Taathira ya Mapinduzi ya Kiislamu katika Hali ya Wanawake Kimataifa
Tuko katika siku za kukaribia kilele cha maadhimisho ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu; mapinduzi ambayo yameweza kuleta mabadiliko makubwa katika nyuga zote hasa katika masuala ya kiutamaduni, kijamii na kisiasa.
Moja ya mafanikio yaliyopatikana baada ya ushindi wa Mapinduzi ya
Kiislamu ni kubadilika mtazamo wa umma kuhusu wanawake. Kwa maneno
mengine ni kuwa, Mapinduzi ya Kiislamu ya mwaka 1979 yalifanikiwa kuleta
mtazamo mpya kuhusu wanawake na kupelekea mwanamke atazamwe kama mwenye
hadhi na thamani ya juu. Iwapo tutaangazia historia ya kushiriki
wanwake katika sekta za kijamii, kiutamaduni, kisayansi na kisiasa
duniani, tunaweza kusema kuwa hivi sasa mwanamke katika Jamhuri ya
Kiislamu ya Iran si tu kuwa anashiriki katika setka mbali mbali za
maisha kwa mafanikio katika dunia ya leo iliyojaa kiza, bali pia uwepo
wake umenawiri kiasi cha kuwa kigezo kwa mataifa yote. Mafanikio hayo
yameweza kupatikana kwa ajili ya tukio la aina yake katika zama hizi,
yaani Mapinduzi ya Kiislamu.
Kabla ya ushindi wa Mapinduzi ya
Kiislamu kulikuwa na misingi miwili ya kuwatazama wanawake. Awali
ilikuwa ni kuwatumia kama chombo cha kwa malengo mbali mbali na pili
ilikuwa ni kupuuza harakati zao za kijamii katika aghalabu ya nchi.
Baada ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu na kwa baraka za mtazamo wenye
kutazama mustakabali wa Imam Khomeini MA, muasisi wa Mapinduzi ya
Kiislamu, wanawake walianza kupewa nafasi kubwa katika harakati za kabla
ya ushindi wa Mapinduzi na baada ya hapo waliweza kupata hadhi yao ya
kibinadmau kwa maana halisi. Imam Khomeini MA, kama muasisi wa Mapinduzi
ya Kiislamu Iran si tu kuwa alizingatia kwa kina nafasi ya mwanamke
katika familia na hadhi yake kama mwenye kumjenga mwanadamu, bai pia
alisititiza kuhusu nafasi ya wanawake katika jamii na muelekeo huo
ulipelekea wanawake wa Iran wawe na harakati katika sekta mbali mbali za
jamii… Ushiriki wa kwanza wa wanawake ulishuhudiwa katika kujumuishwa
kwao katika harakati zilizopelekea ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu.
Kuafiki kushiriki wanawake pembeni mwa wanaume katika maandamano ya
mitaani ni jambo ambalo liliwapa utambulisho, umuhimu na itibari.
Mapinduzi ya Kiislamu yaliweza kuwapa wanawake utambulisho na hivyo
kubadilisha mtazamo potofu wa kuwadhalilisha….
Baada ya ushindi wa
Mapinduzi ya Kiislamu na punde baada ya hapo kufuatiwa na vita vya
kulazimishwa vya utawala wa Kibaath wa Iraq dhidi ya Iran, kulishuhudia
mtazamo mwingine wa mafanikio ya uwepo wanawake katika jamii ya Iran.
Katika kipindi hicho cha vita, wanawake walikuwa wakijishughulisha na
kutoa huduma za matibabu, mapishi n.k kwa wapiganaji waliokuwa katika
mstari wa mbele vitani. Wanawake walishiriki katika medani ya vita
katika kipindi chote cha miaka minane ya Kijihami Kutakatifu. Baada ya
vita uliendelezwa muelekeo huo wa Mapinduzi ya Kiislamu wa mtazamo wa
wastani kuhusu wanawake katika sekta mbali mbali za kijamii. Wanawake
wakiwa wanashirikiana na wanaume walijumuika katika ustawi na maendeleo
ya Iran. Kwa msingi huu, wanawake Wairani ni kigezo kwa wanawake
wanaotaka mabadiliko. Hivi sasa sifa ya kipekee ya ushijaa wa mwanamke
Muirani pamoja na subira yake isiyo na kikomo ni jambo ambalo limekuwa
ni mfano wa kuigwa wa mapambano na muqawama endelevu wa wanawake Ghaza,
Lebanon, Syria, Iraq, nchi za Kiafrika, Asia, Amerika ya Latini na hata
katika nchi za magharibi. Mtazamo wa wastani wa Mapinduzi ya Kiislamu
kwa wanawake ni jambo ambalo limepelekea kuwepo taathira katika misimamo
mikali kihusu nafasi ya mwanamke katika uga wa kimataifa.
