Jan 01, 2024 23:18 UTC
  • Jumanne, tarehe 02 Januari, 2024

Leo ni Jumanne tarehe 19 Jamadithani 1445 Hijria sawa na Januari Pili 2024.

Katika siku kama ya leo miaka 158 iliyopita leo, alizaliwa Gilbert Murray, mshairi na malenga wa Australia.

Akiwa na umri wa miaka 11 Murray alielekea nchini Uingereza na baada ya kumaliza masomo ya juu katika Vyuo Vikuu nchini humo, alifundisha taaluma ya utamaduni na fasihi ya Kigiriki katika Chuo Kikuu cha Oxford.

Murray alifariki dunia mwaka 1957 na kuacha athari za vitabu kadhaa kama vile, 'Historia ya Fasihi ya Ugiriki ya Kale' na 'Imani, Vita na Siasa'. 

Gilbert Murray

Katika siku kama ya leo miaka 104 iliyopita, alizaliwa Isaac Asimov, mwandishi na mkemia maarufu wa Kimarekani aliyekuwa na asili ya Russia.

Asimov alivutiwa mno na elimu ya kemia na akafanikiwa kupata shahada ya uzamivu katika taaluma hiyo. Msomi huyo alifanya utafiti na uhakiki mkubwa wa elimu ya kemia na taaluma nyingine. Hata hivyo jambo lililomtofautisha na wasomi wengine ni uwezo wake wa kuarifisha sayansi mbalimbali kwa lugha nyepesi kwa watu hususan tabaka la vijana. Isaac Asimov ameandika karibu vitabu 270 katika nyanja mbalimbali za sayansi, hisabati na sayansi za jamii. 

Isaac Asimov

Miaka 82 iliyopita katika siku kama ya leo, alifariki dunia Ayatullah Fayyaz Zanjani fakihi na msomi mahiri wa elimu ya Usuul. Awali alisoma masomo yake kwa Mujtahidi Akhund Mullah Muhammad. Baadaye akahudhuria masomo kwa walimu mahiri wa zama hizo mjini Tehran kama Mirza Muhammad Hassan Ashtiyani na kuwa mahiri katika taaluma za fikihi, Usuul, mantiki na tafsiri.

Mwanazuoni huyo alikuwa Marjaa Taqlidi wa Zanjani. Kwa kipindi cha zaidi ya miaka 30 alikuwa mmoja wa waeneza mafundisho ya Ahlul Bait na waalimu wakubwa wa Maktaba ya Ushia.

Ayatullah Fayyaz Zanjani

Katika siku kama ya leo miaka 8 iliyopita yaani tarehe Pili Januari 2016 utawala wa Saudi Arabia ulimuua mwanazuoni wa Kiislamu Sheikh Nimr Baqir al-Nimr. 

Baqir al Nimr aliyekuwa mwanazuoni wa Kiislamu wa madhehebu ya Shia alizaliwa tarehe 21 Juni mwaka 1959 katika mji wa Awwamiyya huko mashariki mwa Saudi Arabia. Alipata elimu ya msingi katika mji huo na mwaka 1400 Hijria yaani mwaka 1989 alielekea Tehran nchini Iran na kupata elimu katika chuo cha kidini cha Qaim kilichoasisiwa na Ayatullah Sayyid Muhammad Taqi Mudarrisi. Baada ya kupata elimu katika chuo hicho kwa kipindi cha miaka 10 Sheikh Nimr alikwenda Syria na kuendelea kutafuta elimu zaidi katika Chuo cha Kidini cha Bibi Zainab (as).

Aliporejea Saudi Arabia, Sheikh Nimr aliasisi kituo cha kidini cha al Imam al Qaim katika mji wa Awwamiyya ambacho kiliweka jiwe la msingi la kuanzishwa Kitiuo cha Kiislamu hapo mwaka 2011. Mwanazuoni huyo wa Kiislamu daima alikuwa akikosoa siasa za ukandamizaji na kibaguzi za utawala wa kifalme wa Saudia na alifungwa jela mara kadhaa kutokana na kusema haki na kweli.

Mara ya mwisho Sheikh Baqir Nimr alikamatwa tarehe 8 Julai mwaka 2012 katika maandamano makubwa ya Waislamu wa Kishia ya kupinga ubaguzi na ukandamizaji wa utawala wa Aal Saud na tarehe 15 Oktoba msomi huyo wa Kiislamu alihukumiwa kifo cha kukatwa kichwa kwa panga na kusulubiwa kadamnasi kwa kile kilichodaiwa kuwa ni kula njama dhidi ya utawala wa nchi hiyo. Hukumu hiyo ilitekelezwa tarehe Pili Januari mwaka 2016.

Kuuawa kwa msomi na mwanaharakati huo kulipingwa vikali na jumuiya za kikanda na kimataifa za kutetea haki za binadamu.

Sheikh Nimr Baqir al-Nimr

Katika siku kama ya leo miaka 3 iliyopita alifariki dunia  Ayatullah Muhammad Taqi Misbah Yazdi.

Misbah Yazdi alizaliwa mwkaa 1313 Hijria Shamsiya katika mji wa Yazd na baada ya masomo ya msingi aliingia katika Chuo cha Kidini cha Shafiiya cha mjini Yazd na akaanza utangulizi wa masomi wa dini ya Kiislamu.  Mbali na masomo hayo ya kidini pia alijifunza fizikia, fiziolojia na lugha ya Kifaransa. Baadaye alielekea mjini Qum kuendeleza masomo ya chini ya wanazuoni wakubwa kama vile Ayatullah Burujerdi, Imam Khomeini, Ayatullah  Araki na Ayatullah Behjat.

Baada ya mapinduzi ya Kiislamu ya Iran mwaka 1979 aliasisi ofisi ya ushirikiano baina ya vyuo vya kidini na vyuo vikuu ili kuleta mabadiliko katika mfumo wa elimu. Aliasisi pia Tassisi ya Elimu na Utafiti ya Imam Khomeini MA mjini Qum na alikuwa mwanachama wa Jumuiya ya Wahadhiri wa Vyuo vya Kidini mjini Qum. Halikadhalika aliwahi kuwa  mjumbe wa Baraza la Wanavyuoni Wataalamu linalomchagua na kusimamia kazi za Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran.

Ameandika vitabu vingi na alikuwa mashuhuri kwa darsa zake za Falsafa. Baada ya umri mrefu wenye baraka na jihadi ya kielimu hatimaye mwaka 1399 Hijria Qamaria aliaga dunia akiwa na umri wa miaka 86 wakati akipata matibabu mjini Tehran.

Ayatullah Muhammad Taqi Misbah Yazdi