Mar 29, 2024 02:34 UTC
  • Ijumaa, tarehe 29 Machi, mwaka 2024

Leo ni Ijumaa tarehe 18 Ramadhani 1445 Hijria sawa na tarehe 29 Machi mwaka 2024.

Siku kama ya leo miaka 451 iliyopita, yaani tarehe 29 Machi 1573 Mfalme Charles wa Tisa wa Ufaransa alitoa amri ya kihistoria iliyojulikana kama amri ya uhuru, ambayo ilikuwa kwa maslahi ya Wakristo wa madhehebu ya Protestanti. Kwa mujibu wa amri hiyo, Waprotestanti wa Ufaransa ambao walijipatia ushindi kwenye vita vya nne dhidi ya Wakatoliki wa nchi hiyo, walikuwa huru kufanya sherehe, ibada na misa zao nchini humo. Vita vya nne vya kidini kati ya Wakatoliki na Waprotestanti vilianza tarehe 16 Julai mwaka 1572 na vilikuwa maarufu kwa jina la Vita vya La Rochelle.   

Mfalme Charles wa Tisa wa Ufaransa

Miaka 348 iliyopita katika siku kama ya leo vita baina Poland na Ufalme wa Othmania vilifikia tamati kwa ushindi wa Ufalme huo na kutekwa sehemu ya ardhi ya Ukraine iliyokuwa chini ya utawala wa Poland. 

Siku kama ya leo miaka 252 iliyopita, alifariki dunia Emmanuel Swedenborg, aliyekuwa mwanafikra mkubwa na msomi wa Sweden.

Swedenborg alizaliwa mwaka 1688 na baada ya kubobea kwenye taaluma ya hesabati, aliweza kuwa mhandisi mahiri nchini humo. Swedenborg hakutosheka na elimu hiyo na badala yake akaongeza juhudi kubwa na kutokea kuwa mtaalamu pia kwenye elimu ya falsafa na irfani. Msingi wa falsafa ya msomi huyo ulikuwa kujitenga na dunia ya kimaada na kuingia zaidi katika ulimwengu wa kimaanawi. Kwa msingi huo Swedenborg aliamini kuwa kadiri mwanadamu anavyosafisha roho yake ndivyo anavyomuelewa na kumjua zaidi Mwenyezi Mungu. Mtaalamu huyo aliandika vitabu zaidi ya 50 kwa ajili ya kuweka wazi falsafa yake. 

Emmanuel Swedenborg

Katika siku kama hii ya leo miaka 122 iliyopita sawa na tarehe 29 Machi mwaka 1902 alizaliwa mwandishi wa Kifaransa, Marcel Ayme.

Awali Ayme alisomea uhandisi, hata hivyo aliachana na taaluma hiyo kutokana na kupatwa na maradhi. Baadaye alijishughulisha na uandishi wa magazeti na taratibu akaanza kujihusisha na uandishi wa riwaya ambapo alitokea kuwa mashuhuri katika uwanja huo.

Marcel Ayme ameandika vitabu kadhaa kama "Beautiful Image", na "The Green Mare".

Marcel Ayme

Usiku wa leo tarehe 18 Ramadhani ni usiku wa kuamkia tarehe 19 Ramadhani na unatambuliwa kuwa mojawapo ya usiku zinazotarajiwa kuwa usiku wa Lailatul Qadr ambamo ndani yake iliteremshwa Qur'ani Tukufu, na mambo yote ya mwaka mzima ya waja hukadiriwa katika usiku huo. 

Qur'ani inazungumzia usiku huu katika Sura za Qadr na Dukhan. Usiku wa Lailatul Qadr umetajwa kuwa ni bora kuliko miezi elfu moja, na Malailka wa rehma huteremka na baraka tele kutoka kwa Mola Karima. 

Usiku haswa wa Qadr hauko wazi; Lakini kwa mujibu wa Hadithi nyingi, unatazamiwa kuwa moja ya usiku za kuamkia tarehe 19, 21, 23 au 27 wa mwezi huu wa Ramadhani.

 

Tags