Jan 01, 2024 06:27 UTC
  • Ulimwengu wa Spoti, Jan 1

Matukio muhimu ya SPOTI yaliyojiri ndani ya siku saba zilizopiita, kitaifa na kimataifa....

Soka: Iran yajiandaa Kombe la Asia

Timu ya taifa ya soka ya Iran inatazamiwa kushuka dimbani Januari 5 kuvaana na Burkina Faso katika mchuano wa kirafiki, kwa ajili ya maandalizi fainali za Kombe la Asia. Mchuano huo utapigwa katika Uwanja Olympic katika kisiwa cha Kish kusini mwa pwani ya Ghuba ya Uajemi. Kadhalika kikosi hicho cha Iran kinachofahamika hapa nchini kama Team Melli kinatazamiwa kutoana udhia na Indonesia mjini Doha nchini Qatar mnamo Januari 7.

Timu ya taifa ya kandanda ya Iran

 

Vijana hao wa Kiirani wanaonolewa na Amir Ghalenoei wamepangwa katika Kundi C pamoja na Imarati, Palestina na Hong Kong kwenye michuano hiyo ya kibara, huku Indonesia ikiwa katika kikosi kimoja na Japan, Vietnam na Iraq. Mkufunzi Ghalenoei tayari ashakitaja kikosi cha timu ya kandanda ya Iran kinachotazamiwa kuanza kampeni kwa kuchuana na Palestina mnamo Januari 14 katika Uwanja wa al-Rayyan nchini Qatar.

Jinai za Israel; Salah asikitishwa na mauaji ya Gaza

Mchezaji soka nyota wa kimataifa Mohammed Salah, raia wa Misri kwa mara nyingine tena ameeleza kusikitishwa na mauaji ya kutisha yanayoendelea kufanywa na utawala wa Israel katika Ukanda wa Gaza. Katika ujumbe wake wa kheri njema ya Krismasi aliotuma kwenye mitandao ya kijamii, Mo Salah anayeichezea Liverpool ameitaka dunia isiwasahau kamwe wanaowaomboleza wapendwa wao Gaza. Huu ni ujumbe wake wa pili kuhusiana na matukio ya Gaza.

Mo Salah

 

Hapo awali, alitoa mwito wa kusitishwa mauaji hayo ya halaiki huko Gaza, sambamba na kutaka kupelekwa misaada ya kibinadamu katika eneo hilo lililo chini ya mzingiro. Wanamichezo mbalimbali wameendelea kutumia kurasa zao za mitandao ya kijamii kulaani jinai za utawala wa Kizayuni dhidi ya Wapalestina wa Gaza. Mpaka sasa, utawala huo pandikizi umeua shahidi Wapalestina zaidi ya 22,000 katika mashambulizi yake ya kijeshi dhidi ya Gaza tokea Oktoba 7.

Riadha: Mkenya avunja rekodi

Mwanariadha nyota wa Kenya, Beatrice Chebet amefungwa mwaka kimtindo, baada ya kuvunja rekodi ya dunia za mbio za kilomita 5 kwa upande wa wanawake. Chebet aliibuka kidedea katika mbio hizo siku ya Jumapili katika mbio za barabarani za Cursa dels Nassos mjini Bercelona nchini Uhispania, kwa kutumia dakika 14 na sekunde 13. Amemuonyesha kivumbi raia wa Ethiopia Ejgayehu Taye Haylu na Mkenya mwenza Lilian Kasait Rengeruk waliobuka wa pili na tatu kwa usanjari huo.

Rais wa Zanzibar na michezo

Tuelekee huko nchini Tanzania, ambapo Rais wa Zanzibar Dk Hussein Ali Mwinyi amesema serikali ya awamu ya nane inatilia mkazo ujenzi wa viwanja vya michezo mbalimbali ili kutanua wigo wa ajira kutokana na michezo pamoja na kuibua vipaji vya vijana. Amesema azma ya serikali ni kuendeleza michezo katika nyanja zote inatimia kwa kuweka miundombinu ya kisasa iliyobora na imara.

Rais Dk Mwinyi

 

Dk Mwinyi alisema hayo Desemba 30 alipoufungua Uwanja wa Michezo wa Matumbatu uliopo Shehia ya Miembeni, Mkoa wa Mjini Magharibi katika shamrashamra za Miaka 60 ya Mapinduzi ya Zanzibar. Rais Mwinyi amewatoa hofu wananchi wa Malindi kuwa dhamira ya ujenzi wa viwanja hivi ni kuwa mbadala maeneo yaliyofanyiwa uwekezaji. Pia amesema michezo ikitumika vizuri itakuwa ni fursa ya kuitangaza Zanzibar na kukuza utalii.