Baada ya
zama za Renaissance (karne za 14-17) barani Ulaya , kulishuhudiwa
mabadiliko katika fikra na mtazamo wa dunia barani Ulaya ambapo
kulibuniwa nadharia ya kimaada na humanism. Hii ni nadharia iliyojengeka
katika msingi kuwa, la kutangulizwa mbele ni binadamu na mahitaji yake
tu na si dini. Kati ya nadharia hatari na za kufurutu ada zilizoibuka
katika zama hizo ni nadharia ya ufeministi. Nadharia hii imejengeka
katika msingi kuwa mwanaume ni sawa na mwanamke katika medani za
kisiasa, kijamii n.k.
Kwa itikadi ya wafeministi, tokea mwanzo wa
historia mwanamke amekuwa akidunishwa na hivyo akawa ni mwenye
kudhulumiwa haki zake. Kutokana na kuwa Wafeministi walikusudia kuondoa
vizingiti alivyowekwa mwanamke kwa msingi wa jinsia yake. Aidha
walipinga thamani za maadili bora huku wakifadhilisha makabiliano ya
mwanamke na mwanaume sambamba na kuvuruga msingi wa familia.
Halikadhalika wafeministi walitaka kuwepo uhusiano baridi baina ya
mwanume na mwanmke badala ya mahaba, mapenzi na ukuruba. Hali hii
ilipelekea kuporomoka maadili katika baadhi ya jaamii hasa za magharibi
ambapo kulishuhudiwa kuongezeka ufasiki, uavyaji mimba, mwanamke na
mwanaume kuishi pamoja pasina kufunga ndoa, uhusiano wa watu wa jinsia
moja n.k. mambo ambayo yalihatarisha usalama wa kiafya wa jamii ya
mwanadamu na kuvuruga misingi ya familia. Ingawa ufeministi katika jamii
za Magharibi uliibuka kutokana na dhulma walizokuwa wakitendewa
wanawake, lakini itikadi hiyo ilipoteza muelekeo kutokana na kufutwa
thamani za kiutamaduni na itikadi za kidini. Mtazamo mwingine usio
sahihi ni muelekeo wa mfumo wa kibepari wa magharibi kuhusu mwanamke.
Mwanamke katika jamii ya Magharibi kibepari hutazamwa chombo cha
kutumika kwa maslahi ya kiuchumi duniani. Katika jamii hiyo ya kibepari,
familia, thamani za kimaadili na utamaduni pia hupuuzwa na kudhoofishwa
kabisa. Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran yalikuwa na mtazamo wa wastani
kuhusu nafasi ya mwanamke. Mtazamo huo wa Kiislamu, ambao ulibainishwa
na Imam Khomeini, ulipelekea mwanamke kupata nafasi na hadhi yake
anayostahiki. Mfumo wa kibepari wa nchi za Magharibi haukumtazama
mwanamke kama mwanadamu kamili bali alikuwa ni chombo cha kibiashara kwa
lengo la kuridhisha matamanio ya mwanaume. Hali kama hii ilipelekea
mwanamke kutengwa zaidi, kuwa kama mfungwa na kutumbukia katika ufisadi.
Mtazamo wa pili kuhusu mwanamke ulikuwa ni ule wa kifeministi ambao
uliompkonya mwanamke thamani na itikadi zake na hilo lilipelekea kuenea
ufuska wa kiutamaduni na kuporomoka hadi ya mwanamke.
Kabla ya
ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu, si tu kuwa wafeministi katika nchi za
magharibi, bali pia hata ndani ya Iran walifanikiwa katika kutekeleza
baadhi ya mipango yao katika sekta mbali mbali za jamii kuanzia sekta za
sinema na utamaduni hadi katika idara za kazi, shule na vyuo vikuu
ambapo walieneza ufuska miongoni mwa wanawake. Lakini kufuatia ushindi
wa Mapinduzi ya Kiislamu na kukita mizizi mafundisho yaliyotokana na
mapinduzi hayo, ufeministi ulitambuliwa kama itikadi potovu na yenye
mafundisho ya kifasiki.
Mtazamo wa Kiislamu wanwastani wa viongozi
wa kidini Iran kuhusu nafasi ya mwanamke na ukosoaji wa mitazamo ya
kifeministi na kimagharibi katika uga wa kimataifa ni mambo ambayo
yalipelekea kuweza kufahamika mtazamo wa wastani, wa sahihi na wenye
kuzingatia uhalisia wa nafasi ya mwanamke. Kwa msingi huo jamii iliweza
kufuatia njia sahihi na kujiweka mbali na ufeministi. Mtazamo wa Imam
Khomeini MA kuhusu mwanamke kama mwenye kumlea mwanadamu ni mtazamo
ambao ulikinzana na ule wa magharibi kuhusu mwanamke. Katika upande wa
pili, kutokana na Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran, kwa mara ya kwanza
katika historia ya kisasa, utambulisho wa Kiislamu ulipata msimulizi
wake. Hii ni kwa sababu wanawake Waislamu duniani waliweza
kujitambulisha na mapambano ya kisiasa ya wanawake wa Iran. Wanawake wa
nchi zingine za Waislamu waliweza kuanzisha mikakati wa kupambana
utamaduni wa kimagharibi.
