Mchango wa Maulamaa wa Kishia Katika Uislamu (77)
Ni matumaini yangu kuwa, hamjambo wapenzi wasikilizaji popote pale mlipo na karibuni katika sehemu nyingine ya kipindi hiki cha Mchango wa Maulamaa wa Kishia Katika Uislamu, ili tuweze kwa pamoja kufungua ukurasa mwingine katika kurasa za historia ya Maulamaa na wanazuoni wa Kishia pamoja na mchango wao katika Uislamu.
Kipindi chetu cha leo ambacho ni sehemu ya 77 ya mfululizo huu kitamzungumzia Agha Nurullah Isfahani, mwanazuoni na alimu ambaye alikuwa na mchango mkubwa katika Uislamu. Nina wingi wa matumaini kuwa mtakuwa pamoja nami hadi mwisho wa kipindi hiki.
Mnamo mwaka 1278 Hijria sawa na 1861 Miladia, alizaliwa mtoto wa kiume kutoka katika kizazi cha mmoja wa Marajii wa Kishia ambaye alipewa jina la Mahdi. Yeye alikuwa mtoto wa tano wa Muhammad Baqir Isfahani, anayejulikana kama Masjid Shahi, na bibi yake mzaa baba alikuwa binti ya Sheikh Jafar Kashif al-Ghitaa.
Mahdi, ambaye baadaye aliondokea kuwa mashuhuri kwa jina la Nurullah, baada ya kujifunza mambo ya msingi kutoka kwa baba yake aliondoka na kuelekea Najaf akiwa na umri wa miaka kumi na saba akiwa na lengo la kujiendeleza zaidi kielimu.
Baada ya muda fulani, alipata lengo lake huko Samarra na akakimbilia kwenda kwa Mirza Shirazi mkubwa na akawa mmoja wa wanafunzi wake.
Nurullah Isfahani alikuwa na umri wa miaka ishirini na sita tu alipokuja kuwa mmoja wa wanachuoni na mafaqihi, na shakhsia wakubwa kama vile Mirza Shirazi na Mirza Habibullah Rashti walithibitisha daraja yake ya Ijtihad. Nurullah Isfahani alirejea Isfahan mwaka 1304 Hijria mwafaka na 1886 Miladia na kuanza shughuli zake za kisiasa na kijamii.
Wakati Shah wa Iran (mfalme wa Iran) alipouza fursa ya kununua na kuuza tumbaku kwa kampuni ya Uingereza kwa muda wa miaka hamsini, Shekhe Nurullah alikuwa miongoni mwa wapinzani wakubwa wa mkataba huu huko Isfahan, na wakati mwalimu wake, Mirza Shirazi Bozorg, alipotangaza matumizi ya tumbaku kuwa haramu, alikuwa miongoni mwa walioendelea kupambana katika njia hiyo hadi kupata ushindi.
Ukarimu wa kifalme wa watumishi utawala wa Shah haukuishia Ulaya na Uingereza tu kupitia mikataba mikubwa, bali uzembe, kutokuwa na ustahiki wa kuongoza na ukosefu wa hekima wa wafalme wa Iran daima ulisababisha matatizo kwa watu, na wanazuoni walijaribu kutatua matatizo hayo, lakini Nurullah Isfahani aliyekuwa mwanazuoni kijana wakati huo alikuwa akitafuta masuluhisho mapya ya kutatua matatizo.
Wakati Agha Nurullah alipoona soko la Iran limejaa bidhaa za kigeni na wafanyakazi na wakulima wanakabiliwa na matatizo ya kiuchumi, badala ya kuwaandikia barua watumishi wa baraza na kuwaonya, aliingia katika uwanja wa uchumi na kuanzisha taasisi za kiuchumi na moja ya taasisi hizo ni Islamic Company.
Alinufaika na uwezo wa mtandao uliounganishwa wa wasomi wa Kishia duniani na kupanua shirika lake la kiuchumi huko London, Calcutta, (Kolkata) Bombay, Cairo, Istanbul, Baghdad, Moscow na Badkoobeh.
Kampuni ya Isfahan Islamia na taasisi zingine zinazofanana na hiyo kwa hakika zilikuwa kampuni za hisa za umma ambazo Muirani yeyote angeweza kununua kuanzia hisa moja hadi elfu kumi, lakini wageni hawakuwa na haki ya kununua au kumiliki hisa za mashirika hayo.
Kwa mujibu wa sheria, ununuzi na uuzaji wa bidhaa zozote zisizo za Kiirani katika makampuni hayo ulipigwa marufuku, na nguvu zote za kifedha na kisheria za makampuni hayo zinapaswa kutumika katika ukuzaji wa uchumi wa ndani wa Iran.
Kuwepo kwa Haj Agha Nurullah na kaka yake, Agha Najafi na mafaqihi wengine katika uongozi wa taasisi hii, kulifanya mamlaka za Iraq kuiunga mkono na kuwaita watu kushiriki katika mipango yake.
Mafanikio ya makampuni hayo ya kiuchumi yalionekana vyema katika matoleo na machapisho makubwa ya siku hizo, hata machapisho ya Kiingereza yalitaja hatua hizi kuwa ni “kuwaamsha Wairani kutoka katika usingizi wao wa mghafala” na kuiona kuwa ni hatari kubwa kwao wenyewe.
