Jumapili, 28 Januari, 2024
Leo ni Jumapili 16 ya mwezi Rajab 1445 Hijria mwafaka na 28 Januari 2024 Miladia.
Miaka 45 iliyopita katika siku kama hii ya leo, kundi kubwa la wanazuoni wa Kiislamu lilianzisha mgomo wa kuketi katika msikiti wa Chuo Kikuu cha Tehran baada ya Waziri Mkuu wa serikali ya wakati huo ya Shah, Shapoor Bakhtiyar, kumzuia Imam Khomeini kurejea nchini Iran akitokea uhamishoni. Wanazuoni hao walisema, sharti pekee la kusitisha mgomo huo ni kuruhusiwa Imam Khomeini kurejea nchini. Mgomo huo ulikuwa miongoni mwa matukio muhimu katika historia ya Mapinduzi ya Kiislamu nchini Iran. Kwani kwa upande mmoja, serikali ya wakati huo ya Shah iliyokuwa ikiungwa mkono na Marekani, ilifanya jitihada kubwa za kumzuia Imam Khomeini asirejee nchini, na kwa upande mwingine ilikuwa ikifanya njama za kuzusha hitilafu na migawanyiko kati ya matabaka mbalimbali ya wananchi kwa kutoa ahadi na kutumia vitisho. Mgomo huo wa wanazuoni wa Kiislamu uliowashirikisha maulamaa mashuhuri kama Shahid Ayatullah Murtadha Mutahhari na Ayatullah Muhammad Beheshti, ulikifanya Chuo Kikuu cha Tehran kuwa kituo kikuu cha harakati za mapambano. ***
Siku kama ya leo miaka 45 iliyopita Shapoor Bakhtiyar, Waziri Mkuu kibaraka wa Shah wa Iran alitangaza kwamba ataelekea Paris, Ufaransa kwa shabaha ya kukutana na kufanya mazungumzo na kiongozi wa harakati za Mapinduzi ya Kiislamu Imam Ruhullah Khomeini. Katika upande wa pili, Imam Khomeini alitangaza akiwa Paris kwamba, hamtambui Bakhtiyar kuwa ni Waziri Mkuu wa Iran, tofauti na uvumi uliokuwa ukienezwa wakati huo. Imam alisisitiza kuwa hatampokea wala kuzungumza na Waziri Mkuu wa Shah kabla hajajiuzulu. Siku hiyo hiyo wananchi wa Tehran walikusanyika katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Mehrabad kwa ajili ya kujiandaa zaidi na kutayarisha mipango ya kumpokea Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu Imam Khomeini (MA). ***
Katika siku kama ya leo miaka 11 iliyopita Jamhuri ya Kiislamu ya Iran iliendeleza utafiti wake wa masuala ya anga za mbali kwa kutuma kiumbe hai angani ikitumia roketi. Kiumbe huyo hai alikuwa tumbili ambaye alirejea ardhini salama katika utafiti huo. Majaribio hayo yaliyokuwa na mafanikio yaliwaonesha walimwengu mafanikio na maendeleo ya masuala ya anga ya Iran katika kipindi hicho cha vikwazo vizito vya kidhalimu vya Marekani na waitifaki wake dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu. ***
Siku hii ya leo ya tarehe 28 mwezi Januari, inaadhimishwa kote duniani kama Siku ya Kimataifa ya Kuwasaidia Wagonjwa Wenye Maradhi ya Ukoma. Siku hii ilipewa jina hilo na Raul Follivero, raia wa Ufaransa yapata nusu karne iliyopita. Wakati huo dunia ilikuwa na watu milioni 15 waliokuwa wakisumbuliwa na maradhi hayo. Kufuatia hali hiyo, Shirika la Afya Duniani (WHO) liliiainisha tarehe 28 Januari kuwa Siku ya Kimataifa ya Kupambana na Ugonjwa wa Ukoma. Tangu yalipoanza mapambano dhidi ya ukoma waathirika wa maradhi hayo wamepungua na kufikia watu milioni mbili. Hata hivyo licha ya juhudi hizo, ugonjwa wa ukoma bado haujatokomezwa kikamilifu. ***