May 09, 2024 02:25 UTC
  • Alkhamisi, tarehe 9 Mei, 2023

Leo ni Alkhamisi tarehe 30 Shawwal 1445 Hijria sawa na tarehe 9 Mei mwaka 2024.

Siku kama ya leo miaka 370 iliyopita, kazi ya ujenzi wa jengo la Taj Mahal linalohesabiwa kuwa miongoni mwa majengo ya kuvutia zaidi duniani na moja kati ya mifano bora zaidi ya usanifu majengo wa Kiislamu huko India ilimalizika baada ya miaka 22.

Ujenzi wa jengo la Taj Mahal ulianza baada ya kufariki dunia mke wa Shah Jahan, mfalme wa India huko katika jimbo la Agra. Jengo hilo lilijengwa kwa kutegemea ramani iliyochorwa na msanifu majengo mashuhuri wa Iran, Isa Isfahani.

Kwa upande wa nje, jengo la Taj Mahal limenakshiwa kwa ustadi kwa rangi mbalimbali huku kuta zake zikiwa zimeandikwa maandishi ya Kiarabu yenye aya za Qur'ani Tukufu.

Ndani ya jengo hilo kuna makaburi mawili ya mfalme Shah Jahan na mkewe, Nur Jahan.   

Taj Mahal

Tarehe 9 Mei miaka 219 iliyopita aliaga dunia mwandishi, malenga na mwandishi wa michezo ya kuigiza wa Kijerumani kwa jina la Johann Christoph Friedrich von Schiller akiwa na umri wa miaka 46.

Von Schiller alipenda sana masuala ya uandishi tangu utotoni mwake. Friedrich Von Schiller alikuwa hodari katika fasihi ya Kijerumani na anahesabiwa kuwa mmoja kati ya waandishi mahiri wa Kijerumani katika uga wa fasihi.   

Johann Christoph Friedrich von Schiller

Miaka 108 iliyopita katika siku kama ya leo ya tarehe 9 Mei, mkataba wa kihistoria wa Sykes-Picot ulitiwa saini na wawakilishi wa Uingereza, Ufaransa na Urusi ya zamani. Hata hivyo Umoja wa Kisovieti baadaye ulijitoa kwenye makubaliano hayo baada ya mapinduzi ya Bolshevik.

Kwa mujibu wa makubaliano hayo, tawala za Uingereza na Ufaransa ziligawana nchi za Kiarabu zilizokuwa chini ya mamlaka ya utawala wa Kiothmania. Kwa msingi huo Iraq na Jordan zikawa chini ya udhibiti wa Uingereza huku Syria na Lebanon zikitawaliwa na Ufaransa. *

Miaka 35 iliyopita katika siku kama ya leo, Dakta Sayyid Jawad Mustafavi mwandishi, mhakiki na mhadhiri wa zama hizi wa Kiirani alifariki dunia. Awali alisoma masomo ya kidini sambamba na kufanya utafiti katika fani mbalimbali katika uwanja huo. Jawad Mustafavi alibobea mno katika elimu za kidini. Baada ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu nchini Iran aliteuliwa kuwa mkuu wa Chuo Kikuu cha elimu za dini mjini Mash'had. Aidha msomi huyo hakuwa nyuma katika uga wa kualifu vitabu. Miongoni mwa vitabu vyake mashuhuri ni al-Kashif na Miftaful al-Wasail.

Dakta Sayyid Jawad Mustafavi

 

Tags