May 03, 2024 08:15 UTC
  • Tuujue Uislamu (15)

Ni wasaa na wakati mwingine wapenzi wasikilizaji tunapokutana katika sehemu nyingine ya kipindi hiki cha Tuujue Uislamu.

 

Kipindi chetu cha wiki pia kitaendelea na maudhui ya tawhidi na kumtambua Mwenyezi Mungu. Kuweni nami hadi mwisho wa kipindi hiki, hii ikiwa ni sehemu ya 15 ya mfululizo huu.

 

Katika Aya nyingi za Qur'an, Mwenyezi Mungu anataja uumbaji wa kipekee wa mwanadamu na anauchukulia uumbaji wake pamoja na maajabu yake yote kuwa ni dalili za elimu na uwezo Wake usio na kikomo. Mfano mmojawapo wa uwezo na mpango mkuu wa Mungu ni kumuumba mwanadamu katika tumbo la uzazi la mama. Mwanzoni, kijusi hakina viungo na sehemu, lakini kwa kasi ya ajabu, inachukua sura mpya na jukumu kila siku. Ni kana kwamba kikundi cha wachoraji na mafundi stadi hufanya kazi juu yake usiku na mchana kwa ajili ya kukiunda ili kwa muda mfupi kiweze  kutoka katika chembe hii ndogo na kuwa kiumbe ambaye muonekano wake ni mzuri na ndani yake kuna mifumo tata na ya kushangaza. Muhtasari wa kuumbwa mwanadamu unaonyesha kwamba, yeye ni mojawapo ya matukio mazuri sana katika ulimwengu na kwamba Mungu ameonyesha uwezo wa ajabu katika kuumba kiumbe hiki. Mwenyezii Mungu anaashiria dhama na nguvu Yake hii ya uumbaji katika Surat al-Muuminun Aya ya 12-14

Na kwa yakini tumemuumba mtu kutokana na asili ya udongo. Kisha tukamjaalia awe tone ya mbegu ya uzazi katika kalio madhubuti. Kisha tukaiumba tone kuwa damu iliyo ganda, na tukaiumba damu kuwa pande la nyama, kisha tukaliumba pande la nyama kuwa mifupa, na mifupa tukaivika nyama. Kisha tukamfanya kiumbe mwengine. Basi ametukuka Mwenyezi Mungu Mbora wa waumbaji.

Wakati kijusi kinapokuwa tayari kwa ajili ya kuchora na kuunda umbo, kila kikundi cha seli za jicho, sikio, ubongo na viungo vingine kinachukua kazi yake maalumu na kuanza jitihada zisizo na mwisho. Qur'an inabainisha kwamba je, mabadiliko haya ya ajabu yanaweza kukubaliwa na dhana ya kukana Mungu? Inawezekanaje kwamba seli za mwili zikawa zinajua wajibu wao na kufuata lengo lao kwa usahihi na utaratibu huo bila meneja mwenye ufahamu na mwenye busara? na kimsingi, kiumbe wa ajabu kama mwanadamu akajitokeza? Je haya yote yanafanyika bila ya muongozo, usimamiajii na uendeshaji? Mwenyezi Mungu anasema kuhusiana na hili katika Surat al-Hashr Aya ya 24 kwamba:

Yeye ndiye Mwenyezi Mungu, Muumbaji, Mtengenezaji, Mtia sura, Mwenye majina mazuri kabisa. Kila kilioko katika mbingu na ardhi kinamtakasa, naye ni Mwenye kushinda, Mwenye hikima.

