Mapinduzi ya Kiislamu na Sanaa ya Kiislamu
Assalaamu Alaykum wapenzi wasikilizaji na karibuni kusikiliza kipindi kingine maalumu tulichokuandalieni kwa mnasaba wa maadhimisho ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran. Kipindi hiki kinakujieni moja kwa moja kupitia Idhaa ya Kiswahili, Saut ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.
Katika hali ambayo Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran yanafanana na mapinduzi
mengine yaliyowahi kutokea katika nchi nyingine za dunia, lakini wakati
huohuo yanatofautiana na mapinduzi hayo kwa mitazamo kadhaa ambapo
uchunguzi na tathmini ya tofauti hizo inaweza kusaidia kueleweka vyema
athari za kiutamaduni, kisiasa na kiuchumi za mapinduzi hayo katika
mtazamo wa ndani na nje ya nchi. Moja ya tofauti muhimu za Mapinduzi ya
Kiislamu ya Iran na mapinduzi mengine ya dunia na ambayo huwa
haizingatiwi sana, ni kufungamanishwa kwa misingi ya kihistoria ya Iran
na mafundisho ya kimaanawi ya Uislamu kuhusiana na suala zima la sanaa,
jambo lililopelekea kubuniwa kwa maudhui inayofahamika kama Sanaa ya
Mapinduzi ya Kiislamu na kutumiwa maudhui hiyo katika kueneza
ulimwenguni ujumbe wa Mapinduzi ya Kiislamu.
Katika ulimwengu wa
sasa, kila harakati na fikra isiyofungamana na sanaa huwa haidumu kwa
muda mrefu wala kuenea sana. Sanaa ikiwa ni moja ya madhihirisho muhimu
zaidi ya utamaduni wa kila taifa huwa ni njia bora na yenye athari kubwa
katika kuarifisha na kufikisha ujumbe wa taifa hilo. Mapinduzi ya
Kiislamu pia hayakutoka kwenye kanuni hii na tokea mwanzoni yamekuwa na
uhusiano mkubwa na madhubuti na sanaa pamoja na fikra za wasanii wake.
Sanaa ya Mapiduzi ya Kiislamu ni sanaa maalumu ambayo ilidhihiri na
kuimarika katika muongo wa kwanza wa Mapinduzi ya Kiislamu na katika
katika kivuli cha thamani na fikra za kimapinduzi na miongozo ya
kiutamaduni, kisiasa na kijamii nchini. Tukio muhimu katika sanaa ya
Mapinduzi ya Kiislamu lilikuwa ni kutumiwa sanaa ya Kiirani na kunufaika
na baadhi ya sanaa ya kisasa kwa ajili ya kuwafikishia walimwengu fikra
na ujumbe wa Mapinduzi ya Kiislamu. Kwa hakika umri wa miaka 37 ya
Mapinduzi ya Kiislamu umekuwa na matunda makubwa ya kiutamaduni ikiwemo
sanaa. Katika kipindi hiki wasanii wa Iran wameweza kuwasilisha kwa njia
ya kuvutia maarifa ya kimaanawi, thamani na hamasa za Mapinduzi ya
Kiislamu kupitia sanaa.
Tunaweza kuchunguza nguzo muhimu za sanaa ya
Mapinduizi ya Kiislamu katika sehemu mbili za madhumuni na ujumi (kanuni
za uzuri au ubaya wa kazi za sanaa). Masuala muhimu ya madhmuni katika
sanaa ya Mapinduzi ya Kiislamu ni yale mambo yanayohusiana na maudhui ya
sanaa bila kujali namna sanaa hiyo inavyobainishwa na kusawalishwa.
Baadhi ya mambo hayo ni kama vile masuala ya kisiasa, kijamii na
kisaikolokia yanayotokana na harakati za Mapinduzi na kuendelea mbele,
mambo ya historia na shakhsia wa kidini, masuala ya kiitikadi na fikra
za Kiislamu. Kuondolewa kwa fikra za misingi ya falsafa na sanaa za
Magharibi na kuanzishwa kwa sanaa ya kupambana na hujuma ya kifikra na
kiutamaduni ya Magharibi.
Dini ni mojawapo ya masuala muhimu
yanayounda sanaa, lugha ya falsafa ya kina zaidi ya mwanadamu na
dhihirisho la maana bora zaidi ya kidini. Mtazamo wa kimaanawi ni moja
ya misingi muhimu ya sanaa ya Kiirani ambao daima umekuwa ukidhihiri kwa
namna tofauti katika kipindi chote cha historia ya Iran. Jambo hili
ambalo limekuwepo hata kabla ya ushindi wa Mapinduzi ya Iran lilikuwa
limedhoofishwa lakini lilihuishwa na kuimarishwa tena miongoni mwa
wasanii wa Iran kufuatia ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu. Kwa ibara
iliyo wazi zaidi ni kuwa Mapinduzi ya Kiislamu hayakukata wala
kudhoofisha uhusiano wake na utamaduni chanya na mkongwe wa Iran.
