Jumanne, tarehe 26 Disemba, 2023
Leo ni Jumanne tarehe 12 Jumadithani 1445 Hijria sawa na tarehe 26 Disemba 2023.
Siku kama ya leo miaka 802 iliyopita kwa mujibu wa kalenda ya Hijria, alifariki dunia Abul Hassan Ali bin Abdu Samad Hamdani, mtambuzi wa lugha, fakihi na mfasiri wa Qur'ani katika karne ya 7 Hijria.
Alizaliwa huko Sakha nchini Misri na akaondokea kuwa mashuhuri kwa lakabu ya Sakhawi. Akiwa na lengo la kujiendeleza kielimu, Abul Hassan Ali bin Abdu Samad alielekea Sham na kuishi Damascus katika Syria ya leo.
Msomi huyo wa Kiislamu ameandika vitabu mbalimbali katika elimu za Tajweed, teolojia na hadithi. Baadhi tu ya vitabu vyake mashuhuri ni pamoja na al Jawahir na Sifrus Sa'ada.

Katika siku kama ya leo miaka 125 iliyopita, Ayatullah Sayyid Ali Husseini Mar’ashi mashuhuri kwa lakabu ya Sayyidul Atibbaa mmoja wa matabibu mahiri wa Iran alifariki dunia.
Alizaliwa katika mji wa Tabriz nchini Iran na baada ya kumaliza masomo ya awali ya kidini alisafiri na kuelekea Najaf Iraq kwa shabaha ya kujiendeleza zaidi kielimu. Sayyid Ali Mar’ashi alisoma kwa kwa walimu mahiri wa zama hizo mjini Najaf na kurejea katika mji aliozaliwa akiwa na shahada ya Ijtihadi. Kutokana na mapenzi yake makubwa na elimu ya tiba alielekea katika mji wa Isfahan na kusoma taaluma hiyo kwa muda wa miaka 15.
Alimu huyo amevirithisha vizazi vilivyokuja baada yake vitabu vingi na vyenye thamani kubwa ambapo Tarikh Tabriz na Sharh Tib al-Nabbi ni baadhi tu ya vitabu vyake muhimu.
Miaka 44 iliyopita katika siku kama ya leo Jeshi Jekundu la Urusi ya zamani liliivamia ardhi ya Afghanistan.
Uvamizi huo wa Russia unatambuliwa na kizazi kipya cha viongozi wa nchi hiyo kuwa ni miongoni mwa makosa makubwa ya ikulu ya Kremlin katika siasa zake za nje. Uvamizi huo wa Urusi ulifanyika kutokana na ombi la Babrak Karmal mmoja wa viongozi wa Afghanistan. Tangu wakati huo Mujahidina wa Afghanistan walianza mapambano dhidi ya jeshi la askari laki moja na 30 elfu la Jeshi Jekundu (Red Army). Katika upande mwingine Marekani ambayo ilitambua kuwepo kwa Urusi ya zamani huko Afghanistan kuwa ni hatari kwa maslahi yake ilianza kuunda makundi ya wapiganaji na kuyasaidia kwa mali na silaha kwa ajili ya kukabiliana na Urusi.
Makumi ya maelfu ya watu waliuawa na wengine kufanywa vilema katika kipindi cha miaka 10 ya uvamizi wa Urusi huko Afghanistan.

Siku kama ya leo miaka 19 iliyopita mtetemeko mkubwa wa ardhi uliokuwa na daraja 9 kwa kipimo cha Rishta ulitokea katika Bahari ya Hindi na kusababisha mawimbi makubwa ya Tsunami.
Mawimbi hayo yalisambaa na kuenea kwa kasi kubwa katika nchi kadhaa za kandokando ya bahari hiyo na kusababisha maafa makubwa. Kitovu cha mtetemeko huo kilikuwa maji ya kusini mashariki mwa Asia na kwa msingi huo nchi za India, Indonesia, Sri Lanka na Thailand ndizo zilizoathiriwa zaidi na mtetemeko huo.
Mawimbi ya Tsunami yaliyosababishwa na mtetemeko huo yalisababisha vifo vya watu wasiopungua laki mbili na elfu 20 na kuharibu nyumba za watu milioni mbili. Nchi hizo pia zilipata hasara ya mamilioni ya dola.

Tarehe 5 Dei mwaka 1382 Hijria Shamsia yaani siku kama hii la leo miaka 20 iliyopita, mtetemeko wa ardhi uliokuwa na nguvu ya 6.8 kwa kipimo cha Rishta ulitokea katika mji wa Bam kusini mwa Iran na maeneo ya kandokando yake.
Mtetemeko huo wa ardhi uliharibu sehemu kubwa ya mji huo na kusababisha vifo vya watu elfu 41. Makumi ya maelfu ya watu wengine pia walijeruhiwa. Maafa ya mtetetemo huo wa ardhi yalikuwa makubwa mno kwa kadiri kwamba baadhi ya jumuiya na taasisi za kimataifa zilijiunga na wananchi na serikali ya Iran katika kutoa misaada ya dharura kwa waathiriwa.
Mbali na hasara za nafsi na vifo vya maelfu ya watu, mtetemeko wa ardhi wa Bam ulisababisha pia hasara kubwa za kiuchumi na kuharibu jengo la kale la Arge Bam.
