Aug 05, 2023 15:11 UTC
  • Sura ya Adh-dhaariyaat, aya ya 15-23 (Darsa ya 955)

Wasikilizaji wapenzi wa Darsa ya Qur’ani, Assalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh. Bismillahir Rahmanir Rahim. Hamdu na sifa zote njema zinamstahikia Allah SWT, na rehma na amani zimshukie Mtume wake Mtukufu na Aali zake watoharifu.

Kwa taufiki yake Mola Karima aliyetupa uhai na uzima tumekutana tena katika mfululizo mwengine wa Darsa ya Qur’ani. Hii ni darsa ya 955 na sura tunayoizungumzia hivi sasa ni ya 51 ya Adh-Dhaariyaat. Tunaianza darsa yetu ya leo kwa aya ya 15 hadi ya 19 ya sura hiyo ambazo zinasema:

إِنَّ الْمُتَّقِينَ فِي جَنَّاتٍ وَعُيُونٍ

Hakika wachamngu watakuwa katika Mabustani na chemchem. 

آخِذِينَ مَا آتَاهُمْ رَبُّهُمْ ۚ إِنَّهُمْ كَانُوا قَبْلَ ذَٰلِكَ مُحْسِنِينَ

Wakipokea aliyo wapa Mola wao Mlezi. Kwa hakika hao walikuwa kabla ya haya wakifanya mema.

كَانُوا قَلِيلًا مِّنَ اللَّيْلِ مَا يَهْجَعُونَ

Walikuwa wakilala kidogo tu usiku. 

وَبِالْأَسْحَارِ هُمْ يَسْتَغْفِرُونَ 

Na wakiomba maghufira, nyakati za kabla ya alfajiri.

وَفِي أَمْوَالِهِمْ حَقٌّ لِّلسَّائِلِ وَالْمَحْرُومِ

Na katika mali zao ipo haki ya aombaye na ajizuiaye kuomba.

Mbinu mojawapo inayotumiwa na Qur’ani Tukufu kuwafunza na kuwalea watu ni kufanya ulinganishaji baina ya watu wema na wabaya. Katika darsa iliyopita tulisoma aya zilizowazungumzia wakanushaji wa Kiyama na watenda maovu. Mkabala wake, aya tulizosoma zimeelezea sifa nyingine za waja safi na wanaomcha Mwenyezi Mungu na kusema: watu hao watapata rehma na fadhila maalumu za Mola Siku ya Kiyama, kwa sababu hapa duniani walikuwa wakiwafanyia wema na ihsani wanadamu wenzao. Huenda hapa mtu atahoji na kusema: baadhi ya wanaokanusha ufufuo, nao pia wanatoa misaada kwa watu kwa sababu na kwa hisia za ubinadamu. Jibu ni kwamba, kwa upande wa waumini wenye nyoyo safi, mbali na kuwafanyia wema na ihsani waja wa Mwenyezi Mungu, wanajenga mawasiliano pia na Yeye Mola kwa kujikurubisha kwake kwa Sala, dua, dhikri na istighfari. Katika mchana wao, hufikiria kutatua shida na matatizo ya viumbe wenzao, na wakati wa usiku wanajielekeza kwa Mola wao ili kuimarisha mawasiliano ya kiroho na kimaanawi na Yeye Allah TWT. Baadhi ya mafunzo tunayopata kutokana na aya hizi ni kwamba, matunda ya kuzisamehe raha na starehe zinazomtumbukiza mtu kwenye lindi la madhambi katika dunia hii, ni kwenda kupata raha na starehe za milele katika ulimwengu wa akhera. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hizi ni kuwa, kwa upande mmoja, kujenga na kudumisha mawasiliano na Allah na kumuelekea Yeye Mola kwa Sala, dua, dhikri na munajati; na kwa upande mwingine kutoa misaada na kuwatendea wema na ihsani wanyonge na wahitaji katika jamii, ni mithili ya mbawa mbili zinazompaisha na kumfikisha mtu kwenye ulimwengu wa malakuti na saada ya milele. Na kwa hakika kuwa na moja tu kati ya mawili hayo hakuwezi kumfikisha mtu kwenye daraja hiyo. Halikadhalika aya hizi zinatuelimisha kwamba, kutenga sehemu ya usiku kwa ajili ya Sala na kunong’ona na Allah na kuwa tayari kuusamehe usingizi mtamu kwa ajili ya hayo ni miongoni mwa sifa za wachamngu wa kweli. Wa aidha aya hizi zinatuonyesha kuwa, muda wa kabla ya alfajiri ndio wakati bora wa kuleta istighfari na kuomba msamaha kwa Allah kwa makosa na madhambi tuliyofanya. Vilevile aya hizi zinatutaka tufahamu kwamba, sehemu ya mali inayotolewa kuwapa wanyonge na wahitaji, ni haki yao watu hao, kwa sababu Mwenyezi Mungu mwenyewe ameweka fungu maalumu katika mali za watu kuwa ni haki ya masikini na wahitaji. Kwa hivyo hatakiwi mtu awasimbulie na kuwasimanga kwa chochote kile anachowapa.