Kutokana na kuwa fikra ya Kiislamu inataka kujenga jamii iliyo bora na
safi kimaanawi, sanaa ya Kiislamu pia imesimama na kustawi kwa msingi
huo.
Ahmad Shakiri mwandishi wa Kiirani anasema kuhusiana na
mfungamano uliopo kati ya sanaa na Mapinduzi ya Kiislamu kuwa, kwa
mtazamo wa historia na sheria, kubainishwa sanaa kuhusu Mapinduzi ya
Kiislamu, kuna maana ya kukurubishwa sanaa hiyo na Mapinduzi ya Kiislamu
na athari zake. Anaendelea kusema kuwa kutokana na ukweli kwamba
Mapinduzi ya Kiislamu katika mtazamo wa kinadharia na misingi ya
kifikra, yalijengeka kwenye msingi wa kifikra na kiitikadi, sanaa
iliyodhihiri baada ya Mapinduzi pia ilikuwa na utambulisho wa kifikra.
Uchunguzi
wa sanaa baada ya Mapinduzi ya Kiislamu unabaini wazi kuwepo kiwango
kikubwa cha alama na mienendo ya kale katika sanaa ya leo. Katika upande
wa pili, wasanii wa siku hizi kwa kutumia mbinu za kuchagua mambo
chanya na kulinda thamani zao za usanii, hawajapuuza udharura wa
kuzingatiwa sanaa ya kisasa katika kazi zao za kiutamaduni. Hii ina
maana kwamba wanazingatia kwa pamoja sanaa za kale na za kisasa katika
kuendeleza shughuli zao za sanaa na usanii. Kwa kutambua vyema turathi
zao za kisanii, wasanii hawa wanaitazama sanaa ya Magharibi kwa mtazamo
wa utamaduni na mila zao za jadi na hivyo kufanya juhudi za kuboresha
turathi zao za kale kwa mtazamo huo. Kwa kutumia mbinu hiyo, wasanii wa
kipindi cha Mapinduzi ya Kiislamu wananufaika na uzoefu huo muhimu
katika kazi zao na hivyo kuleta ubunifu mpya katika usanii wao wa zama
hizi. Kwa mfano kushiriki wasanii wa uchoraji katika michoro na mabango
ya baada ya Mapinduzi ya Kiislamu ni thibitisho tosha katika uwanja huo.
Uchunguzi
wa athari za sanaa ya Iran katika taaluma mbalimbali unaonyesha wazi
kuwa sanaa hii kongwe imekuwa ikidumishwa kwa nguvu na udhaifu katika
vipindi tofauti vya historia ya nchi hii. Kwa kutazama athari tofauti za
kiusanii, tunatambua kwamba leo thamani za kimaanawi zimepewa nafasi
muhimu na ya juu, na wasanii wa Mapinduzi wamefutilia mbali sanaa
inayofungamana na mielekeo ya kabla ya Mapinduzi ya Kiislamu na kuweka
utambulisho wa Kiirani na Kiislamu mahala pake. Baada ya Mapinduzi ya
Kiislamu, wasanii wamekuwa na hamu kubwa ya kuwasilisha kazi zao katika
mfumo wa ujumi kwa madhumuni ya kuwaarifishia walimwengu utamaduni na
utambulisho wa Kiirani. Kazi za ujumi za wanasanaa hao kama ufumaji wa
mazulia unaofanywa kwa mikono, zinavutia na kuyashangaza mataifa yote
duniani. Kuna itikadi hii baina ya wanasanaa hao kwamba hata kama kazi
zao hazitakuwa na athari ya moja kwa moja kwa watu waliokusudiwa lakini
ujumbe wa kazi hizo za ujumi daima utaendelea kudumishwa na hivyo
kulinda thamani zake maalum. Kwa msingi huo licha ya wasanii kutumia
mbinu mbalimbali za ujumi na picha kuwasilisha thamani za kimaanawi za
Mapinduzi ya Kiislamu, wamekuwa wakitumia pia sanaa ya Iran katika
mitindo mipya kwa lengo la kuwafikishia walimwengu ujumbe halisi wa
Mapinduzi ya Kiislamu. Mfano mzuri wa jambo hilo katika uwanja wa sanaa
na usanii unaonekana wazi katika uwanja wa utengenezaji filamu ambapo
watengenezaji filamu wa Iran wamefanikiwa pakubwa katika ufikishaji
ujumbe huo katika pembe mbalimbali za dunia na hivyo kuwafanya wapate
umashuhuri kimataifa.
Na hadi hapa wapenzi wasikilizaji ndio
tumefikia mwishio wa kipindi chetu hiki maalumu, tulichokuandalieni
katika siku hizi za maadhimisho ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu ya
Iran. Basi hadi tutakapokutana tena wakati mwingine panapo majaaliwa,
tunakuageni nyote wapenzi wasikilizaji kwa kusema, Wassalaamu Alaykum
Warahmatullahi Wabarakaatuh.