Nov 27, 2023 05:07 UTC
  • Palestina, Suala Kuu la Umma wa Kiislamu 3

Assalaam Alaykum wapenzi wasikilizaji wa Idhaa ya Kiswahili, Sauti ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inayokutangazieni kutoka mjini Tehran. Tunaendelea kuzungumzia kwa ufupi historia ya ardhi ya Palestina kabla ya kudhihiri dini ya Uislamu. Tunakuombeni muwe pamoja nasi hadi mwisho wa kipindi, karibuni.

Palestina ni ardhi takatifu kwa dini zote za mbinguni na kimsingi historia ya ardhi hii inaanza kwa majina ya Mitume watukufu wa Mwenyezi Mungu. Kwa mujibu wa wanahistoria, Palestina imekuwa mahali pa kuishi wanadamu tangu Enzi za Mawe na imeshuhudia hatua za maendeleo ya maisha ya mwanadamu kutoka enzi za kuhamahama hadi enzi za kilimo. Ardhi hii daima imekuwa kiunganishi cha ustaarabu na mahali pa kuteremkia na kupanuka dini za mbinguni na  hivyo kuwa kitovu cha mazingatio na heshima kwa wafuasi wa dini kuu duniani na mataifa yote ulimwenguni. Katika mfululizo wa vipindi hivi, tunakusudia kuzungumzia sababu za umuhimu wa ardhi hii kwa dini ya Uislamu na wafuasi wake, na ni kwa nini suala la Palestina ni moja ya masuala muhimu katika ulimwengu wa Kiislamu. Tunazungumzia historia ya ardhi hii ili upate kujua zaidi mpenzi msikilizaji, umuhimu wake kwa Uislamu bali kwa dini zote za mbinguni na jamii ya mwanadamu kwa ujumla. Tunakuomba uwe pamoja nasi katika sehemu hii ya tatu ya mfululizo wa vipindi vya "Palestina, Suala Kuu la Umma wa Kiislamu." Karibu.

Tulisema katika kipindi kilichopita kwamba uasi na kutotii Bani Israel amri ya Mtume wao Nabii Musa (as) kuliwafanya waadhibiwe na Mwenyezi Mungu kwa kuwaacha watangatange jangwani kwa miaka 40 na kutoruhusiwa kuingia katika ardhi ya Palestina hadi pale mtume huyo alipoaga dunia. Baada ya kauga dunia Nabii Musa (as), Bani Israel waliongozwa na Yusha' Wasii wa Nabii Musa (as) kuvuka Mto Jodan na kuingia katika mji wa Jericho katika ardhi ya Palestina. Mbali na Jericho na kadiri miaka ilivyosonga mbele, waliteka, kutawala na kudhibiti miji mingine mingi katika ardhi hiyo tukufu wakiongozwa na Mitume na wafalme wengine wa Bani Israel kama vile Talut (Shaol), kisha Nabii Dawood (as) na Nabii Suleiman (as)  hadi takriban miaka 500 kabla ya kuzaliwa Isa Masih (as).

