Hikma za Nahjul Balagha (52)
Bismillahir Rahmanir Rahim. Assalaamu Alaykum wasikilizaji wapenzi. Karibuni katika sehemu hii ya 52 ya mfululizo wa makala hizi fupifupi za Hikma za Nahjul Balagha. Leo pia tutaangalia kwa muhtasari hikma nyingine za Imam Ali bin Abi Talib AS kama ilivyonukuliwa kwenye kitabu cha Nahjul Balagha tukiwa na matumaini mtakuwa nasi hadi mwisho wa kipindi. Ingawa hii ni sehemu ya 52 ya mfululizo huu, lakini hikma tunayoichambua ni ya 45.
لَوْ ضَرَبْتُ خَیْشُومَ الْمُؤْمِنِ بِسَیْفِی هَذَا عَلَى أَنْ یُبْغِضَنِی مَا أَبْغَضَنِی، وَ لَوْ صَبَبْتُ الدُّنْیَا بِجَمَّاتِهَا عَلَى الْمُنَافِقِ عَلَى أَنْ یُحِبَّنِی مَا أَحَبَّنِی وَ ذَلِکَ أَنَّهُ قُضِیَ، فَانْقَضَى عَلَى لِسَانِ النَّبِیِّ الْأُمِّیِّ (ص) أَنَّهُ قَالَ: یَا عَلِیُّ لَا یُبْغِضُکَ مُؤْمِنٌ وَ لَا یُحِبُّکَ مُنَافِقٌ
Lau nitampiga muumin kwa upanga wangu huu ili anichukie hawezi kunichukia na lau nitamminia mnafiki dunia yote na mpambano yake ili anipende, hatonipenda. Na hiyo ni kutokana na yalliyoamuliwa na Allah kupitia Mtume ummiyyi SAW aliposema: Ewe Ali! Muumin hakuchukii wewe na mnafiki kamwe hakupendi.
Katika Hekima ya 45, Imam Ali AS anataja uhakika mmoja wa ajabu ambao athari zake zinaonekana katika tarikhi na sira yote ya Imam katika umri wake wote. Katika hikma hii, Imam Ali AS anasema, hata ingetokezea kumshambulia muumin kwa upanga wake, basi muumin huyo asingeweza kumchukia kabisa kwa sababu muumin hamchukii Imam Ali AS na lau angemfanyia wema mkubwa kiasi gani mnafiki, mnafiki huyo angeendelea kumchukia Imam AS kwani munafik hawezi kumpenda Imam Ali AS.
Tunajifunza kwenye hadithi hii tukufu kwamba, Imam Ali mwenyewe kama yeye na sifa zake aali na tukufu ni kipambanuzi baina ya muumin na mnafiki. Waumini wa kweli huwa wanajipamba kwa sifa za mtukufu huyo. Kila muumin wa kweli anakubwa na mapenzi makubwa kwa Imam Ali AS lakini wanafiki hata wafanye vipi, hawawezi kumpenda Imam Ali kwani sifa na dhati yao inakinzana kikamilifu na sifa na dhati ya Imam Ali AS.
Tunamuona hapa Imam AS anasema: Hata ingetokezea nimemshambulia muumin kwa upanga, basi muumin huyo hawezi kunichukia kwani atakuwa anajua kwa dhati kuwa nikufanya hivyo bure. Na kama ingetokezea nimpe mnafiki dunia yote na vilivyomo ili anipende, hawezi kunipenda kwani nguvu za taasubu, chuki na uadui ndani yake dhidi ya Imam ni kubwa kuliko dunia na vilivyomo.
Cha kuzingatia zaidi hapa ni kwamba, kumepokewa hadithi nyingine kutoka kwa Bwana Mtume Muhammad SAW kwamba kumpenda Imam Ali bin Abi Talib AS ni kipimo cha kuwa muumin na kumchukia ni ushahidi wa kuwa mnafiki. Mfano mmoja ni ile hadithi iliyopokewa kutoka kwa Abu Said al Khudri iliyomo kwenye vitabu kama Ansab al-Ashraf cha Ahmad bin Yahya Baladhri, mwanahistoria ya karne ya kwanza ya Hijria ambacho kimejikita kwenye nasaba za Waarabu na kitabu cha Sunan cha Abu Isa Muhammad Tirmidhi na ambacho ni miongoni mwa vitabu muhimu vya Hadith vinavyotegemewa sana na Waislamu wa Kisuni. Kwa mujibu wa vitabu hivyo, Abu Said al Khudri amesema: Sisi jamii ya Ansari wa Madina tulikuwa tukiwajua wanafiki kwa chuki zao kwa Ali bin Abi Talib. Hadithi nyingine ni ile inayosema: Siku moja Mtume wa Allah aliwatangazia masahaba wake vielelezo vya mtu kuwa muumin na mtu kuwa munafiki na mwisho wa hadhithi hiyo ndefu kidogo, Mtume alimwashiria Imam Ali AS na akasema yeye ndiye kielelezo na kipimo cha kumpenda Allah kikwelikweli na yeye ndiye kielelezo pia cha kumjua mnafiki na adui wa Allah.
Wassalaamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakaatuh.