Apr 13, 2024 02:10 UTC
  • Jumamosi, Aprili 13, 2024

Leo ni Jumamosi tarehe 4 Mfunguo Mosi Shawwal 1445 Hijria sawa na Aprili 13 mwaka 2024.

Siku kama ya leo miaka 1094 iliyopita yaani tarehe 4 Shawwal mwaka 351 Hijria alifariki dunia Muhammad bin Hassan Darqutni, aliyekuwa miongoni mwa wanazuoni wakubwa wa Kiislamu wa karne ya nne Hijria.

Darqutni alikuwa miongoni mwa maqari na wafasiri mashuhuri wa Qur'ani wa zama hizo. Mwanazuoni huyo alitumia wakati mwingi wa umri wake kuandika vitabu, na mashuhuri zaidi kati ya vitabu vyake ni "Al Muujamul Akbar" na "al Manasik Wal Maudhi' Fii Maanil Qur'an." 

Siku kama ya leo miaka 105 iliyopita, kulijiri tukio la umwagaji damu mkubwa katika Bustani ya Jallianwala (Jallianwala Bagh Massacre) nchini India.

Mwaka 1919 na kwa lengo la kuzuia uasi na mapambano ya wananchi, serikali ya kikoloni ya Uingereza ilipasisha sheria iliyowapa polisi haki ya kuwatia mbaroni wanaharakati wa India bila sababu yoyote na kuwashikilia kwa muda usiojulikana. Sheria hiyo iliwakasirisha mno wananchi wa India na katika siku kama ya leo zaidi ya Wahindi elfu tano waliokuwa wamekusanyika kwa amani katika Bustani ya Jallianwala katika mji wa Amritsar walimiminiwa risasi kwa amri ya kamanda mmoja wa Uingereza. Watu 1200 waliuawa na wengine 4000 kujeruhiwa katika tukio hilo.

Baada ya mauaji hayo, harakati ya ukombozi wa India ikiongozwa na shujaa Mahatma Ghandhi ilipamba moto. 

Picha ya Jallianwala Bagh Massacre

Tarehe 13 Aprili mwaka 1945 yaani miaka 79 iliyopita, Austria ilidhibitiwa na kukaliwa kwa mabavu na vikosi vya nchi Waitifaki.

Tukio hilo lilijiri katika miezi ya mwisho ya Vita Vikuu vya Pili vya Dunia. Kabla ya Vita Vikuu vya Pili vya Dunia, Austria ilikuwa nchi huru na inayojitawala. Lakini muda mchache baada ya kuanza vita hivyo, Adolph Hitler aliiunganisha ardhi ya nchi hiyo na Ujerumani na wanajeshi wa Austria wakaingia vitani kupigana upande wa Ujerumani. Baada ya Ujerumani kuondoka Austria na nchi hiyo kukaliwa kwa mabavu na madola Waitifaki, iligawanywa katika maeneo matano ambapo kila eneo likadhibitiwa na kuendeshwa na moja ya madola hayo, huku mji mkuu Vienna ukiendeshwa kwa pamoja na madola manne.

Hatimaye mwaka 1946, madola Waitifaki yalitambua rasmi uhuru wa Austria ambapo baada ya kutiwa saini mkataba wa amani kati ya pande mbili, mwaka 1955, majeshi ya nchi waitifaki yakaondoka katika ardhi ya Austria.

Austria

Katika siku kama ya leo miaka 49 iliyopita, shambulio la wanamgambo wa Kikristo wenye misimamo ya kufurutu ada wa kundi la Mafalanja lililolenga basi moja lililokuwa na Wapalestina na kuua watu 30 kati yao, lilipelekea kuibuka vita vya ndani nchini Lebanon.

Kufuatia mauaji hayo, Waislamu na wazalendo wa Lebanon walianzisha mapambano ya kukabiliana na Mafalanja hao. Muda mfupi baadaye harakati za wapiganaji wa Kipalestina pia ziliingia katika vita hivyo vya ndani vya Lebanon.

Vita hivyo ambayo vilikuwa vikichochewa na utawala haramu wa Israel, viliisababishia hasara kubwa ya mali na roho serikali ya Beirut.   

Bndera ya Lebanon

Tarehe 25 Farvardin miaka 36 iliyopita serikali ya wakati huo ya Iraq ilikiri kwamba ilitumia silaha za kemikali katika vita vyake dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.

Katika kipindi chote cha miaka minane ya vita hivyo Iran iliwasilisha mashtaka katika jumuiya za kimataifa kwamba Iraq inatumia silaha za kemikali dhidi ya wapiganaji wa Jamhuri ya Kiislamu. Wakati huo Iraq haikukiri wala kukadhibisha habari hiyo.

Hata hivyo katika siku kama hii ya leo wakati vita vilipokuwa vimepamba moto, serikali ya Baghdad ilikiri kwamba inatumia silaha za kemikali zikiwemo za gesi ya sumu na hatari ya haradali dhidi ya malengo ya kijeshi na kiraia ya Iran.

Katika siku kama ya leo miaka 21 iliyopita, yaani tarehe 13 Aprili 2003, yalifanyika maandamano ya kwanza ya wananchi wa Iraq dhidi ya wavamizi baada ya miongo mitatu ya mbinyo na ukandamizaji ya utawala wa dikteta Saddam Hussein.

Baada ya kuangushwa utawala wa Saddam na chama cha Baath Aprili 9 mwaka 2003 na kisha nchi hiyo kukaliwa kwa mabavu na vikosi vamizi hususan majeshi ya Marekani, maandamano ya kwanza ya wananchi ya kupinga kuvamiwa na kukaliwa kwa mabavu nchi yao yalifanyika.  ***