Wakati wa Nabii Dawood na baada ya hapo katika zama za Nabii Suleiman (as), Bani Israel walipata utukufu na nguvu kubwa. Nabii Daudi (as) alitawala sehemu kubwa ya ardhi ya Palestina na karibu mwaka 1000 kabla ya kuzaliwa Yesu Kristo, aliweza kuiondoa Yerusalemu (Quds) kutoka mikononi mwa Wapalestina na kuanza kujenga huko mji wa Beitul Muqaddas na kuufanya kuwa mji mkuu wa utawala wake. Kwa mtazamo wa kisiasa, kipindi cha utawala wa Nabii Dawood kinachukuliwa kuwa kipindi cha dhahabu cha utawala wa Bani Israel. Baada ya kuaga dunia Nabii Dawood utawala wa Bani Israel ulichukuliwa na mwanae Nabii Suleiman (as) na kukamilisha ujenzi wa Beitul Muqaddas. Katika kipindi cha uongozi wake, Palestina ilishuhudia maendeleo na ustawi mkubwa. Katika zama hizo, Bani Israel waliteka na kudhibiti ardhi kubwa yenye rutuba na iliyostawi ya Palestina. Baada ya kuaga dunia Nabii Suleiman (as) Mayahudi walihitilafiana kuhusu mrithi wa utawala huo. Makabila kumi ya Bani Israel yalikataa kula kiapo cha utiifu na kumbai mwana wa Sulemani, Rehoboam, na ni makabila mawili tu ya Yahuda na Benjamin ndiyo yalikula kiapo cha utiifu kwake. Tofauti hizo zilipelekea ufalme huo kugawanyika katika makundi mawili ya "Ufalme wa Yahuda (Yuda)" na "Ufalme wa Kaskazini". Mizozo, vita na umwagaji damu kati ya tawala hizo mbili uliibuka na kupelekea utawala wa Mayuda kuushinda utawala wa Kaskazini. Serikali ya Mayuda (Mayahudi) ilipinduliwa na Bakht al-Nasr, mfalme wa Babeli aliyekuwa na kiu ya kumwaga damu, na hapo Palestina ikaunganishwa na utawala wa Wakaldayo, na Mayahudi wakafanywa watumwa.

Ukimbizi wa Mayahudi uliendelea hadi wakati wa shambulio la Kuroush, mfalme wa Iran ambaye aliangamiza utawala wa Babeli. Kuroush aliikomboa Babeli  na kuwaruhusu Mayahudi warejee Jerusalem (Quds). Kwa kupinduliwa utawala wa Babeli na Kuroush wa ukoo wa Waamenidi (Achaemenid), Palestina ikawa chini ya utawala wa Waamenidi, ambapo ufalme wa Iran uliwasaidia sana Mayahudi kujenga upya Yerusalemu (Quds) na kuukarabati tena mji huo. Yerusalemu iliendelea kuwa katika hali ya utulivu hadi mwisho wa utawala wa Daryush III, mmoja wa wafalme wa nasaba ya Waamenidi wa Iran (381 hadi 330 BC) hadi Alexander wa Macedonia alipozishambulia Iran, Misri, Syria na Palestina karibu 323 BC na kusababisha uharibifu, mauaji na uporaji mkubwa katika nchi hizo. Tangu wakati huo, Yerusalemu na Palestina zikatawaliwa kikamilifu na Wagiriki.

Kuroush akiwa Babeli

Baada ya Alexander wa Macedonia, warithi wake walitawala na kuidhibiti Palestina kwa kipindi fulani lakini hawakuweza kuitawala kwa miaka mingi ambapo Warumi waliwashambulia na kuchukua udhibiti wa maeneo mengi ya ardhi hiyo tukufu kupitia vita vingi vilivyopiganwa katika miongo ya 70 na 80 baada ya kuzaliwa Nabii Isa Masih (as). Wakati huo, Yerusalemu iliporwa; Hekalu la Pili, ambalo lilijengwa upya wakati wa utawala wa Waamenidi, liliharibiwa, na ni ukuta wa Magharibi tu ndio uliobaki. Kufuatia udhibiti wa utawala wa Warumi huko Yerusalemu na licha ya hali nzuri iliyotawala Palestina katika miaka iliyofuata, Mayahudi walirejelea tena tabia yao ya kutotii amri na kupanga njama na hivyo kuanzisha njama dhidi ya utawala wa Warumi. Jambo hilo liliwakasirisha sana watawala wa Kirumi ambao waliamua kuwachukulia hatua na kuwaadhibu. Kwa hivyo, mwaka 135 BC, Hadrian, mfalme wa Roma, aliwafukuza Mayahudi kutoka Yerusalemu na kuwapiga marufuku kuingia, kuishi au hata kuukaribia mji huo. Wakati wote huo, Palestina ikawa sehemu ya utawala wa kisiasa na kiutendaji wa Milki ya Roma.

