waliokuwa wakijua kusoma na kuandika; lakini sasa takwimu hii inakaribia 95%. Idadi ya wanawake wanaohitimu vyuo vikuu katika ngazi mbalimbali pia imeongezeka kwa kiasi kikubwa. Takwimu za Wizara ya Sayansi, Utafiti na Teknolojia ya Iran zinaonyesha kuwa, takriban 60% ya wanafunzi na 35% ya wahadhiri wa vyuo vikuu ni wanawake.    ****

Wanawake wa Kiirani katika sekta ya sayansi na teknolojia 

Katika kipindi cha miaka 45 ya uhai wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, hatua kubwa zimechukuliwa kwa ajili ya kuimarisha afya ya wanawake hususan katika maeneo yenye maendeleo duni, kwa kadiri kwamba, kiwango cha wastani cha matarajio ya mtu kuishi (human life expectancy) miongoni mwa wanawake kimefikia miaka 78, ambacho ni kikubwa zaidi kuliko wastani wa dunia. Pia, vifo vya akina mama wajawazito vimepungua hadi kufikia 20 kwa kila wazazi hai 100,000, mafanikio ambayo hayaonekani isipokuwa katika nchi chache sana.

Katika uga wa michezo pia, wanawake wa Iran wamepata maendeleo makubwa. Kabla ya ushindi wa Mapinduzi, ya Kiislamu hapa nchini wanawake walikuwa wakishiriki katika michezo 7 tu, lakini sasa wanashiriki katika michezo zaidi ya 40 katika vilabu vyao makhsusi 8,000 na hadi sasa wameshinda medali 3,300 katika mashindano mbalimbali ya kimataifa. Jambo muhimu la kuashiria hapa ni kwamba, wanariadha wa kike wa Iran wanashiriki katika mashindano yote wakizingatia mavazi ya Kiislamu, ili kuonyesha utambulisho wao wa Kiislamu.

Hatupasi kusahau kuwa, baada ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu, wanawake wa Kiirani wamepata mafanikio makubwa katika nyanja nyingine nyingi kama vile sayansi na teknolojia, fasihi, sanaa na masuala ya kiutamaduni na kidini, jambo ambalo limedhihirisha zaidi nafasi yao katika maendeleo ya Iran ya Kiislamu.