Aug 13, 2023 14:29 UTC
  • Sura ya At-T’uur, aya ya 1-12 (Darsa ya 960)

Wasikilizaji wapenzi wa Darsa ya Qur’ani, Assalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh. Bismillahir Rahmanir Rahim. Hamdu na sifa zote njema zinamstahikia Allah SWT, na rehma na amani zimshukie Mtume wake Mtukufu na Aali zake watoharifu.

Kwa taufiki yake Mola Karima aliyetupa uhai na uzima tumekutana tena katika mfululizo mwengine wa Darsa ya Qur’ani. Hii ni darsa ya 960. Baada ya kukamilisha tarjumi na maelezo kwa muhtasari ya sura ya 51 ya Adh-Dhaariyaat, katika darsa hii tutaanza kutoa tarjumi na maelezo kwa muhtasari ya sura ya 52 ya At-T’uur. Sura hii iliteremshwa Makka na ina aya 49. Maudhui kuu za aya zake kama ilivyo kwa akthari ya sura za Makka zinahusu masuala ya maadi, yaani kufufuliwa viumbe na hatima ya watu wema na wabaya Siku ya Kiyama. Baada ya utangulizi huo mfupi, sasa tunaianza darsa yetu hii kwa aya yake ya mwanzo hadi ya nne ambazo zinasema:

بِسْمِ اللَّهِ الرَّحْمَٰنِ الرَّحِيمِ

Kwa Jina la Allah Mwingi wa rehema, Mwenye kurehemu

وَالطُّورِ

Naapa kwa mlima wa T'ur,

وَكِتَابٍ مَّسْطُورٍ

Na Kitabu kilicho andikwa

فِي رَقٍّ مَّنشُورٍ

Katika waraka wa ngozi iliyo kunjuliwa, 

وَالْبَيْتِ الْمَعْمُورِ

Na kwa Nyumba iliyo jengwa,

Sura hii kama zilivyo baadhi ya sura nyingine za Qur’ani imeanza kwa viapo kadhaa. Viapo vya sura hii ni vya aina mbili: Aina ya kwanza ni ya kuapiwa vitu vitakatifu vya dini; na aina ya pili ni ya kuapiwa vitu vya kimaumbile. Kwa upande wa vitu vitakatifu vya dini, aya tulizosoma zimeapia vitu vitatu: Cha kwanza ni mlima T’uri, mahali alipokuwa akienda Nabii Musa AS kupokea wahyi wa Taurati. Kitu cha pili ni vitabu vitakatifu vya mbinguni, kikiwemo alichoteremshiwa Mtume huyo na walivyoteremshiwa Mitume wengine wa Allah ili kuwafikishia watu wa umati zao. Na kitu cha tatu kitakatifu kilichoapiwa katika aya hizi ni Al-Kaaba; kituo cha Tauhidi ardhini kilichojengwa upya na Nabii Ibrahim AS na kustawishwa katika zama zote za historia kwa mahudhurio ya mahujaji na waja wanaompwekesha Allah SWT. Baadhi ya mafunzo tunayopata kutokana na aya hizi ni kwamba, kukiapia kitabu, tena katika zama za ujahilia za watu waliokuwa hawajui kusoma wala kuandika, kunaashiria utukufu na thamani aali kiliyonayo kitabu na uandishi. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hizi ni kuwa, kutunza na kuhifadhi urithi ulioachwa na Mitume waliopita na kuenzi na kuendeleza utajo na kumbukumbu zao ni jukumu la dini zote na wala haliwahusu wafuasi wa dini maalumu. Halikadhalika tunajielimisha kutokana na aya hizi kwamba, vitabu vya mbinguni inapasa viandikwe juu ya vitu bora, madhubuti na vya kudumu na kuchapishwa kwa wingi ili ujumbe na mafundisho yake yaweze kuwafikia watu daima.

Tunaiendeleza darsa yetu kwa aya ya tano hadi ya nane ya sura yetu ya At-T’ur ambazo zinasema:

وَالسَّقْفِ الْمَرْفُوعِ

Na kwa dari iliyo nyanyuliwa juu,

وَالْبَحْرِ الْمَسْجُورِ

Na kwa bahari inayowaka,

 إِنَّ عَذَابَ رَبِّكَ لَوَاقِعٌ

Hakika adhabu ya Mola wako Mlezi hapana shaka itatokea.

مَّا لَهُ مِن دَافِعٍ

Hapana wa kuizuia.

