Jumamosi, 18 Mei, 2024
Leo ni Jumamosi 9 Mfunguo Pili Dhul-Qaadah 1445 Hijria sawa na 18 Mei 2024 Miladia.
Siku kama ya leo miaka 220 iliyopita, Baraza la Seneti la Ufaransa lilimpasisha Napoleon Bonaparte kuwa mfalme wa Ufaransa na kwa utaratibu huo kwa mara nyingine tena mfumo wa kidikteta ukatawala nchi hiyo ikiwa ni miaka 15 imepita baada ya ushindi wa Mapinduzi makubwa ya nchi hiyo ya bara Ulaya. Hata hivyo, mfumo wa kifalme ulifikia mwisho miaka kumi baadaye, sawa na tarehe 11 Aprili mwaka 1814, baada ya Napoleone kushindwa katika vita vyake na nchi za Ulaya na kubaidishwa. ***
Miaka 194 iliyopita katika siku kama ya leo, ilianza operesheni ya jeshi la Ufaransa kwa shabaha ya kuikalia kwa mabavu Algeria. Kisingizio cha Charles wa Kumi mfalme dikteta wa wakati huo wa Ufaransa cha kutoa amri ya kufanywa mashambulio hayo, ni eti vitisho vilivyokuwa vimetolewa miaka mitatu kabla na mtawala wa wakati huo wa Algeria akiitaka Ufaransa ilipe deni la nchi hiyo la Franc milioni saba. Hata hivyo, kinyume na ilivyodhania Paris, wananchi wa Algeria walisimama kidete katika kukabiliana na mashambulio hayo. Ijapokuwa Ufaransa ilifanikiwa kuikalia kwa mabavu Algeria na kupora maliasili na utajiri wa nchi hiyo, hatimaye nchi hiyo ya Kiafrika ilijipatia uhuru wake mwaka 1962. ***
Katika siku kama ya leo miaka 152 iliyopita, alizaliwa Bertrand Russell mwanafalsafa na mwanahesabati mashuhuri wa Uingereza. Russell alijiunga na Chuo Kikuu cha Cambridge mjini London baada ya kumaliza masomo yake ya awali. Alikuwa mpinzani mkubwa wa Vita vya Kwanza na vya Pili vya Dunia na vita vya Marekani dhidi ya Vietnam, na hata kufikia hatua ya kufungua mashtaka dhidi ya viongozi wa Marekani ambayo yaliyopewa jina lake la Russell. Mwaka 1950 msomi huyo alitunukiwa tuzo ya fasihi ya Nobel na alifariki dunia mwaka 1970. ***
Siku kama ya leo miaka 50 iliyopita, sawa na tarehe 18 Mei 1974, India ilifanya jaribio la kwanza la kombora lake la nyuklia katika jangwa la Rajasthan, karibu na mpaka na Pakistan. Kwa utaratibu huo baada ya nchi za Marekani, Russia, Uingereza, China na Ufaransa, India inakuwa nchi ya sita kwa kuwa na nguvu za nyuklia duniani. Miaka 24 baadaye yaani mwaka 1998 India ilifanya majaribio mengine matano ya nyuklia na kufanikiwa kutengeneza silaha za atomiki. ***
Na katika siku kama ya leo miaka 47 iliyopita, kwa mujibu wa azimio la Mkutano wa Kumi na Mbili wa Baraza Kuu la Kamati ya Kimataifa ya Makumbusho, siku hii iliainishwa na kutangazwa kuwa "Siku ya Makumbusho Duniani." Moja ya malengo muhimu ya baraza hilo lilikuwa kupanuliwa makumbusho katika kona mbalimbali duniani, kuweko ushirikiano wa kila upande wa majumba ya makumbusho ulimwenguni kwa malengo ya kiutamaduni na wakati huo huo kuzuia kuangamizwa athari za kale za kiutamaduni. Ni vyema kuashiria hapa kwamba, lengo la kuanzishwa sehemu kwa jina la makumbusho ni kuhifadhi athari za kale za vizazi vilivyopita kwa ajili ya vizazi vijavyo. ***