May 12, 2024 02:29 UTC
  • Jumapili, 12 Mei, 2024

Leo ni Jumapili tarehe 3 Mfunguo Pilii Dhul-Qaadah 1445 Hijria sawa na tarehe 12 Mei 2024 Mildia.

Siku kama ya leo miaka 204 iliyopita, alizaliwa Florence Nightingale, mwanzilishi wa uuguzi wa kisasa huko Florence nchini Italia. Nightingale aliyejulikana kwa jina mashuhuri la 'mwanamke mwenye taa mkononi' alikuwa muuguzi na mwanahesabati mashuhuri wa Uingereza. Alipewa lakabu ya 'mwanamke mwenye taa mkononi' kutokana na uvumilivu wake mkubwa na kujinyima usingizi kwa ajili ya kuwahudumia wagonjwa nyakati za usiku. Alifanya juhudi kubwa kwa ajili ya kuboresha huduma za afya katika hospitali nyingi nchini Uingereza. Kazi hiyo aliyoifanya kwa miaka mingi bila kuchoka ilimdhoofisha sana kimwili kwa kadiri kwamba, alipofuka macho mwishoni mwa umri wake, na hatimaye aliaga dunia tarehe 13 Agosti 1910. ***

Florence Nightingale

 

Siku kama ya leo miaka 79 iliyopita, Berlin mji mkuu wa Ujerumani iligawanywa katika sehemu mbili za Mashariki na Magharibi. Kwa mujibu wa mapatano yaliyofikiwa baada ya kumalizika Vita vya Pili vya Dunia kati ya nchi nne zilizoikalia kwa mabavu Ujerumani, mji huo uligawanywa na kudhibitiwa na Russia, Ufaransa, Uingereza na Marekani. Muda mfupi baadaye mji huo ulizingirwa na Urusi ya zamani. Harry Truman rais wa wakati huo wa Marekani alichukua uamuzi wa kuvunja mzingiro na udhibiti huo wa Urusi. Katika kutekeleza hatua hiyo Marekani ilikaribia kupigana vita na Urusi. Matokeo mengine ya mgogoro huo ilikuwa kugawanywa Ujerumani katika sehemu mbili za Ujerumani Magharibi na Mashariki. ***

Picha inayoonyesha ujenzi wa ukuta wa Berlin

 

Katika siku kama ya leo miaka 45 iliyopita kulingana na kalenda ya Hijria Shamsiya, mkataba wa kutoshtakiwa Wamarekani nchini Iran au Capitulation Accord ulifutwa nchini kufuatia mapambano yasiyosita ya wananchi Waislamu wa Iran, ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Kiislamu na kuasisiwa mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu. Kwa mujibu wa sheria za mkataba huo, raia wa Marekani aliyekuwa nchini Iran alikuwa na kinga kamili ya kisheria dhidi ya kufunguliwa mashtaka. Kwa kadiri kwamba hakuna taasisi au chombo chochote cha kisheria cha Iran kilichokuwa na mamlaka ya kumfungulia mashtaka na kumhukumu raia wa Marekani aliyekuweko Iran na kesi za raia hao wa Kimarekani zilipaswa kusikilizwa katika nchi yao. ***

 

Miaka 16 iliyopita, katika siku kama ya leo, tetemeko lenye ukubwa wa 7.9 kwa kipimo cha Rishta, liliukumba mji wa Sichuan ulioko kusini magharibi mwa China. Katika tetemeko hilo la kutisha watu wapatao 87,000 walifariki dunia na wengine laki tatu na 80,000 kujeruhiwa. Tukio hilo la kutisha liliwaacha mamilioni ya watu bila makazi.***

 

 

Tags