Katika muendelezo wa viapo vilivyoanzia katika aya zilizotangulia, kwenye aya hizi tulizosoma zimeapiwa alama na ishara mbili muhimu za uumbaji. Ya kwanza ni mbingu iliyoinuliwa juu kabisa na yenye adhama ya ajabu, ambayo licha ya wanadamu kupiga hatua kubwa sana kielimu na kuunda aina chungu nzima za teleskopu zinazotumia teknolojia mpya kabisa na za kisasa, wanasayansi hawajaweza bado kuifahamu hakika yake kwa ukamilifu na kila siku tunasikia habari za kugunduliwa galaksi na maumbo mengine mapya ya angani. Na alama ya pili ni bahari yenye kuwaka, iliyofura na kututumka. Baadhi ya wafasiri wanasema, iliyokusudiwa hapa ni bahari inayotutumka kutokana na mada zinazoyeyuka na kuchemka, ambayo iko kwenye vina vya chini kabisa ya ardhi. Bahari hiyo, na katika nyakati tofauti, ndiyo inayofoka na kububujika kwenye tobo la volkano na kutawanyika kandokando yake. Lakini wafasiri wengine wanasema, zilizokusudiwa hapa ni bahari hizihizi za ardhini ambazo zitafura na kuwaka wakati wa kuwadia Kiyama na kutokea zilzala na tetemeko kubwa kabisa la ardhi. Baada ya kujiri matukio hayo, ndipo kitakaposimamishwa Kiyama chenyewe, ambayo itakuwa ni siku ngumu na nzito mno kwa waovu na madhalimu. Wakati huo, waovu hao hawatapata pa kukimbilia ili kuiepuka adhabu, wala hawatakuwa na kinga na kizuizi cha kuwalinda na madhara yake. Miongoni mwa mafunzo tunayopata kutokana na aya hizi ni kwamba, tukizitalii na kuzitafiti alama na ishara za Mwenyezi Mungu katika vitu vya maumbile tutabainikiwa na qudra na uwezo wa Mola wa kusimamisha Kiyama. Vilevile tunabainikiwa kutokana na aya hizi kuwa adhabu za duniani ni za muda na za kumalizika haraka, lakini adhabu kuu na halisi iko huko akhera na hakutakuwa na njia ya kuiepuka.

Tunaihitimisha darsa yetu ya leo kwa aya ya 9 hadi ya 12 za sura hii ya At-T’uur ambazo zinasema:

يَوْمَ تَمُورُ السَّمَاءُ مَوْرًا

Siku zitakapo tikisika mbingu kwa mtikiso,

وَتَسِيرُ الْجِبَالُ سَيْرًا

Na milima iwe inakwenda kwa mwendo mkubwa.

فَوَيْلٌ يَوْمَئِذٍ لِّلْمُكَذِّبِينَ

Basi ole wao siku hiyo hao wanao kadhibisha,

الَّذِينَ هُمْ فِي خَوْضٍ يَلْعَبُونَ

Ambao wanacheza katika mambo ya upuuzi. 

Aya hizi zinaendeleza yale yaliyozungumziwa katika aya zilizopita kwa kuashiria namna mbingu na ardhi zitakavyokuwa wakati wa kuwadia Kiyama na kueleza kwamba, mfumo na nidhamu inayotawala katika galaksi, sayari na maumbo ya angani itavurugika na nyota zitakengeuka mikondo zinayofuata; na mgongano utakaotokea baina yao utaijaza anga ya mbingu moshi na vumbi kubwa. Sayari hii ya ardhi ambayo sisi tunaishi juu yake, licha ya kuwa katika harakati na mwendo wa kujizunguka yenyewe na kulizunguka jua, lakini tunaiona imepoa na kutulia tuli, kiasi kwamba hatuhisi mtetemeko wala mtikisiko wowote na kwa hivyo tunaishi juu yake kwa raha na utulivu. Lakini kitakapokaribia Kiyama na kutokea zilzala kubwa na ya kutisha, milima na majabali yatang’oka na kutawanyika huku na kule. Aya hizi tulizosoma zinaashiria kwa ujumla nukta moja kuu, nayo ni kwamba wakati wa Kiyama, ulimwengu mwingine mpya wenye nidhamu na mifumo mipya utachukua nafasi ya ulimwengu huu uliopo. Ni wakati huo, mwanadamu atakuja kubainikiwa na matokeo ya amali na matendo yake. Siku hiyo waliokadhibisha Kiyama watazinduka na kutoka kwenye usingizi wa mghafala na kubaini makosa yao, lakini wapi! Kushuhudia ishara za Kiyama na adhabu, kukiri na kuungama na kujuta kwa maneno machafu waliyokuwa wakisema kuhusiana na Kiyama hakutawafalia kitu wakati huo wala kuwapunguzia chochote katika adhabu inayowangojea. Baadhi ya mafunzo tunayopata kutokana na aya hizi ni kwamba, kuvurugika kwa mfumo na nidhamu inayotawala dunia ni utangulizi wa kuletwa mfumo mwingine kwa ajili ya kusimama Kiyama; mfumo ambao sheria na kanuni zinazotawala ndani yake ni tofauti na kanuni za dunia hii ya kimaada. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hizi ni kuwa, wakanushaji wa Kiyama hawana mantiki wala hoja yoyote ya maana. Wayasemayo katika kukanusha Kiyama ni maneno batili na yasiyo na mashiko wanayoporoja kwa ajili ya kujichangamsha wao wenyewe na kuwapumbaza watu wengine. Wapenzi wasikilizaji, darsa ya 960 ya Qur’ani imefikia tamati. Tunamwomba Allah aijaalie kalima ya Tauhidi ya Laa Ilaha Illa-Llah idumu katika ndimi zetu na matendo yetu, hadi mwisho wa uhai wetu. Wassalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh…/

 

Tags