Darsa yetu ya leo inahitimishwa na aya ya 20 hadi ya 23 ya sura yetu ya Adh-Dhaariyaat ambazo zinasema:

وَفِي الْأَرْضِ آيَاتٌ لِّلْمُوقِنِينَ

Na katika ardhi zipo Ishara kwa wenye yakini. 

وَفِي أَنفُسِكُمْ ۚ أَفَلَا تُبْصِرُونَ

Na pia katika nafsi zenu - Je! Hamwoni?

وَفِي السَّمَاءِ رِزْقُكُمْ وَمَا تُوعَدُونَ

Na katika mbingu ziko riziki zenu na mliyo ahidiwa.

فَوَرَبِّ السَّمَاءِ وَالْأَرْضِ إِنَّهُ لَحَقٌّ مِّثْلَ مَا أَنَّكُمْ تَنطِقُونَ

Basi naapa kwa Mola Mlezi wa mbingu na ardhi, hakika haya ni kweli kama ilivyo kweli ya kwamba nyinyi mnasema. 

Baada ya aya tulizosoma katika darsa iliyopita kuzungumzia Kiyama, aya hizi zimerudia maudhui ya asili ya uumbaji na kuhoji kwa kusema: kwa nini mwanadamu hafumbui macho yake akatazama adhama ya uumbwaji wake yeye mwenyewe na ulimwengu uliomzunguka? Katika miongozo ya viongozi wateule wa dini, nukta hii imetiliwa mkazo kwa kauli isemayo:  “Man a’rafa nafsahu faqad a’arafa Rabbahu”, maana yake ni kwamba, atakayeitambua nafsi yake (kwa kujijua yeye hasa ni nani) basi bila shaka utambuzi huo utamfikisha kwenye kumjua Mola wake Mlezi aliyemuumba. Leo hii kuna kuna kozi kadha wa kadha za vyuo vikuu katika taaluma za sayansi ya utabibu na saikolojia ambazo kwa namna fulani zinatalii na kutafiti hali mbalimbali za mwanadamu kwa upande wa kimwili na kiroho, ili kupata ufahamu na utambuzi uliokamilika zaidi wa kumjua kiumbe huyo. Pamoja na hayo, na licha ya juhudi na bidii zote zilizofanywa na wataalamu juu ya suala hilo tunaweza kusema kuwa, hali nyingi zinazohusu ujudi na nafsi ya kiumbe mwanadamu bado hazijafahamika; na hadi sasa, mwanadamu angali ni kiumbe ambaye bado hajafahamika hasa alivyo. Hatua na marhala za ukuaji wa kiumbe mwanadamu, kuanzia kipindi anapokuwa kiinitete ndani ya tumbo la mama hadi anapofikia umri wa baleghe na wa mtu aliyepevuka kiakili, pamoja na uwezo na vipawa vya kustaajabisha alivyojaaliwa kuwa navyo, yote hayo ni miongoni mwa maajabu ya uumbaji, yanayoonyesha na kuthibitisha kwamba Mola Muumba alikuwa na uelewa kamili wa mahitaji yote ya kiumbe mwanadamu. Kila kimoja kati ya viungo vya mwili wa mtu, kama vile macho, masikio na meno au mifumo ya ndani ya kiwiliwili chake ukiwemo mzunguko wa damu, mmeng’enyo wa chakula na upumuaji au hata mfumo wake wa kinga ya mwili ni mambo yanayohitaji wataalamu bingwa na wabobezi wa kutalii na kufanya utafiti juu ya viungo na mifumo hiyo ili kupata ufahamu mpana na wa kina zaidi wa miundo yao na namna inavyofanya kazi. Kwa upande mwingine, sayari ya ardhi tunayoishi juu yake, umbali uliopo baina yake na jua na sayari nyinginezo, mizunguko yake mbalimbali ukiwemo wa kujizunguka yenyewe na kulizunguka