Jumapili, 17 Disemba, 2023
Leo ni Jumapili tarehe Tatu Mfunguo Tisa Jamad Thani 1445 Hijria mwafaka na tarehe 17 Disemba 2023.
Siku kama ya leo miaka 1434 iliyopita alikufa shahidi Bibi Fatima al Zahra, binti mtukufu wa Mtume wetu Muhammad (saw) na mke wa Imam Ali bin Abi Twalib (as). Alizaliwa miaka mitano baada ya kubaathiwa Nabii Muhammad (saw) na mtukufu huyo akampa jina la Fatima. Alipewa malezi na wazazi wake wawili yaani Bibi Khadija na Mtume wa Mwenyezi Mungu na kupata maarifa aali ya dini kutoka kwa baba yake. Bibi Fatima alifikia daraja za juu za ukamilifu wa kiroho na kimaanawi ndani ya nyumba ya wahyi na ufunuo. Baada ya kuolewa na Imam Ali bin Abi Twalib ambaye alikuwa kielelezo halisi cha takwa na uadilifu, Bibi Fatima alikuwa na nafasi kubwa na alitoa mchango wa aina yake katika jamii ya Kiislamu. Alikuwa dhihirisho la uchamungu, ukarimu, kujitolea, subira, kujipinda katika ibada na kuwasaidia watu wote na alilea watu adhimu kama Imam Hassan na Hussein (as). ***

Katikka siku kama ya leo miaka 786 iliyopita, kwa mujibu wa kalenda ya Hijria alifariki dunia Abu Bakr Muhammad bin Ahmad maarufu kwa jina la Ibn Sayyidun-Naas, faqihi, mtaalamu wa hadithi, mwanahistoria na msomi wa fasihi wa Andalusia au Hispania ya leo. Mwanazuoni huyo alifariki dunia nchini Tunisia. Ibn Sayyidun-Naas alizaliwa mwaka 597 Hijiria katika viunga vya mji wa Seville (Ishbilia) huko Uhispania na kuanza kujishughulisha na masomo. Abu Bakr Muhammad bin Ahmad alifundisha kwa miaka mingi katika eneo hilo na kulea wanafunzi wengi. Msomi huyo alitabahari pia katika taaluma ya mashairi na fasihi; na mashairi yake mengi yanamsifu Mtume Muhammad (saw). Miongoni mwa vitabu vya msomi huyo ni kile cha Sira na Maisha ya Mtume Muhammad (saw). ***

Miaka 245 iliyopita katika siku kama ya leo, alizaliwa Humphrey Davy mwanakemia na mwanafikizia wa Kiingereza. Katika majaribio yake ya kimaabara, msomi huyo aliweza kutenganisha elementi za Sodium, Potassium, Calcium, Barium, Magnesium na Strontium miongoni mwa elementi nyinginezo na hatua hiyo ilihesabiwa katika zama hizo kuwa mafanikio makubwa katika sayansi ya kemia. Davy mbali na kuwa mwasisi wa elimu inayojulikana kama "electrochemical", aliweza pia kuwasilisha nadharia ambayo iliitaja gesi ya Hydrojen kuwa gesi inayoweza kuzitambua asidi. Mwanakemia huyo wa Kiingereza alifariki dunia mwaka 1829 Miladia. ***
Katika siku kama ya leo miaka 120 iliyopita inayosadifiana na tarehe 17 Disemba mwaka 1903, ndege ya kwanza duniani iliyokuwa ikitumia injini ya mota, ilifanikiwa kuruka na kupaa angani kwa dakika moja baada ya kufanyiwa majaribio kadhaa. Ndege hiyo ilitengenezwa na ndugu wawili walioitwa Wilbur na Orville Wrights na kufanyiwa majaribio katika jimbo la North Carolina nchini Marekani. Ndugu hao wawili walikuwa watengeneza baiskeli ambao baadaye walipatwa na shauku kubwa ya kutengeneza ndege yenye kutumia injini ya mota. ***
Miaka 32 iliyopita katika siku kama ya leo mwili wa Mhandisi Muhammad Javad Tondguyan, Waziri wa Mafuta wa wakati huo wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ulirejeshwa nchini Iran kutoka Iraq baada ya kupita miaka 11. Waziri Tondguyan na maafisa wengine kadhaa wa wizara hiyo walitekwa nyara na wanajeshi wavamizi wa Iraq wakati walipokuwa katika ziara ya kutembelea visima vya mafuta vya kusini mwa Iran. Waziri huyo na wenzake walitekwa nyara mwezi mmoja baada ya Iraq kuvamia ardhi ya Iran. Utawala wa Saddam wakati huo uliendelea kukanusha kutekwa nyara Mhandisi Tondguyan kwa muda fulani, lakini hatimaye ulikiri kumteka nyara waziri huyo wa zamani wa mafuta wa Iran. Uchunguzi wa kidaktari na ushahidi uliotolewa na watu waliokuwa karibu na Waziri Muhammad Jawad Tondguyan ulithibitisha kwamba waziri huyo wa zamani wa mafuta wa Iran alikufa shahidi kutokana na kuteswa na askari jeshi wa utawala wa Baath wa Iraq. ***
Siku kama ya leo miaka 31 iliyopita, sawa na tarehe 17 Disemba mwaka 1992 utawala wa Kizayuni wa Israel, kwa kisingizio cha kuuawa polisi wake mmoja wa mpakani, uliwabaidisha kusini mwa Lebanon viongozi 415 wa harakati ya Jihadul Islam na Hamas kutoka Palestina. Baada ya serikali ya Lebanon kupinga hatua hiyo isiyo ya kibinadamu na kukataa kuwapokea Wapalestina hao, hasira na upinzani wa ulimwengu wa Kiislamu ulilifanya Baraza la Usalama kupitisha azimio nambari 977 lililolaani hatua hiyo ya Tel Aviv na kutaka kurejeshwa Wapalestina hao waliobaidishwa nchini kwao. ***

Tarehe 17 Disemba miaka 13 iliyopita kijana mmoja wa Kitunisia aliyejulikana kwa jina la Tariq Mohamed Bouazizi alijiteketeza kwa moto na kuanzisha harakati ya ukombozi wa wananchi wa nchi hiyo dhidi ya utawala wa kidikteta wa Habib Bourguiba na Zainul Abidin bin Ali uliodumu kwa kipindi cha nusu karne. Kujichoma moto kwa Bouazizi ilikuwa cheche ya harakati ya mapinduzi ya wananchi wa Tunisia na katika nchi nyingine za Kiarabu kama Misri, Libya, Yemen na Bahrain dhidi ya watawala dhalimu na vibaraka wa Magharibi. Bouazizi ambaye alikuwa na shahada ya Chuo Kikuu alikuwa akiuza bidhaa za mkononi mitaani aliponyanganywa bidhaa zake na kudhalilishwa na afisa wa kike wa halmashauri ya mji na ndipo alipoamua kujiteketeza kwa moto, kitendo ambacho kiliamsha hasira za wananchi wa Tunisia na kuwa chachu ya harakati iliyohitimisha utawala wa dikteta Zainul Abidin. ***