Dec 18, 2023 23:08 UTC
  • Jumanne, Disemba 19, 2023

Leo ni Jumanne tarehe 5 Mfunguo Tisa Jamadithani 1445 Hijria sawa na tarehe 19 Disemba 2023.

Siku kama ya leo miaka 1017 iliyopita, inayosadifiana na tarehe na tarehe 5 Mfunguo Tisa Jamadi Thani mwaka 428 Hijria, alifariki dunia Abul Hassan Mahyar  Deilami, mshairi na mwandishi mashuhuri wa Kiirani. Awali msomi huyo alikuwa mfuasi wa dini ya Kizartoshti, hata hivyo kutokana na kupata elimu na miongozo kutoka kwa wasomi mashuhuri katika zama zake, hatimaye alisilimu na kuingia katika dini ya Kiislamu. Kwa muda mrefu Deilami alisoma kwa mwalimu wake Sayyid Radhi.

Katika siku kama ya leo miaka 825 iliyopita, aliaga dunia huko Damascus Syria Ibn Qudamah Moqaddasi fakihi na mpokezi hadithi wa Kiislamu. Ibn Qudamah alihitimu masomo yake ya awali na ya utangulizi huko Damascus ambapo alijifunza Qur'ani na hadithi. Baadaye alifanya safari huko Baghdad katika Iraq ya leo na kuhudhuria masomo ya maulama na wanazuoni wakubwa katika zama hizo. Ibn Qudamah hakuwa nyuma pia katika uwanja wa uandishi wa vitabu na amevirithisha vizazi vilivyokuja baada yake vitabu vyenye thamani kubwa. Kitabu cha Raudhatun Nadhir ni moja tu kati ya vitabu hivyo.

Miaka 773 iliyopita katika siku kama ya leo kwa mujibu wa kalenda ya Hijria, aliaga dunia Maulana Jalaluddin Balkhi maarufu kwa jina la Moulavi mmoja wa malenga na washairi mahiri wa Iran.  Moulavi alikuwa mshairi mkubwa na mwenye uwezo na kipaji kikubwa katika karne ya 7 Hijria. Alizaliwa mwaka 604 Hijria katika mji wa Balkhi kaskazini mwa Afghanistan ya leo. Miongoni mwa athari kubwa za Maulana au Jalaluddin Balkhi ni kitabu cha mashairi cha Masnavi Manavi.

Katika siku kama ya leo miaka 236 iliyopita mwafaka na tarehe 19 Disemba 1787, nchi ya Kiafrika ya Sierra Leone iliunganishwa na Uingereza baada ya kupita miaka 327 tangu ardhi ya nchi hiyo igunduliwe na wazungu. Sierra Leone "iligunduliwa" na mtalii wa Uhispania na kukoloniwa. Katika miaka ya kukoloniwa kwake na Uhispania, maelfu ya wanaume na wanawake wa Sierra Leone walichukuliwa watumwa na kwenda kuuzwa katika masoko ya Ulaya. Mwenendo huo uliendelea pia baada ya Waingereza kuishinda Uhispania na kuanza ukoloni wa Uingereza nchini humo. Mwaka 1961 Sierra Leone ilianza kujitawala na kuwa na utawala unaosimamiwa na jeshi, na mwaka 1971 ikawa na utawala wa Jamhuri.   

Bendera ya Sierra Leone

Miaka 117 iliyopita katika siku kama hii ya leo alizaliwa kiongozi wa Urusi ya zamani, Leonid Brezhnev katika familia maskini nchini Ukraine. Mwaka 1931, Leonid Brezhnev alijiunga na kuwa mwanachama wa chama hicho cha Kikomonisti. Brezhnev alitwaa uwaziri mkuu wa Russia na uongozi wa Chama cha Kikomonisti cha Urusi ya zamani mwaka 1964 wakati Nikita Khrushchev alipokuwa safarini nje ya nchi. Mashambulizi dhidi ya Czechoslovakia na kukaliwa kijeshi Afghanistan yalifanyika katika zama zake. 

Leonid Brezhnev

Miaka 33 iliyopita katika siku kama ya leo, Sadeq Ganji mwambata wa Kituo cha Utamaduni cha Jamhuri ya Kiislamu ya Iran huko Lahore Pakistan alishambuliwa kwa risasi na vibaraka wa ubeberu wa kimataifa na kuuawa shahidi. Kwa karibu miaka minne Ganji alikuwa akitekeleza jukumu lake la kutangaza na kuziarifisha thamani aali za Kiislamu na kupanua uhusiano wa kiutamaduni baina ya wananchi wa Iran na Pakistan. Sadeq Ganjia aliuawa shahidi akiwa amekaribia kurejea hapa nchini baada ya hafla ya kumuaga iliyoandaliwa na wana utamaduni na shakhsia wa kielimu na kifasihi wa Lahore Pakistan.   

Sadeq Ganji

Na siku kama ya leo miaka 51  iliyopita, inayosadifiana na 19 Disemba 1972, kiongozi wa wakati huo wa Uganda Jenerali Idi Amin Dada aliwapatia wafanyakazi wa Kiingereza waliokuwa wakifanya kazi nchini humo makataa ya siku 12 wakubali kupunguziwa mishahara yao kwa asilimia 40 au waondoke nchini humo. Zoezi hilo liliwajumuisha karibu wafanyakazi 780 wa Kiingereza waliokuwa wakifanya kazi kwenye mashirika mbalimbali nchini Uganda.   ***