jua, milima mirefu na mabonde mapana na ya kina pamoja na bahari kuu, ambazo ni vyanzo adhimu vya akiba ya maji ya sayari ya dunia, yote hayo ni miongoni mwa alama na ishara za ujuzi, tadbiri na uendeshaji mambo wa Allah SWT. Kusema kweli, ardhi hii ni mithili ya mama mkarimu, anayekidhi mahitaji yote ya kimaumbile ya mwanadamu na maelfu kwa maelfu ya aina za wanyama wanaoishi ndani yake. Udongo wake laini ni tandiko la kuoteshea juu yake anuai za mimea na miti itoayo kila aina ya matunda. Halikadhalika, ardhi hii imebeba juu yake milima imara iliyosimama wima na kuhifadhi pia ndani yake aina mbalimbali za madini na vitu vinginevyo vinavyohitajiwa na wanadamu. Ni wazi kwamba, yeyote yule atakayetafakari kwa umakini juu ya uumbwaji wa mwanadamu na ulimwengu uliomzunguka, atafikia kwenye hitimisho la kukiri juu ya kuwepo kwa Muumba mjuzi na mwenye hekima, ambaye kuumba kwake kumefanyika kwa hekima, tadbiri na umakini na kwa lengo lililotukuka la kumuumba mwanadamu katika ulimwengu huu. Lengo ambalo, bila ya shaka yoyote haliishii kwa kifo cha kiumbe huyo, bali linaendelea pia katika maisha ya baada ya kufa kwake. Miongoni mwa mafunzo tunayopata kutokana na aya hizi ni kwamba, moja ya mbinu inayotumia Qur’ani kumtambulisha Mola Muumba, ni kuyaelekeza macho, fikra na akili kwenye ishara za Mwenyezi Mungu katika ardhi ambazo zinamthibitishia mwanadamu juu ya kuwepo Mola Muumba, mwenye ujuzi na uwezo mutlaki. Ni wazi kwamba, maendeleo ya sayansi na ugunduzi wa siri mbalimbali zilizojificha kwenye ulimwengu wa maumbile vitazidi kudhihirisha siku baada ya siku alama na ishara za qudra na uwezo wa Allahu Jalla Jalaaluh katika ardhi. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hizi ni kuwa kujitambua mtu nafsi yake ni miongoni mwa njia bora za kumjua Mwenyezi Mungu, kwa sababu nafsi ya mtu humfikisha yeye mwenyewe kwenye elimu na ujuzi wa kumtambua Mola wake. Aidha, aya hizi zinatuonyesha kwamba, chimbuko la riziki liko angani; na ushirikiano wa mbingu na ardhi ndio unaomwandalia mwanadamu riziki yake. Mwanga wa jua, mawingu, upepo na mvua vinahuisha ardhi isiyo na uhai na kutoa riziki ya chakula kwa ajili ya viumbe wote wenye uhai. Vilevile aya hizi zinatutaka tujue kuwa, uwezo wa kutamka na kusema ni mojawapo ya at’iya na neema ya kipekee aliyojaaliwa mwanadamu na Mola Muumba, ambapo Yeye Allah ameutumia utamkaji na usemaji wa mwanadamu kutolea hakikisho la kuthibiti ahadi yake kwa waja wake. Wapenzi wasikilizaji, darsa ya 955 ya Qur’ani imefikia tamati. Tunamwomba Allah atuonyeshe haki na atupe taufiki ya kuifuata na atuonyeshe batili na kutuwezesha kuiepuka. Wassalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh…/