Dondoo za Hapa na Pale

Tuanze na michuano ya Ligi Kuu ya Soka ya Uingereza, ambapo ndoto ya klabu ya Arsenal ya kutwaa ubingwa wa ligi imeendelea kufifia kutokana na vichapo mtawalia. Siku ya Jumapili, Gunners walichabangwa mabao 2-1 ugenini katika Uwanja wa Craven Cottage jijini London walipochuana na Fulham. Na kwa kuwa kutangulia sio kufika, bao la mapema la Bukayo Saka dakika 5 baada ya kuanza ngoma liliweka kifua mbele Wabeba Bunduki kwa dakika 20 hivi, kabla ya Raul Jimenez kusawazisha mambo kunako dakika ya 29, na kisha Bobby De Cordova-Reid kuipa Fulham la ushindi katika dakika ya 59 ya cmchezo. Katika mechi ya usiku wa kuamkia Desemba 29, klabu ya Arsenal ilirambishwa pia magoli 2-0 na West Ham. Vichapo hivyo vimewatupa Wanabunduki hadi katika nafasi ya 4 kwenye jedwali la EPL wakiwa na pointi 40, sawa na Manchester City. City hiyo imesogea hadi katika nafasi ya tatu baada ya kuicharaza Sheffiled City mabao 2-0 siku ya Jumamosi. Tuiache Liverpool iendelee kutuama kileleni, hasa baada ya mchuano wa Jumatatu dhidi ya New Castle. Kama watani wao Gunners, Manchester United siku ya Jumamosi iliendelea kunyolewa pia kwa chupa kwa kucharazwa mabao 2-1 na Nottingham Forest katika Uwanja wa City Ground. Licha ya kucheza kiume na kumiliki mpira kwa asilimia 55, lakini walijikuta wakibamizwa 2 kupitia Nocolas Dominguez na Morgan Gibbs-White, huku Marcus Rashford akiwapa la kufutia machozi. Mgala muue na haki yake mpe, Mashetani Wekundu hawa Disemba 26 walitoka nyuma kwa maba 2-0 na kupata ushindi wa aina yake wa mabao 3-2 dhidi ya Aston Villa.

Wakati huohuo, bilionea wa Uingereza, Jim Ratcliffe amekubali kununua hisa asilimia 25 za Man U kwa takriban Dola bilioni 1.3. Tajiri huyo mwenye umri wa miaka 71 pia atatoa Dola milioni 300 ambazo sawa na pauni 236 kuwekeza uwanja wa Old Trafford hapo baadaye. Tangazo hilo linakuja miezi 13 baada ya wamiliki wa klabu hiyo, familia ya Glazer, kusema wanafikiria kuuza ili kutafuta mbinu mbadala. Familia hiyo ya Marekani ilinunua klabu hiyo kwa Pauni milioni 790 mwaka 2005. Mzabuni mwingine pekee aliyetangazwa hadharani, mwanabenki wa Qatar Sheikh Jassim bin Hamad Al Thani, aliondoa ofa yake ya kununua 100% ya klabu mnamo Oktoba mwaka huu. United wamekuwa na mwenendo usio mzuri kwa miaka ya hivi karibuni hawajashinda Ligi Kuu tangu 2013, huku mashabiki wakiandamana mara kadhaa kushinikiza kuondoka kwa familia ya Glazer ambao ndio wamiliki wa klabu kwa sasa.

CR7

 

Na nahodha wa klabu ya kandanda ya al-Nassr ya Saudi Arabia, Cristiano Ronaldo ndiye aliyeongoza kwa ufungaji wa mabao mwaka uliomalizika 2023. Jumanne ailiyopita aliifungia klabu yake inayoshiriki Ligi Kuu ya Soka ya Saudia mabao mawili na kufikisha jumla ya mabao 53 kwa mwaka 2023, katika mchuano ambao al-Nassr walipata ushindi wa magoli 5-2 dhidi ya Ittihad.  Raia huyo wa Ureno mwenye umri wa miaka 38 amewapiku Kylian Mbappe wa PSG, Harry Kane wa Beyern Munich, ambao walifunga 52 kila mmoja, huku Erling Halaand wa Man City akifunga mwaka kwa mabao 50.

………………….TAMATI……………