May 23, 2024 11:01 UTC
  • Tuujue Uislamu (17)

Ni wasaa na wakati mwingine wapenzi wasikilizaji tunapokutana katika sehemu nyingine ya kipindi hiki cha Tuujue Uislamu.

Katika kipindi cha wiki hii, tutamalizia darsa na maudhui ya maajabu ya uumbwaji wa mwanadamu kwa kuangalia utendajikazi tata wa ubongo na Mfumo wa mmeng'enyo wa chakula; ingawa mambo mengi yatakuwa yamebakia na hayajazungumziwa katika suala hili. Kuweni nami hadi mwisho wa dakika hizi chache za kipindi hiki, hii ikiwa ni sehemu ya 17 ya mfululizo huu.

 

Bila shaka  sote tuna kumbukumbu nyingi za zamani na hata utoto wetu, Je, kumbukumbu hizi huhifadhiwa na kuainishwa vipi katika akili zetu? Je tumewahi kujiuliza kuhusu mfumo wa kumbukumbu ambao ni wa ajabu na wa kushangaza? Kwa nini katika hali ya kawaida mwanadamu huonyesha radiamali ya haraka anapokabiliwa na hatari kama vile kuungua ngozi ya mikono? Ni nini humfanya mwanadamu aonyeshe radiamali na kutoa jibu la ghafla katika tukio kama hili? Bila shaka mwanadamu ana mambo mengi aliyojifunza na ambayo ameyahifadhi na hajayasahau.

Kitovu na kituo cha mafunzo haya kiko wapi? Unapojifunza ujuzi fulani, unadumishaje ujuzi huo maishani mwako? Ubongo ndio kitovu cha mambo haya yote tuliyoyataja. Ubongo ni mojawapo ya zawadi kuu za Mwenyezi Mungu, na ndiye kamanda mkuu wa mwili wa mwanadamu. Kiungo hiki muhimu cha mwili, kina uzito wa takriban wa gramu 1400, na kiko kwenye kichwa cha binadamu na kati ya mifupa ya fuvu. Fuvu la kichwa cha binadamu ni kama ngao au kofia inayolinda ubongo dhidi ya majeraha na mapigo.

Ubongo hudhibiti mifumo mingine ya viungo vingine vya mwili, iwe kwa kusisimua misuli au kwa kusababisha kutolewa kwa kemikali kama vile homoni. Udhibiti huu kutoka mahali moja unaruhusu majibu ya haraka na yaliyoratibiwa kwa mabadiliko katika mazingira. Ubongo ni kiunganishi kati ya mwili na mazingira ya nje, na vile vile kitovu cha fikra za mwanadamu na shughuli za kiakili. Tishu za ubongo zimeundwa na mabilioni ya seli za neva, ambapo kazi na utendaji wake ni wa kushangaza. Ubongo una mambo na vifaa vya kusaidia mwili kuwasiliana na mazingira ya nje. Karakana za hisi tano, kila moja ikiwa na muundo wake wa kushangaza, hushirikiana na ubongo kwa uangalifu sana na kuanzisha uhusiano wa kibinadamu na ulimwengu wa nje.

 

Mfano mwingine ni jicho. Jicho huona mtazamo wa vitu kutoka nje na huchukua picha zao kwa kifaa maalum sawa na kamera. Kisha, kwa mwendo wa kasi, inapeleka picha hiyo kwenye ubongo. Ubongo wa binadamu unawakilisha 2% tu ya uzito wa mwili, unapokea 15% cha kinachozalishwa na moyo, 20% ya jumla ya matumizi ya oksijeni mwilini, na 25% ya jumla ya matumizi ya glukosi mwilini.

Licha ya hayo, lakini inashangaza kuwa, ubongo una uwezo wa kupokea habari nyingi kwa wakati mmoja, mapokezi ya habari hii kutosababisha maingiliano na kuvuruga utendajikazi wake. Kwa mfano, wakati ubongo unapopokea habari kupitia macho, haupuuzi ripoti za vifaa vingine vya mawasiliano na huchunguza kwa uangalifu na kuchambua yote ili kufanya uamuzi muhimu. Kwa sababu hii, ni lazima tukubali kwamba Mungu ameumba kiwanda cha ajabu na sahihi zaidi ulimwenguni katika kiungo kidogo kiitwacho ubongo. Katika ubongo wa mwanadamu, kuna vituo ambavyo hudhibiti kwa njia ya automatiki vitendo visivyo vya hiari, kama vile kituo kinachohusiana na kupumua na harakati za mapafu, mienendo ya moyo na shughuli za tumbo na utumbo na viungo vingine vya mwili. Vitendo hivi bila hiari vinadhibitiwa kwa uangalifu na kwa ustadi.

