Mar 13, 2024 02:08 UTC
  • Jumatano, Machi 13, 2024

Leo ni Jumatano tarehe Pili Ramadhani mwaka 1445 Hijria inayosadifiana na tarehe 13 Machi 2024 Milaadia.

Siku kama ya leo miaka 1105 iliyopita alifariki dunia Abdur Rahman Zujaji Nahavandi aliyekuwa mwanafasihi, mtaalamu wa lugha na faqihi wa karne ya 4 Hijria katika mji wa Damascus. Alipata elimu kwa wanazuoni wakubwa na mashuhuri wa zama zake kama Ibn Dorayd na akafanikiwa kuwa miongoni mwa wanazuoni wakubwa katika elimu hizo. Miongoni mwa vitabu mashuhuri vya msomi huyo wa Kiislamu ni "al Idhah". 

Siku kama ya leo miaka 291 iliyopita, yaani 13 Machi, 1733 alizaliwa Joseph Priestley, mkemia na mwanafizikia wa Uingereza. Msomi huyo aliishi katika kipindi kilichokuwa maarufu kama zama za dhahabu za kemia na elimu hiyo ilikuwa imepiga hatua. Katika uchunguzi na utafiti wake, Priestley alivumbua uvutaji pumzi katika mimea na gesi za oksijeni na haidrojeni. Joseph Priestley alifariki dunia mwaka 1804.

Joseph Priestley

Miaka 76 iliyopita sawa na tarahe 13 Machi 1948, Wazayuni waliokuwa na mfungamano na kundi la kigaidi la Haganah walishambulia kitongoji cha Wapalestina cha Husseiniyah katika eneo la kaskazini mwa Jalilah. Wazayuni hao licha ya kuwaua shahidi zaidi ya Wapalestina 60, waliharibu nyumba zao kadhaa. Hali kadhalika katika siku hiyo hiyo, wanajeshi wa Israel walizilipua kwa mabomu nyumba za Wapalestina katika eneo la 'Qatmun' lililoko Baitul Muqaddas. Mauaji ya Waislamu wa Palestina yaliyofanywa na makundi ya kigaidi ya Israel yalitekelezwa kwa lengo la kutaka kutangaza uwepo wa utawala huo bandia kwenye ardhi zinazokaliwa kwa mabavu za Palestina baada ya kuondoka vikosi vya majeshi ya Uingereza katika eneo hilo.

Jinai za Israel huko Palestina

Siku kama ya leo miaka 62 iliyopita sawa na tarehe 23 Esfand 1340 Hijria Shamsia, alifariki dunia Ayatullah Sayyid Abul Qassim Kashani, mwanachuoni na shakhsia maarufu wa kisiasa katika historia ya Iran. Ayatullah Kashani alifanikiwa kupata daraja la ijtihadi akiwa bado barobaro huko Najaf nchini Iraq lakini baadaye alifukuzwa nchini humo kutokana na misimamo yake ya kupinga ukoloni wa Uingereza. Aliporejea nchini Iran, Ayatullah Kashani aliendelea na misimamo yake ya kupambana na ukoloni wa Uingereza na kufungwa jela mara kadhaa. Baada ya kutoka jela wananchi wa Tehran walimchagua kuwa mwakilishi katika bunge la Taifa.

Ayatullah Kashani