Alkhamisi, Februari 29, 2024
Leo ni Alkhamisi tarehe 19 Sha'aban 1445 Hijria mwafaka na tarehe 29 Februari, 2024.
Katika siku kama ya leo miaka 36 iliyopita, baada ya utawala wa Saddam Hussein wa Iraq kushindwa mtawalia katika medani ya vita na Iran, utawala huo wa Baath ulishambulia kwa makombora ya masafa ya mbali makazi ya raia katika mji wa Tehran.
Mashambulio hayo dhidi ya makazi ya raia mjini Tehran katika miji mingine ya Iran yaliendelea kwa muda wa mwezi mmoja ambapo mamia ya watu waliuawa na kujeruhiwa.
Sababu ya kutekelezwa mashambulio hayo dhidi ya makazi ya raia ilikuwa ni kufidia kushindwa kwake utawala wa Saddam Hussein katika medani ya vita na Iran, na kutoa mashinikizo dhidi ya raia na viongozi wa Iran ili wakubaliane na matakwa yake ya kidhalimu na yasiyo ya kiadilifu.

Miaka 43 iliyopita katika siku kama ya leo, Kamati ya Nia Njema ilianza kazi zake mwanzoni mwa vita vya kichokozi vilivyoanzishwa na utawala wa Baath wa Iraq dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.
Kamati hiyo ilianzishwa kwa pendekezo la Mawaziri wa Jumuiya ya Kiislamu na baada ya kupasishwa na wakuu wa jumuiya hiyo ya OIC. Kamati ya Nia Njema ilikuwa na jukumu la kuhitimisha vita vya Iraq dhidi ya Iran kupitia njia ya amani. Kamati hiyo baadaye ilibadilishwa jina na kufahamika kama Kamati ya Amani.

Katika siku kama ya leo, miaka 45 iliyopita, hayati Imam Ruhullah Khomeini kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran aliwasili katika mji wa kidini wa Qum baada ya kuwa uhamishoni kwa kipindi cha miaka 15.
Imam alipelekwa uhamishoni na utawala wa Shah hapo mwaka 1343 Hijria Shamsia baada ya matukio ya umwagaji damu ya tarehe 15 Khordad mwaka 1342. Tarehe 12 Bahman mwaka 1357 Imam alirejea nchini akitokea Ufaransa na katika siku kama ya leo baada ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu aliwasili katika mji mtakatifu wa Qum na kuishi huko.
Miezi kadhaa baadaye Imam Ruhullah Khomeini alihamia Tehran kutokana na udharura wa kuongoza Mapinduzi. *****

Siku kama ya leo miaka 1439 iliyopita kulingana na kalenda ya Hijria, kulijiri vita vya Bani Mustaliq.
Mustaliq ni moja ya makabila ya Khuza'a ambayo yalihamia katika viunga vya mji wa Makka, muda mrefu katika historia. Viongozi wa kabila hilo walieneza ibada ya kuabudu masanamu.
Baada ya Waislamu kusimamisha dola ya Kiislamu mjini Madina, kabila hilo la Mustaliq ambalo liliendelea kuabudu masanamu, lilitangaza utayarifu wake kwa ajili ya kupambana na Waislamu. Kwa sababu hiyo Mtukufu Mtume (saw) akiwa na kundi la wafuasi wake alilazimika kupambana na kabila hilo na hatimaye kulishinda vibaya.