Aug 31, 2023 02:27 UTC
  • Alkhamisi, Agosti 31, 2023

Leo ni Alkhamisi Mwezi 14 Mfunguo Tano Safar, 1445 Hijria, sawa na tarehe 31 Agosti, 2023 Milaadia.

Katika siku kama ya leo miaka 813 iliyopita sawa na tarehe 14 Safar mwaka 632 Hijria alifariki dunia Abul Mahasin Bahauddin mashuhuri kwa jina la Ibn Shidad, fakihi, kadhi na mwanahistoria wa Kiislamu. Alizaliwa mwaka 539 huko Mosul, moja ya miji ya Iraq na alihifadhi Qur'ani akiwa bado mtoto na baadaye akajifunza hadithi, tafsiri na kusoma Qur'ani na kupata umahiri mkubwa katika taaluma hizo. Ibn Shidad alifanya safari katika nchi mbalimbali za Kiislamu kwa ajili ya kutafuta elimu. Miongoni mwa vitabu vyake mashuhuri ni an Nawadir al Sultwaniya, Dalailul Ah-kam na al Aswaa kinachozungumzia maisha ya Nabii Musa A.S. na mapambano yake dhidi ya Firauni. 

Miaka 438 iliyopita katika siku kama hii ya leo kwa mujibu wa kalenda ya Hijria, alizaliwa Mulla Muhsin Faidh Kashani, aliyekuwa faqihi, mpokezi wa hadithi, mwanafalsafa na arifu mkubwa wa Kiislamu nchini Iran. Faidh Kashani alipata elimu za fiqhi, hadithi, tafsiri na falsafa kwa wanazuoni wakubwa wa zama zake kama Muhammad Taqi Majlisi, Sheikh Bahai na Mulla Sadra. Msomi huyo mkubwa ameandika vitabu vingi, mashuhuri zaidi vikiwa ni tafsiri ya Qur'ani ya al Swafi, Mafatiihu Sharaai', al Wafi na al Mahajjatul Baidhaa.  ***

Miaka 202 iliyopita katika siku kama hii, yaani tarehe 31 Agosti 1821, alizaliwa mwanafizikia na tabibu  mashuhuri Hermann Ludwig Ferdinand von Helmholtz katika mji wa Potsdam nchini Ujerumani. Msomi huyo alihitimu masomo yake katika fani ya utabibu na mnamo mwaka 1849 alifikia daraja ya uprofesa wa fiziolojia na fizikia katika vyuo vikuu vya Berlin na Heidelberg. Japokuwa Helmholtz alitambulika zaidi kama mwanafizikia, mwanabiolojia na tabibu, lakini alikuwa mtaalamu wa hisabati na falsafa pia. Mwanafizikia huyo alitoa mchango mkubwa sana katika fani za electrodynamics na chemical thermodynamics. Katika uga wa falsafa, Herman Ludwig Ferdinand Von Helmholtz ndiye mwasisi wa falsafa ya sayansi, ambayo ni tawi la falsafa linalohusika na misingi, njia na matumizi ya sayansi. Msomi huyo alifariki dunia mwaka 1894 akiwa na umri wa miaka 73.

Hermann Ludwig Ferdinand von Helmholtz

Miaka 66 iliyopita, yaani tarehe 31 Agosti 1957 nchi ya Malaysia iliyoko mashariki ya bara la Asia ilipata uhuru wake kutoka kwa Uingereza. Watu wa Malaysia walianza kidogo kidogo kuingia katika Uislamu katika karne ya 13 Miladia. Ushawishi wa Wazungu kutoka Ulaya katika nchi hiyo ulianza mwanzoni mwa karne ya 16 alipowasili nchini humo baharia wa Kireno Afonso de Albuquerque. Mnamo karne ya 17 Uholanzi iliikalia na kuitawala Malaysia; na ulipofika mwaka 1824 na kufuatia mkataba wa makubaliano yaliyofikiwa baina ya Uingereza na Uholanzi, Malaysia ikatawaliwa na Uingereza na Indonesia ikakabidhiwa Uholanzi. Uingereza iliendelea kuitawala Malaysia hadi ilipopata uhuru wake katika siku kama ya leo.

Bendera ya Malaysia

Miaka 45 iliyopita katika siku kama hii ya leo, yaani tarehe 31 Agosti 1978, Imamu Musa Sadr alitoweka katika mazingira ya kutatanisha alipokuwa safarini nchini Libya. Imamu Musa Sadr alizaliwa tarehe 4 Juni mwaka 1928 katika mji wa Qum nchini Iran. Baada ya kumaliza masomo, mwaka 1959 alielekea Lebanon. Wakati huo, Waislamu wa nchi hiyo walikuwa na hali mbaya sana kijamii, kisiasa na kiuchumi. Kutokana na hali hiyo, Imamu Musa Sadr alichukua hatua kadhaa za msingi ili kuboresha hali zao na ndipo alipobuni taasisi ya kushughulikia masuala ya Waislamu wa Kishia iitwayo "Baraza Kuu la Mashia wa Lebanon". Taasisi hiyo ilipitishwa katika bunge la nchi hiyo na yeye akachaguliwa kuwa mkuu wake. Imamu Musa Sadr alikuwa pia akiunga mkono kikamilifu mapambano ya Wapalestina dhidi ya utawala haramu wa Kizayuni wa Israel; na kwa ajili hiyo akaanzisha "Harakatul-Mahrumin" ambayo ililenga kutetea haki za Waislamu wa Lebanon pia. Tangu Imamu Musa Sadr alipotoweka, zimefanyika jitihada nyingi na kubwa za kupata taarifa kuhusu hatima yake, lakini hadi sasa hazijazaa matunda.

Imamu Musa Sadr

 

Tags