 

Imamu Sadiq (a.s.) ambaye ni miongoni mwa Ahlul-Bayt wa Mtume (saww) alisema hivi kwa mmoja wa wanafunzi wake aitwaye Mufadhal kuhusu kuumbwa kwa mwanadamu: Ewe Mufadhal! Kwanza, kijusi huundwa ndani ya tumbo la mama, ambapo hakuna jicho linaloweza kukiona na hakuna mkono unaoweza kukifikia. Hatua hii ya kupanga inaendelea hadi kijusi kinakamilika na kila kiungo kinachohitaji huundwa ndani yake. Kisha kiumbe huyu anatia mguu katika ulimwengu huu. Katika mwili wa mwanadamu, kuna kila kitu cha siri na cha dhahiri, yaani kinachoonekana na kisichoonekana. Kuanzia viungo hadi mifupa, nyama, ubongo, mishipa na gegedu au tishu. Viungo vyote vya mwili vinakua sawa na kila kimoja kwa namna ambayo umbo la viungo hivyo halibadiliki na idadi yake haiongezeki wala kupungua. Kukua kwa kichanga tumboni hakupeleki kuongezeka idadi ya macho yake, miguu, vidole au mikono.

Kama mnnavyojua, muundo wa viumbe hai wote duniani una vitengo vidogo vinavyoitwa seli. Seli ni msingi wa maisha ya mimea na wanyama. Mwili wa mwanadamu pia unajumuisha vitengo hivi vidogo vya kimuundo. Idadi ya seli katika mwili wa binadamu ni kubwa sana. Kikundi cha seli ambazo ni sawa katika muundo na ziko kwa ajili ya kazi fulani, huunda tishu. Kuna aina tatu za seli za damu, ambazo ni seli nyekundu, seli sahani pamoja na seli nyeupe. Kwa idadi seli nyeupe ndizo zilizo chache kuliko seli nyingine zote.

Seli nyeupe hufanya kazi ya kupambana na viini vya magonjwa mbalimbali. Viini vya magonjwa huweza kuwa vijidudu, bakteria au virusi. Seli nyeupe hufanya kama askari wa mwili. Viini vya magonjwa vinapoingia mwilini huanza kushambulia kwanza seli nyeupe za damu. Hivyo kama seli hizo ni dhaifu basi ni rahisi mwili kushambuliwa na viini hvyo. Mpangilio huu katika mwili wa mwanadamu ni moja ya ishara za wazi za kuweko Muumba wa mwanadamu huyu.

 

Mfano mwingine ni mfumo wa mzunguko wa damu. Mzunguko wa damu unafikisha mwilini mwote virutubishi, oksijeni, homoni na seli za damu ili kulisha, kukinga dhidi ya maradhi, pamoja na kudhibiti halijoto na uwiano kwa jumla. Damu ni chombo cha kusafirisha mahitaji ya seli kama vile virutubishi na oksijeni pale panapohitajika, halafu inapokea dutu zisizohitajika tena kutoka seli na kuzipeleka kwa viungo zinapoondolewa mwilini.

Kwa mamalia pamoja na binadamu mfumo wa mzunguko wa damu kwa jumla huwa na pande mbili: Mzunguko wa damu wa mwili wote ("systemic circulation")

mzunguko wa damu wa mapafu ("pulmonary circulation") unaopitisha damu kwenye mapafu wa kusudi la kuondoa hewa chafu na kuingiza oksijeni

Hapana shaka kuwa, utendaji huu makini wa mzunguko wa damu, mapigo ya moyo, mfumo imara wa seli, upumuaji na mengineyo katika mwili wa mwanadamu ni ishara za wazi za uwepo wa muendeshaji wake ambaye si mwingine bali ni Mola Muumba.

Qur'an inaufasiri ulimwengu wa ndani wa mwanadamu kuwa ni nafsi; chanzo cha kufikiri kwenye faida na kugundua ukweli na uhakika wake. Anasema katika Aya ya 53 ya Surat Fussilat:

Sema: Mnaonaje! Ikiwa haya yanatoka kwa Mwenyezi Mungu, nanyi ikawa ndio mmeyakataa, ni nani aliye potea zaidi kuliko aliye katika upinzani wa mbali?

 

Wapenzi wasikilizaji kutokana na kumalizikak muda wa kipindi hiki, sina budi kukomea hapa kwa leo. Tukutane tena wiki ijayo katika sehemu nyingine ya mfululizo huu.

Wassalaam Alaykum Warahmatullahi Wabarakaatuh