Katika kipindi cha utawala wa Warumi huko Palestina, Isa Masih (as) (Yesu Kristo) alizaliwa katika mji wa Beit Laham (Bathlehemu), moja ya miji ya kihistoria ya Palestina na kuleta ujumbe wa dini mpya. Makuhani wa Kiyahudi walichukulia dini hiyo pamoja na Masih, Mtume mpya kuwa hatari kubwa kwa utawala na udhibiti wao wa kidini, kisiasa na kiuchumi huko Palestina. Kwa msingi huo Wakanaani na Wapalestina ambao walikubali na kufuata dini hiyo mpya walikabiliwa na mateso na maudhi makubwa kutoka kwa Mayahudi hao. Kwa lengo la kukabiliana na dini hiyo mpya na kuzuia kuenea kwake, makuhani wa Kiyahudi walikuwa wakienda kwenye makasri ya wafalme wa Kiroma na kufanya uchochezi na fitina dhidi ya Masih (as), wanafunzi na wafuasi wake. Hatimaye mfalme wa Roma akasalimu amri mbele ya mashinikizo ya makuhani hao wa Kiyahudi na kutoa amri ya kusulubiwa Nabii Isa (as). Kwa mujibu wa riwaya hiyo, Nabii Isah (as) alisulubiwa juu ya mlima Jaljala (az-Zaitun) mjini Yerusalemu na kisha kupaishwa mbinguni. Bila shaka Qur'ani Tukufu, Kitabu Kitakatifu cha Waislamu, inakanusha kusulubiwa Nabii Isa (as), lakini pamoja na hayo inafafanua njama, uchochezi na fitina za Mayahudi kwa ajili ya kusulubiwa Nabii huyo mtukufu (as).

Warumi walipokubali na kuingia katika dini ya Ukristo na kugawanyika utawala wa Roma, Constantinople ukawa mji mkuu wa utawala wa Roma ya Mashariki, ambapo kabla ya hapo ulikuwa ukiitwa Byzantium. Malkia Helena, mama yake Mtawala  wa Constantinople, alitembelea Palestina mnamo 326 Miladia na akajenga Kanisa la Ufufuo huko Jerusalem na Kanisa la Al-Mahd huko Beit Lahm (Bethlehem). Baadaye, wakati wa Dola la Byzantine, karibu 390 Milaadia, Palestina iligawanywa katika maeneo matatu: Palestina ya Kwanza, Palestina ya Pili, na Palestina ya Tatu: Palestina ya Kwanza ilijumuisha Yahud (Yudea), Samaria, Sahel, na Ardhi Takatifu. Palestina ya Pili ilijumuisha Jimbo la Jalil (Galilaya), Jezreeli, Maeneo ya Mashariki ya Jimbo la Galilaya na Sehemu ya Magharibi ya Dekapolis ya zamani. Palestina ya Tatu nayo ilijumuisha Jordan Kusini, ambayo hapo zamani ilikuwa sehemu ya eneo la Waarabu. Jina lingine la Palestina ya Tatu lilikuwa Palestina Salutaris. Mgawanyo huu uliweka eneo la Waarabu kama sehemu ya Jordan Kaskazini mashariki mwa Ardhi Takatifu.

Kanisa la Kiyama (Kanisa la Ufufuo) katika eneo la kihistoria la Quds

Utawala wa Byzantine Palestina ulimalizika kwa muda wakati ilipotekwa na Waajemi mnamo 614, kwa kutilia maanani kuwa wakati huo, Khosrow Parviz, mfalme wa Wasassanidi, aliwashinda askari wa Kirumi na kuuteka mji wa Yerusalemu (Palestina) kwa mwongozo wa Mayahudi ambao walikuwa wakishirikiana na Iran. Lakini baada ya kuaga dunia Khosrow Parviz, ardhi hiyo iliangukia tena mikononi mwa Wakristo. Wakati huo, dini ya Uislamu ilikuwa imedhihiri katika ardhi ya Uarabuni na Bara Arabu, na hivyo kuibua matukio mapya duniani, hasa katika ardhi ya Palestina. Tutajadili suala hilo katika kipindi chetu kijacho, Inshallah, kwaherini.