Mfano mwingine ni Mfumo wa mmeng'enyo wa chakula ambao nao ni moja ya viungo vyenye umuhimu mkubwa katika mwili wa mwanadamu. Mfumo wa mmeng'enyo wa chakula ni jumla ya viungo mwilini mwa binadamu na mamalia wengine vinavyofanya kazi ya kuingiza chakula mwilini, kukisagasaga, kukisafirisha ndani ya mwili, kukimeng'enya, kuondoa lishe ya mwili ndani yake, na kutoa mabaki nje ya mwili. Kwa hiyo mfumo wa mmeng'enyo wa chakula ni njia yote kuanzia mdomo hadi sehemu ya haja kubwa.

Ili chakula kiweze kutumika mwilini, ni lazima kivunjwevunjwe kiwe katika hali rahisi ya kuweza kusharabiwa. Kazi hiyo hufanywa na mfumo wa mmeng’enyo wa chakula. Sehemu kuu zinazohusika katika umeng’enyaji huo ni kinywa, umio, mfuko wa tumbo, ini, mfuko wa nyongo, utumbo mwembamba, kongosho, utumbo mpana na puru.

 

Chakula kinaposafiri katika njia yake hufanyiwa mabadiliko ya kiumbo na ya kikemikali. Kila sehemu ya mfumo wa mmeng’enyo wa chakula ina kazi maalumu. Chakula cha mnyama au binadamu huweza kuwa cha wanga, protini, mafuta au mchanganyiko wa viambato hivyo. Myeyuko wa makundi hayo ya vyakula hutokea katika sehemu mbalimbali za njia ya chakula kwa njia za kemikali. Kazi ya mmeng’enyo wa chakula hufanyika hatua kwa hatua na kuna viungo ambavyo vinahusika moja kwa moja katika kufanikisha zoezi hili. Kinywa ni sehemu ya kwanza kupokea chakula. Chakula kinapokuwa mdomoni huvunjwavunjwa na kusagwa na meno au kwa lugha nyingine husagwa kimekanika. Mate husaidia kukilainisha. Ulimi husaidia kugeuzageuza chakula hicho na kukiviringisha kuwa tonge. Meno huvunjavunja chakula kuwa vipande vidogovidogo wakati wa kutafuna na kusaga.

Hivyo chakula huwa katika vipandevipande ambavyo huongeza eneo zaidi kwa shughuli za umeng’enyaji zinazofanywa na vimeng’enya vinavyopatikana katika njia ya chakula. Vilevile meno husaidia kufanya chakula kuwa rahisi kumezwa. Kwa msaada wa ulimi, tonge husukumwa kuelekea kwenye umio. Chakula kinapoingia katika umio, huelekea kwenye mfuko wa tumbo. Vyakula rojorojo hupita kwa haraka zaidi kuliko vyakula vizito.

Chakula huhifadhiwa katika mfuko wa tumbo. Mfuko huo una uwezo wa kupanuka wakati unapopokea chakula na kusinyaa unapokuwa hauna chakula. Chakula huwa katika tumbo mwa muda wa saa tatu hadi nne. Muda huo hutegemea aina ya chakula. Chakula cha kabohaidreti, kwa mfano uji wa mahindi huwa tumboni kwa muda usiozidi saa moja. Chakula cha protini kwa mfano nyama, huweza kukaa tumboni kwa muda wa saa moja au mbili.  Je mpangilio wote huu makini na ambao hufanyika hatua kwa hatua, inawezekana kwamba, umetokea hivi hivi tu pasi na kuweko muumba na msimamizi wa yote haya? Bila shaka kuna Muumba na msimamizi wa yote haya na mpangilio huu makini ni ishara nya wazi ya kuweko Muumba.

 

Wapenzi wasikilizaji muda wa kipindi chetu kwa leo umefikia tamati, tyukutane tena wiki ijayo katika sehemu nyingine ya mfululizo huu.

Wassalaam Alaykum Warahmatullahi Wabarakaatuh