Matukio ya hivi karibuni ya mwamako wa
Kiislamu katika nchi za Mashariki ya Kati na Afrika Kaskazini na nafasi
ya wanawake katika mwamko huo ni jambo linaloashiria kuwepo utambulisho
wa Kiislamu na kuondolewa dhulma dhidi ya wanwake.
Kubainishwa
nafasi na shakhsia ya mwanamke katika Uislamu baada ya Mapinduzi ya
Kiislamu ni jambo ambalo lililobatilisha mitazamo isiyofaa kuhusu
mwanamke. La kusikitisha ni kuwa hivi sasa dunia inashuhdia mitazamo ya
pote la Uwahhabi na makundi ya kigaidi kama Daesh au ISIS kuhusu
wanawake. Kwa mtazamo wa kifikra na kiitikadi , ISIS ni kundi la wenye
kuwakufurisha Waislamu wasio afiki itikadi zao potovu. Kundi hili
linafuata msingi wa kifikra uliowekwa na mwanzilishi wa Uwahhabi,
Abdulwahab na pia mwananadharia maarufu wa Uwahhabi aitwaye Ibn Taimiya.
Wawili hao walikuwa na fikra zilizojaa taasubi na tafsiri zenye
misimamo mikali kuhusu Uislamu, misimamo ambayo inakinzana na Uislamu
halisi pamoja na akili katika masuala yote ya maisha. Kwa msingi huo
hatutazamii nchi kama Saudia yenye kufuatia misingi ya Uwahhabi kuwa na
mtazamo sahihi kuhusu mwanamke. Fikra ya Uwahhabi humtizama mwanamke
kama mwenye kutenda ufisadi na asiye na maadili. Ili kuujua mtazamo wa
Mawahhabi kuhusu wanawake inatosha kusoma fatwa za baadhi ya mamufti wa
pote hilo na hapo tutafahamu kina cha namna walivyozama katika upotovu.
Kwa mtazamo wa mamufti wa Kiwahhabi, uwepo wote wa mwanamke ni wa shari,
wanamtazama mwanamke kama shetani, wanaharamisha mwanamke kuendesha
gari na kwamba wanwake wanaoendesha gari wanapaswa kuuawa. Aidha
Mawahhabi wanaamini kuwa mwanaume anaweza kumpa talaka mke wake kwa njia
rahisi sana kama vile ujumbe mfupi wa simu ya mkononi. Halikadhalika
baadhi ya mamufti wa Kiwahhabi wameharamisha mwanamke kutumia intaneti.
Kwa msingi huo, tunaona ambavyo hivi sasa makundi wa Kiwahhabi na
magaidi wa ISIS katika eneo wanavyo mdhalilisha mwanamke kijinsia na
hata kuwauza na kuwanunua wanawake kama bidhaa sokoni katika maeneo
wanayoyadhibiti.
Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran yanapinga kikamilifu
mitamzamo kama hii ya misimamo mikali kuhusu wanawake. Ni kwa sababu hii
ndio mapinduzi ya Kiislamu yameweza kuleta mabadiliko mazuri katika
jamii mbali mbali.
Bi. Melanie Franklin ambaye sasa ni maarufu kama
Mardhiya Hashimi, ni Mwislamu Mmarekani ambaye hapa anazungumza namna
Mapinduzi ya Kiislamu yalivyomuathiri: "Binafsi nimeathiriwa na
Mapinduzi ya Kiislamu na shakhsia ya Imam Khomeini MA hasa kuhusu nafasi
na hadhi ya mwanamke. Kwa msingi huo nilifanya utafiti kuhusu Uislamu
na hatimaye nikasilimu na kufuata madhehebu ya Shia. Kwa hakika hilo
limetokana na ukarimu wa Mwenyezi Mungu."
Mapinduzi ya Kiislamu
yalimletea mwanamke mabadiliko na kuinua hadhi yake katika sekta mbali
mbali za kielimu, kiutamaduni na kijamii. Mazingira ya baada ya
Mapinduzi ya Kiislamu yalipelekea mwanamko kuwa na nafasi inayofaa
katika jamii na natija ya kuwa ni kuwaona wanawake Wairani wakiwa katika
sekta mbali mbali za umma sambamba na kushika nafasi muhimu za uongozi.
Wanawake Waislamu Wairani kwa kutegemea misingi ya Kiislamu na uelewa
sahihi wa thamani za maadili bora, uadilifu na kupinga dhulma wameweza
kujiunga na wanawake wapenda uhuru duniani na hivyo kuwa na taathira
katika mfumo wa kimataifa kw akushiriki katika makongamano ya kimataifa
na taasisi za kimataifa zisizo za kiserikali ambapo wamweza kuchangia
pakubwa katika kupitishwa maazimio ya kimataifa.