Waingereza, kama kawaida, walijaribu kukabiliana na hatari hii kubwa kwa uwongo na kuzusha mifarakano. Waliwashutumu waanzilishi wa makampuni hayo kwa kutafuta faida na kujinufaisha binafsi na wakajaribu kuwazuia Wakristo wasijiunge na makampuni hayo ya Kiislamu kwa kuleta mfarakano kati ya Waislamu wa Iran na Wakristo. Hata hivyo, umakini na kuwa macho watu kuliwawafanya wasipate mafanikio yoyote ya maana katika uga huo.
Kazi na harakati zingine tofauti na za aina yake za Haj Agha Nurullah huko Isfahan ilikuwa ni kuanzisha mahali pa mjadala wa kidini na Wakristo. Wakati huo, ilikuwa imepita muda mrefu tangu wamisionari wa Kikristo kutoka Uingereza, Marekani na Ufaransa watumie njia mbalimbali, ikiwa ni pamoja na kuanzisha shule na hospitali kwa ajili ya kueneza Ukristo nchini Iran.
Hata hivyo ilikuwa takribani mwaka 1320 wakati mtu aliyejulikana kwa jina la William St. Clair Tisdall akiwa na kundi la wamisionari alikuwa amekwenda Isfahani na kusambaza kitabu cha Yanabiu al-Islam kilichokuwa kikitoa majibu dhidi ya Uislamu. Bwana huyo alidai katika kitabu chake hicho kwamba, licha ya miito yetu, Waislamu hawashiriki katika midahalo na mijadala na hawaandiki majibu ya ukosoaji wetu na kukanusha kwetu Uislamu.
Madai haya yalipelekea Haj Agha Nurullah kuunda jukwaa madhubuti na lenye utaratibu wa mjadala na dini zingine. Akiwa pamoja na kaka yake, Agha Najafi na kikundi cha wanazuoni wa kidini na wafanyabiashara wa Isfahan, waliunda chama na kuamua kuanzisha ofisi ya Da’awat al-Islamiyah "Wito wa Kiislamu". Waliita ofisi hii "Safakhane" na wakamteua rasmi Seyyid Muhammad Ali Da'i al-Islam na kumpa jukumu kufanya mijadala na wamisionari wa Kikristo huko Safakhaneh.
Da'i al-Islam alikuwa mmoja wa wahitimu wa Hawza ya Isfahan, ambaye alizoea kufanya vikao vya mijadala na Wakristo katika chumba chake. Alikuwa akifahamu vyema lugha za Kiingereza, Kiarabu, Kiebrania na Kiurdu na alikuwa akifahamu vizuri sana mafundisho ya vitabu vya Agano la Kale na Agano Jipya.
Ripoti za majadiliano na mijadala yake na wamisionari wa Kikristo zilikuwa zikichapishwa katika jarida la "Al-Islam", ambalo lilikuwa gazeti la kwanza la kidini nchini Iran, na kusambazwa kwa umma. Mijadala iliyojumuishwa katika jarida la kila mwezi la "Al-Islam" hivi karibuni imechapishwa katika kitabu kiitwacho "Safakhaneh Isfahan".
Nurullah Isfahani alikuwa mmoja wa waungaji mkono kindakindaki wa mapinduzi ya katiba nchini Iran, na sambamba na ushindi wa wapigania katiba, aliweka katika mipango yake suala la kuanzishwa kwa shule na hospitali mpya huko Isfahan.
Pia alifanya hima na idili kubwa kuhakikisha usalama wa barabara za jiji na vitongoji unapatikana kwa msaada wa makabila na watu. Panda shuka ya mapinduzi ya katiba na kuzuka Vita vya Kwanza vya Dunia vilimfanya kuondoka Isfahan mara kadhaa na kwenda Iraq, lakini hatimaye mnamo 1332 Hijria sawa na 1914 Miladia baada ya kifo cha kaka yake, Agha Najafi, alirejea katika mji wa Isfahan Iran na kubakia huko. Baadaye Agha Nurullah aliondokea kuwa mmoja wa wapinzani wa mfalme Reza Khan. Agha Nurullah aliugua ghafla na hatimaye aliaga dunia tarehe Mosi Rajab 1346 Hijria sawa na 1927 akiwa na umri wa miaka 70, umri ambao sehemu yake kubwa ilijaa harakati, hima, juhudi na mapambano ya kupigania Uislamu. Mwili wake ulisafirishwa na kwenda kuzikwa katika mji wa Najaf Iraq katika makaburi ya babu yake mzaa mama Sheikh Ja’afar Kashif al-Ghitaa.
Wapenzi wasikilizaji muda wa kipindi chetu kwa leo umefikia tamati tukutane tena juma lijalo katika sehemu nyingine na ukurasa mwingine wa mwanazuoni mwingi katika mfululizo wa vipindi hivi vya Mchango wa Maulamaa wa Kishia Katika Uislamu. Asanteni kwa kunitegea sikio na kwaherini.