May 01, 2024 04:37 UTC
  • Jumatano, tarehe Mosi Mei, mwaka 2024

Leo ni Jumatano tarehe 22 Shawwal 1445 Hijria, inayosadifiana na tarehe Mosi Mei, mwaka 2024.

Siku kama ya leo miaka 135 iliyopita yaani tarehe Mosi Mei 1889, ilitangazwa rasmi kuwa 'Siku ya Wafanyakazi Duniani'.

Tarehe Mosi Mei 1886, zaidi ya wafanyakazi elfu 40 walifanya maandamano katika mji wa Chicago nchini Marekani kwa shabaha ya kudai haki zao. Wafanyakazi hao walitaka nyongeza za mishahara, kuboreshwa suhula za maeneo yao ya kazi na uadilifu kazini. Maandamano hayo yaliingiliwa na askari polisi, na matokeo yake yakawa ni idadi kadhaa ya wafanyakazi hao kuuawa na wengine kujeruhiwa. 

Siku kama ya leo miaka 109 iliyopita, sawa na tarehe Mosi Mei 1915, wakati wa Vita vya Kwanza vya Dunia yalitokea mapigano makali kati ya majeshi ya Urusi na Ujerumani katika eneo la Krakow lililoko nchini Poland.

Jeshi la Ujerumani lililoyashinda majeshi ya Urusi kwenye Vita vya Kwanza vya Dunia mwaka 1914, katika vita hivyo kwa kutumia mizinga liliyashinda majeshi ya Urusi na hatimaye kulidhibiti eneo la Poland. Kushindwa kwa majeshi ya Urusi katika Vita vya Kwanza vya Dunia na hali kadhalika hali mbaya iliyokuwemo nchini humo, ni miongoni mwa sababu muhimu za kujiri mapinduzi ya Kikomonisti nchini humo mwaka 1917, na hatimaye nchi hiyo kujiondoa kwenye Vita vya Kwanza vya Dunia.  ***

Miaka 45 iliyopita katika siku kama ya leo, mwafaka na tarehe 12 Ordibehesht 1358 Hijria Shamsia, mwanachuoni na mwanafikra mashuhuri wa Kiislamu, Ayatullah Murtadha Mutahhari, aliuawa shahidi na kundi lililokuwa dhidi ya Mapinduzi la Furqan hapa nchini.

Tukio hilo lilitokea katika kipindi cha chini ya miezi mitatu baada ya kupata ushindi Mapinduzi ya Kiislamu nchini Iran. Shahidi Mutahhari alijistawisha kielimu kutoka kwa maulamaa wakubwa wakiwemo Ayatullahil Udhma Burujerdi, Allamah Tabatabai na Imam Ruhullah Khomeini MA, mwasisi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran. Ayatullah Murtadha Mutahhari ameandika makumi ya vitabu katika taaluma mbalimbali.

Na miaka 19 iliyopita katika siku kama hii, tarehe Mosi Mei 2004, nchi nyingine 10 za Ulaya zilijiunga na Umoja wa Ulaya na kufikisha jumla ya nchi 25 wanachama wa umoja huo.

Nchi hizo ni Estonia, Latvia, Lithuania, Poland, Jamhuri ya Czeck, Slovakia, Hungary, Slovenia, Cyprus, na Malta. Licha ya kuwa kujiunga nchi hizo kulihesabiwa na jumuiya hiyo kuwa moja ya mafanikio, lakini kuna ufa wa kisiasa, kiuchumi na kijamii kati ya nchi wanachama wa zamani na wapya.

Vilevile mwaka 2007, nchi za Romania na Bulgaria zilijiunga na umoja huo na jumla ya nchi wanachama wa Umoja wa Ulaya kufikia 27.